Hikma za Nahjul Balagha (1) + SAUTI
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika mfululizo huu mpya wa makala fupifupi. Jina la mfululizo huu ni Hikma za Nahjul Balagha. Ni matumaini yetu mtanufaika vya kutosha na makala hizi.
Wapenzi wasikilizaji, semi fupi fupi za Amir al Muuminin Ali bin Abi Talib AS ndani ya kitabu cha Nahjul Balagha zimejaa hikma ambazo ni vigumu kuzipata mfano wake isipokuwa ndani ya Qur'ani na katika maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Semi hizo zinazungumzia maudhui tofauti kama kumtambua Mwenyezi Mungu, masuala ya fiqhi, maadili bora, masuala ya kijamii na kisiasa na kila kitu ambacho kinamuhusu mwanadamu katika masuala yake mbalimbali. Hiki ni kipindi cha kwanza cha mfululizo huu na tutajadili ndani yake matamshi ya Imam Ali AS ambayo yanasema:
کُنْ فِی الْفِتْنَةِ کَابْنِ اللَّبُونِ- لَا ظَهْرٌ فَیُرْکَبَ وَ لَا ضَرْعٌ فَیُحْلَبَ
Kuwa katika fitna kama ndama wa ngamia, hana mgongo wa kupandwa wala kiwele cha kukamuliwa maziwa. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

Mpenzi msikilizaji, baadhi ya wakati huzuka fitna katika jamii na mambo yakawa yamechanganyikana kiasi kwamba mtu anashindwa kujua haki iko upande gani. Wakati huo busara ni mtu kusubiri hadi vumbi liondoke na uhakika udhihirike, asifanye pupa. Wakati jua la haki litakapokuwa limeng'ara, hapo tena huwa si sahihi kukaa kimya bali ni wajibu kuiunga mkono haki. Lakini wakati mwingine katika fitna, haki haionekani kabisa hata mtu akisubiri vumbi liondoke. Katika fitna hiyo, makundi yote yanayogombana huwa hayako kwenye haki. Wakati huu ndipo mtu anapotakiwa kuwa macho, asiruhusu kutumiwa vibaya na upande wowote ule.
Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib AS katika hikma ya kwanza cha Nahjul Balagha anazungumzia fitna hii ya pili kwa kusema:
کُنْ فِی الْفِتْنَةِ کَابْنِ اللَّبُونِ- لَا ظَهْرٌ فَیُرْکَبَ وَ لَا ضَرْعٌ فَیُحْلَبَ
Kuwa katika fitna kama ndama wa ngamia, hana mgongo wa kupandwa wala kiwele cha kukamuliwa maziwa.
Katika hikma hii, Imam Ali AS anawaambia watu, wakati zinapotokea fitna baina ya pande za batili, wewe kuwa kama ndama wa ngamia, usikubali kabisa kutumiwa vibaya na upande wowote ule. Lakini ili kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu maneno hayo ya hikma ya Imam Ali AS, tunapenda hapa kuzungumzia maneno mawili, ibnu labun na fitna. Ibnu labun ni ndama dume wa ngamia mwenye umri wa miaka miwili ambapo kutokana na kuwa kwake dume, huwa hana kiwele cha maziwa. Ndama wa miaka miwili hana nguvu za kuwabeba wengine, hivyo mtu hawezi kumtumia kwa kumpanda mgongoni wala kumkamua maziwa.
Amma neno fitna maana yake kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ni maneno ya kuleta ugomvi, uadui, chuki na uchochezi. Maana nyingine katika lugha nyingine fitna ni fujo machafuko, kulaghai na kupotosha watu. Katika khutba ya 50 ya Nahjul Balagha, Imam AS anasema, chanzo cha fitna zote ni kufuata hawaa na matamanio ya nafsi. Mara nyingi katika fitna za kisiasa na kijamii, utapata kuna makundi mawili ya batili ambayo kila moja linataka kumzidi nguvu mwenzake. Wanaanzisha fujo na uchochezi katika jamii mpaka inakuwa vigumu kwa watu kujua wafuate upande upi. Wakati huo inabidi wananchi wawe macho sana ili wasije wakatumbukia kwenye mtego wa kundi lolote lile. Imam Ali AS anasema, katika fitna ya namna hiyo, ni wajibu wa kila mtu kutoruhusu kutumiwa vibaya iwe ni kwa njia ya moja kwa moja au kwa namna isiyo ya moja kwa moja.
Mifano ya fitna hizo ni mingi, zikiwemo zile zilizotokea sana katika karne ya kwanza cha Uislamu. Maimamu maasumu na wafuasi wao walikuwa wakijiepusha na fitna hizo. Vita vya Umawiyyun na Zubeiriyyun ni mfano wa wazi wa fitna zilizosimama juu ya batili. Abdullah bin Zubeir ambaye wakati fulani alikuwa adui wa Imam Ali AS na ni katika wasababishaji wakubwa wa vita vya Jamal, alidai ukhalifa kwa madai ya kupigania kisasi cha damu ya Imam Husain AS. Katika upande wa pili wa fitna hiyo, alikuweko Yazid na Bani Umayya ambao ndio waliomuua Imam Husain AS. Waislamu wengi waliuawa katika vita baina ya makundi hayo mawili, wakati makundi yote yalikuwa katika batili na yalichojali ilikuwa ni kupigania madaraka tu.
Tab'an kama tulivyosema mwanzoni mwa kipindi hiki, Imam Ali hapa hakukusudia kusema wasisaidiwe Waislamu na wapigania haki wakati kundi la batili linapowashambulia. Kwani Aya ya 9 ya Surat al Hujurat imesema wazi kwamba: Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh