Nov 23, 2022 02:43 UTC
  • Jumatano tarehe 23 Novemba 2022

Leo nu Jumatano tarehe 28 Rabiuthani 1444 Hijria sawa na Novemba 23 mwaka 2011.

Miaka 806 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus. Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka, Halab (Aleppo) na Baghdad, na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Ibn Arabi alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al-Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".

Katika siku kama ya leo miaka 532 iliyopita, alizaliwa Mirza Sharaf Jihan Qazvini, mshairi mahiri wa Kiirani. Alizaliwa katika mji wa Qazvin moja ya miji ya Iran. Alisoma kwa Amir Ghiyath Din mwanazuoni mashuhuri wa zama hizo. Mirza Sharaf Jihan mbali na kubobea katika elimu za akili na nakili na kuzifundisha alikuwa mwalimu pia katika taaluma za fasihi na mashairi.

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita Jagadish Chandra Bose, msomi mtajika wa Bangladesh alifariki dunia. Jagadish alizaliwa Novemba 30 mwaka 1858 katika moja ya maeneo ambayo ni viungwa vya mji mkuu Dhaka. Miongoni mwa elimu alizokuwa amebobea Jagadish nii fizikia, sayansi ya mimea na akiolojia. Hata hivyo umashuhuri wa Jagadish Chandra Bose unatokana na kuvumbua kwake Radio na tanuri ya miale (Microwave). 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.

André Malraux

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, yaani tarehe 23 Novemba mwaka 1996, ndege ya abiria ya Ethiopia iliyokuwa imetekwa nyara ilianguka katika fukwe za Bahari ya Hindi huko nchini Comoro baada ya kuishiwa na mafuta. Ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia aina ya Boeing 767 ilikuwa na abiria 175. Abiria 125 walipoteza maisha yao katika ajali hiyo. Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi.