Dec 20, 2022 11:12 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 7 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya Saba.

وَ الصَّدَقَهُ دَوَاءٌ مُنْجِحٌ وَ أَعْمَالُ الْعِبَادِ فِی عَاجِلِهِمْ نُصْبُ أَعْیُنِهِمْ فِی آجَالِهِمْ:

Kutoa sadaka ni dawa yenye matunda mazuri, na matendo ya waja katika dunia hii, yataonekana mbele ya macho yao kesho.

Mara nyingi, wakati maumivu yanapotujia, unatuona tunafanya kila kitu ili kuondoa maumivu hayo, lakini maumivu hayo hayaondoki. Mara nyingi pia tumeshuhudia maumivu yakiponywa na kitu ambacho hatukukitarajia kabisa na huwa hata hatukufikiria kwamba maumivu hayo yangeponywa na jambo hilo. Moja ya mambo ambayo Uislamu umeyausia sana na kuyapa kipaumbele, ni sadaka kwani sadaka si tu ni tiba ya maumivu, lakini pia huepusha mabalaa mengi.

 

Naam, sadaka ni dawa ya ajabu kwa maumivu yote. Sadaka inaweza kutibu maumivu na ugonjwa wowote kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Haijalishi maumivu hayo ni ya kimaada au ya kimwili au ya kiroho! Sadaka ni dawa kwa kila mtu. Ina manufaa muhimu kwa kila mmoja wetu. Tofauti na dawa nyingine nyingi za madaktari au njia tofauti zinazotumiwa na wanadamu kujaribu kuondoa matatizo, na ambazo baadhi ya wakati tunaziona zikizidisha tu maumivu na matatizo yaliyopo au kusababisha maumivu na ugonjwa mpya, lakini sadaka kwa upande wake haina madhara wala hasara yoyote.

Mtu anapotoa sadaka hhuwa ameingia katika kanuni jumla ya Aya ya 60 ya Sura Al-Rahman isemayo: هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ Hivi yaweza kuwa malipo ya ihsni isipokuwa ihsani? Je! malipo ya anayefanya ihsani yanaweza kuwa kitu kingine isipokuwa wema na ihsani? Kwa kweli, mtu anapowatendea wema na hisani wengine, huwa ameitanua njia ya kupokea msaada wa Mwenyezi Mungu na inakuwa ni rahisi kuondolewa na Allah maumivu na matatizo aliyo nayo.

Inabidi hapa tukumbuke jambo moja muhimu sana. Nalo ni kuwa "sadaka" si msaada wa kifedha tu na haiishii tu kwenye kuingiza fedha za msaada katika hesabu ya benki ya familia fulani ya watu maskini na wenye shida. Bali, inawezekana pia kutoa sadaka kwa mikono mitupu yaani bila ya kutoa hata senti moja. Ingawa misaada ya kifedha ni muhimu sana na ni jambo linalostahiki kushukuriwa na kupongezwa, lakini lililo muhimu zaidi, ni kitendo kizuri na cha kupendeza kinachofanyika katika jamii ya wanadamu. Kwa mfano, jiwe dogo tunaloliondoa njiani, kwenye kichochoro au barabarani ili watu wasijikwae, au tabasamu tunalompa mzee kwa upendo, au tunapomtuliza mtoto anayelia kwa kumpa pipi au kumbembeleza, au kupuna kichwa cha mtoto yatima kuonesha mapenzi na kumtuliza moyo wake n.k, yote hayo ni aina fulani ya sadaka. Kwa sharti kwamba uifanye ibada hii kwa ikhlasi na usafi wa moyo kabisa, kwa sababu neno lenyewe la sadaka chimbuko lake ni kufanya kitu kiuaminifu kiukweli na kwa ikhlasi. 

Kuwasaidia wanyonge

 

Baada ya Imam Ali AS kuelezea umuhimu wa sadaka, anaendelea na hotuba yake iliyosheheni busara kwa kusema: “Amali za waja katika dunia hii zitaonekana mbele yao kesho siku ya Kiyama”. Kama tunavyojua; hii haina maana kuwa mtu katika dunia hii akitoa fedha ya sadaka na kumpa masikini atakwenda kuziona fedha hizo huko Akhera, bali maana yake ni kuwa atapata malipo mazuri kwa kitendo chake hicho chema cha kuwatatulia watu matatizo yao. Labda hapa ni vyema tutoe mfano ili kuivuta karibu zaidi taswira ya suala hili. Kwa mfano mtu anapotumia neno moja tu la nakupenda kumueleza mwenzake, ijapokuwa neno hilo ni moja tu na sirefu, lakini athari yake kwa roho ya mwenzake aliyemwambia neno hilo ni kubwa na ya kustaajabisha. Sadaka pia huenda aliyetoa hakutoa kitu kikubwa mbele ya macho ya watu, lakini athari yake ni kubwa sana na inatibu maumivu makubwa na itakuwa na matunda bora Siku ya Kiyama. Qur’ani Tukufu katika Aya za 7 na 8 ya Surat az Zilzal inatukumbusha jambo hili kwa njia nyingine na kusema: Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anayetenda chembe ya uovu atauona!

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.