Mar 18, 2023 22:48 UTC
  • Jumapili, 19 Machi, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 26 ya mwezi Shaaban 1444 Hijria mwafaka na tarehe 19 Machi 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1339 iliyopita, alifariki dunia, Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa wakati huo. Yazid bin Abdul-Malik aliingia madarakani baada ya kufariki dunia Omar bin Abdul-Aziz hapo mwaka 101 Hijiria. Kiongozi huyo mbali na kufanya dhulma na ukandamizaji, hakuzingatia pia masuala ya Waislamu. Kwa kuzingatia kuwa alikuwa ni mtu wa karibu na ukoo wa Hajjaj Thaqafi, hivyo aliwapa umuhimu mkubwa watu wa ukoo huo. ***

Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan,

 

Siku kama ya leo miaka 689 iliyopita, alifariki dunia Ibn Fasih, aliyekuwa faqihi, malenga na mtaalamu mashuhuri wa lugha ya Kiarabu, huko mjini Damascus, Syria. Baada ya kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha ya Kiarabu, alianza kujifunza elimu ya Hadithi na kuwa gwiji katika uwanja huo. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa na kiwapa kikubwa cha kutunga mashairi. Ameandika vitabu mbalimbali kuhusu maudhui tofauti. ***

Ibn Fasih,

 

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita alizaliwa Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza. Sir Haworth alifanya utafiti na uhakiki mwingi wa kisayansi kuhusu haidrokaboni na akafanikiwa kubuni mpango mpya kwa ajili ya muundo wa molekuli ya sukari. Vilevile Sir Haworth alifanya utafiti na majaribio kuhusu vitamini C ambayo muundo wa molekuli yake unashabihiana na sukari na akatayarisha aina yake ya kutengenezwa viwandani kwa jina la asidi askobiki. Mwaka 1937 Sir Norman Haworth alitunukiwa tuzo ya kemia ya Nobel kutokana na uhakiki na utafiti wake mkubwa. Alifariki dunia mwaka 1950. ***

Sir Norman Haworth

 

Katika siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, Frederic Joliot mwanafizikia na mwanakemia wa Kifaransa alizaliwa huko Paris. Baada ya kusoma masomo yake ya Chuo Kikuu alifanikiwa kuwa msaidizi wa Marie Curie mwanafizikia na mvumbuzi wa radiamu. Baadaye alimuoa binti ya Marie Curie ambapo akishirikiana mkewe walifanikiwa kugundua mpangilio mpya wa radiactive. Frederic Joliot aliaga dunia mwaka 1958. ***

Frederic Joliot

 

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Machi 1987 alifariki dunia Louis de Broglie, ambaye alikuwa wa mwisho katika kizazi cha waasisi wa fizikia ya kisasa akiwa na umri wa miaka 95. Louis de Broglie alizaliwa mwaka 1892 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia alianza utafiti wa elimu ya fizikia. Mtaalamu huyo wa fizikia wa Ufaransa alitatua masuala mengi ya elimu hiyo kwa nadharia yake mashuhuri ya Wave Particle Duality. Mwaka 1929 alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel. ***

Louis de Broglie