Ijumaa terehe 24 Machi 2023
Leo ni Ijumaa tarehe Pili Ramadhani 1444 Hijria sawa na 24 Machi mwaka 2023.
Miaka 117 iliyopita katika siku kama leo, alifariki dunia mwandishi wa hadithi wa Kifaransa Jules Verne akiwa na umri wa miaka 77. Verne alizaliwa Februari mwaka 1828 na alifanikiwa kuandika vitabu vingi na vya kuvutia vya hadithi ambapo ndani yake alielezea utabiri wake kuhusu ustawi wa sayansi ya mwanadamu. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na vitabu alivyoviita Twenty Thousand Leagues Under the Sea, A Journey to the Center of the Earth na Around the World in Eighty Days. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, filamu mbalimbali zenye kutoa mafunzo kwa watoto na vijana zilitengenezwa kwa mujibu wa baadhi ya hadithi hizo za Jules Verne.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, yaani sawa na tarehe 4 Farvardin 1365 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ustadh Amir Hussein Yazdgerdi akiwa na umri wa miaka 57. Yazdgerdi alikuwa miongoni mwa wataalamu wa elimu ya fasihi wa Iran. Sambamba na kufundisha katika chuo kidogo cha al-Hayat cha mjini Tehran, alikuwa pia mhariri wa baadhi ya majarida kwa kushirikiana na Ustadh Forouzanfar, ambaye pia alikuwa kati ya magwiji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi. Kazi muhimu ya Yazdigerdi ilikuwa kusahihisha, kufanya uchunguzi na kusherehesha vitabu vya watafiti wengine hususan kwenye uwanja wa historia.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Msikiti Mkuu wa mji wa Ganja ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Azerbaijan ulikarabatiwa na kufunguliwa upya baada ya kufungwa kwa miaka 70. Msikiti huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1920 na kufunguliwa tena katika muongo wa 80 katika hafla iliyofanyika sambamba na kuswaliwa Swala ya jamaa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, makumi ya misikiti ilikarabatiwa na kutumiwa na Waislamu kufuatia matukio ya kisiasa yaliyotokea Urusi ya zamani na katika jamhuri zake na pia kutokana na matakwa ya Waislamu wote wa Jamhuri ya Azerbaijan.
Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na kifua kikuu au Tuberculosis. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 daktari Robert Koch daktari na mtafiti wa Kijerumani alieleza uvumbuzi wake wa ugonjwa wa kifua kikuu katika mkutano uliofanyika Berlin na kwa mnasaba huo siku hii ya tarehe 24 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kifua Kikuu.
