Jumanne, tarehe 21 Machi, mwaka 2023
Leo ni Jumanne tarehe 28 Shaaban 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Machi mwaka 2023.
Leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1402 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi Machi 21 (yaani tarehe Mosi Farvardin) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama sikukuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

Katika siku kama ya leo miaka 814 iliyopita alifariki dunia Ibn Hajib, mtaalamu wa Hadithi na mwanahistoria maarufu wa Kiislamu. Ibn Hajib alizaliwa mwaka 593 Hijiria huko Damascus, Syria na kuelekea kwenye miji tofauti kwa ajili ya kusomea elimu ya Hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa wakati huo. Alitambuliwa kuwa gwiji wa elimu ya Hadithi katika zama zake kutokana na umahiri wake mkubwa katika taaluma hiyo. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa.

Siku kama ya leo miaka 255 iliyopita inayosadifiana na 21 Machi 1768, alizaliwa Joseph Baron Fourier mwanahisabati na mwanafizikia mashuhuri wa Ufaransa. Baron Fourier alikuwa ni miongoni mwa wahadhiri wa mwanzoni kabisa waliofundisha somo la hesabati mara baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Paris.
Katika siku kama hii ya leo miaka 98 iliyopita barua rasmi za serikali ya Iran zilianza kuandikwa kwa kutumia tarehe ya mwaka wa Hijria shamsia kufuatia azimio lililopasishwa na Bunge la Taifa. Kwa utaratibu huo kalenda ya Iran ilibadilika kutoka mwaka wa Hijria Qamaria na kuwa Hijria Shamsia. Mwanzo wa miaka hiyo miwili ya Qamaria na Shamsia ni mmoja yaani hijra na tukio la kuhama Mtume (saw) kutoka Makka na kwenda Madina katika mwaka wa 13 baada ya kupewa utume (mwaka 622), lakini mwaka wa Qamaria unahesabiwa kwa kuzunguka mwezi mara 12 kandokando ya sayari ya dunia, na mwaka wa Shamsia unahesabiwa kwa dunia kuzunguka jua mara moja. Kwa kuwa mwaka wa Hijria Shamsia una siku 365, kila mwaka huwa na siku 11 zaidi ya mwaka wa Hijria Qamaria ambao huwa na siku 354.

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku ya mauaji ya umati dhidi ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini yaliyotokea mwaka 1960 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kufuta Ubaguzi wa Rangi". Waafrika weusi wapatao 69 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa katika siku kama ya leo, baada ya askari makaburu kuwafyatulia risasi watu hao waliokuwa wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga siasa za ubaguzi wa rangi.Japokuwa sera za ubaguzi wa rangi zimefutwa nchini Afrika Kusini lakini ubaguzi na ukosefu wa usawa vingali vinashuhudiwa katika sura mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali ya dunia hususan katika nchi za Magharibi.

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano makubwa kati ya harakati ya PLO ya Palestina na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Karama ulioko Jordan. Kwa uchache wanajeshi 1,230 wa Kizayuni waliangamizwa na makumi ya vifaru kutekelezwa au kuchukuliwa ngawira na wanamapambano wa Kipalestina kwenye mapigano hayo. Harakati ya PLO ilianza kupoteza hadhi yake ya kimapambano baada ya kulegeza misimamo yake ya kimapinduzi mwaka 1991 na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani na utawala ghasibu wa Israel; mazungumzo ambayo hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina.

Tarehe 21 Machi 1990, nchi ya Namibia ilipata uhuru na kujitenga na Afrika Kusini. Mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni wa Kijerumani, Uingereza na Ureno walianza kuvutana kwa minajili ya kudhibiti na kupora utajiri na maliasili za Namibia. Uhuru wa Namibia ulipatikana kutokana na mapambano ya harakati ya SWAPO chini ya uongozi wa Sam Nujoma.
