Mar 27, 2023 22:41 UTC
  • Jumanne, tarehe 28 Machi, 2023

Leo ni tarehe 6 Ramadhani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 28 mwezi Machi mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 981 iliyopita, yaani tarehe 6 Ramadhan 463 Hijiria, alifariki dunia Allamah Hamza Ibn  Abdul-Aziz Dailami, maarufu kwa jina la Sallar Dailami, mmoja wa wataalamu wa kubwa wa sheria za Kiislamu (fiqhi). Sallar Dailami alifariki dunia mjini Tabriz, moja ya miji ya kaskazini magharibi mwa Iran. Alikuwa ni mkazi wa mji wa Tabaristan, kaskazini mwa Iran huku lakabu yake ikiwa ni Abu Ali. Aidha Sallar alikuwa ni mmoja wa wanafunzi mashuhuri wa Sheikh Mufid na Sayyid Murtadha Alamul-Huda. Athari mashuhuri ya msomi huyo ni kitabu cha 'Al-Maraasimul-Alawiyyah wal-Ahkaamun-Nabawiyyah' pamoja na kitabu kingine kinachoitwa 'jawaamiul-Fiqhi.' Aidha miongoni mwa athri nyingine za Allamah Hamza Ibn  Abdul-Aziz Dailami ni kitabu kinachoitwa 'Al-Abewaab wal-Fusuul' na 'At-Taqriib.'

Kaburi la Allamah Hamza Ibn  Abdul-Aziz Dailami

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Russia Alexei Maximovich Peshkov aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Maksim Gorky. Gorky alilazimika kusoma na wakati huo huo akifanya kazi ili kuweza kukidhi mahitaji yake ya maisha kutokana na umaskini mkubwa uliokuwa ukimkabili. Alianza kuandika riwaya haraka sana na kufanikiwa kuchapisha riwaya yake ya kwanza katika gazeti la Tbilisi wakati alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya reli. Miaka miwili baadaye mwandishi Gorky alipata mafanikio makubwa ambapo alichapisha riwaya yake katika kitabu na taratibu akaanza kuingia katika safu ya waandishi wakubwa na mashuhuri duniani.

Maksim Gorky

Katika siku kama leo miaka 84 iliyopita, baada ya kupita karibu miaka miwili na nusu ya vita vya ndani huko Uhispania, wapigania usultani chini ya uongozi wa Jenerali Francisco Franco waliwashinda wapigania jamhuri na kudhibiti Madrid, mji mkuu wa nchi hiyo. Machafuko yalianza huko Uhispania wakati Alphonso wa 13 mfalme dikteta wa nchi hiyo alipolazimika kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya wapigania jamhuri na baadaye mfumo wa jamhuri ukaasisiwa huko Uhispania.

enerali Francisco Franco

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita mwandishi wa Kiingereza, Bi Virginia Woolf aliaga dunia kwa kujiua. Woolf alizaliwa mwaka 1882 na alianza kufaidika na maktaba binafsi ya baba yake ambaye alikuwa mwandishi na mkosoaji wa fasihi, akiwa bado mtoto. Virginia Woolf alianza kuandika vitabu mapema na miongoni mwa vitabu hivyo ni Mrs. Dalloway, The Waves na To the Lighthouse. Hata hivyo maradhi ya kiakili na kinafsi yaliyompata akiwa bado kijana yaliendelea kumuandama na hatimaye mwandishi huyo wa Uingereza aliamua kujiua katika siku kama hii ya leo.

Virginia Woolf