Hikma za Nahjul Balagha (8) + SAUTI
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 8 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya Nane.
اِعْجَبُوا لِهَذَا اَلْإِنْسَانِ یَنْظُرُ بِشَحْمٍ وَ یَتَکَلَّمُ بِلَحْمٍ وَ یَسْمَعُ بِعَظْمٍ وَ یَتَنَفَّسُ مِنْ خَرْمٍ:
Mshangaeni mwanadamu huyu, anaona kwa kipande cha mafuta (yaani jicho), anazungumza kwa kipande cha nyama (yaani ulimi) anasikia kwa mfupa (yaani sikio lenye mifupa), na anapumua kwa tundu.
Baadhi ya wakati kueleza jambo jepesi tu humpeleka mtu kwenye kiwango cha juu cha ufahamu na kutambua ukweli na uhakika wa mambo. Hikma za Nahjul Balagha ni miongoni mwa maudhui hizo zinazobainisha mambo kwa lugha nyepesi lakini yenye maana pana na mafundisho makubwa. Hapa Imam Ali (AS) anavuta hisia na mazingatio yetu kwa kutaja nukta zinazoonekana kuwa rahisi na za kawaida lakini zenye maana pana. Kila nukta ni bahari ya hikma na maarifa. Katika hikma hii ya nane, Imam Ali AS anasema: "Mshangaeni mwanadamu huyo, anaona kwa kipande cha mafuta, anazungumza kwa kipande cha nyama, anasikia kwa kipande cha mfupa na anapumua kwa tundu yaani pua."
Imam Ali AS hapa anasema: Jiangalie! Fikirieni enyi wanadamu jinsi mnavyoweza kuona kila kitu na kipande cha mafuta! Jicho ni mafuta mepesi sana ambayo kamera zote za kisasa kabisa za picha na video haziwezi na hazitowahi kufikia nguvu na kazi tata ya jicho. Kipande hiki cha mafuta, hakihitaji filamu ya kuwekwa ndani yake, wakati mwingine hufanya kazi yake ya upigaji picha kwa miaka sabini au themanini bila ya kuchoka, na kinachovutia zaidi ni kwamba picha na filamu zake zote ni za kiwango cha juu mno. Wakati sehemu inapokuwa na mwangaza mkubwa, jicho hujipanga vizuri na kupokea mwanga mchache na wakati mwangaza unapokuwa mchache, jicho hujipanga vizuri kwa kupokea mwangaza mwingi zaidi kulingana na mazingira alipo mtu. Maajabu mengine ya jicho ni kwamba, mara kwa mara huwa linapwesa kutokana na unyevunyevu na chemchemu ndogo sana za machozi. Kama suala hili la kupwesa lisingelikuwepo, bila ya shaka unyevunyevu uliomo ndani ya jicho ungelikauka na kumfanya mtu apoteze nguvu zake za kuona.
Msikilizaji mpenzi, hebu jiangalie! Hebu kaa kidogo utafakari jinsi unavyozungumza kwa kipande cha nyama yaani ulimi! Kaa ufikiri, vipi kipande hiki cha nyama kinaweza haraka sana kubadilisha makhraj za herufi unazozungumza tena hata katika lugha tofauti?! Je, umekaa na kufikiria muujiza na neema hii kubwa ya Allah? Wakati wa kutamka neno, ulimi hufanya haraka sana kubadilisha muundo na nafasi yake mdomoni, huenda mbele na nyuma na kulia na kushoto na juu na chini kwa haraka sana ili kwenda sambamba na herufi za neno linalotamkwa. Unaona tunauamrisha ulimi utamke herufi Z kwa mfano na chini ya sekunde moja tunauamrisha utoke kwenye Z uje kwenye B kwa mfano na yote hayo yanatekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kipande hiki cha nyama kilichomo mdomoni. Hiyo ni kazi ya kutamka neno moja fupi. Hebu sasa fikiria hali inakuwaje wakati wa kusoma makala au kutoa hotuba? Ulimi huu una nguvu kiasi gani na ni nani aliyeupa nguvu hizo kama si Mwenyezi Mungu? Ulimi ukiteleza kidogo tu hukosea na maneno huparaganyika. Lakini nguvu za ulimi ni kubwa kiasi kwamba, mtu anapododosa au anapokuwa na kigugumizi, huwafanya watu wengine wamwangalie kwa namna nyingine kutokana na uwezo mkubwa wa ulimi wa kutamka maneno. Lakini je umekaa na kumshukuru Allah aliyekupa neema hii kubwa ya ulimi?
Msikilizaji mpenzi, kaa tena na utafakari! Jiangalie! Fikiria jinsi unavyosikia kwa kipande cha mfupa. Mawimbi ya sauti hupitia kwenye kiwambo cha sikio na hutetemeka vipande vitatu vya mfupa mdogo na kutufanya kusikia na kuelewa haraka sana bila ya hata kukiona kinachotoa sauti hiyo.
Hebu kaa tena na utafakati! Je, umewahi kuzifikiria tundu mbili za pua yako unazopumulia? Mwenyezi Mungu ameweka upana wa tundu hizo kwa kiwango bora na kinachohitajika kwa kila mtu. Lau kama tundu hizo zingelibanwa, mtu huyo angekosa pumzi na lau kama tundu hizo ni pana kupindukia, hewa ya nje ingeliingia mwilini mwake na kwenda kuharibu mapafu yake.
Katika hekima hii, Amirul-Mu’minin, Ali bin Abi Talib AS, anatuhimiza tuzingatie mambo ambayo kijuujuu yanaonekana mepesi lakini mazingatio yake ni makubwa sana. Ametuhimiza tuzingatie hayo ili tusisahau kwamba njia ya kumfikia Mwenye Mungu si lazima kuwa ya hoja tata za kifalsafa. Naam! Ikiwa mtu ana macho ya kuona ukweli, maumbile ya mwili wake yanatosha kumuona Allah katika kila nukta na kukiri wajibu wa kumuabudu na kumshukuru. Qur'ani Tukufu inasema katika aya ya 21 ya Surat al Dhariyat kwamba: Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.