Jumatano, tarehe 29 Machi, mwaka 2023
Leo ni Jumatano tarehe 7 Ramadhani 1444 Hijria sawa na tarehe 29 Machi mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka wa 10 tangu kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume (saw) katika mji wa Makka. Baada ya kufariki dunia Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad (saw), Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na alisimama imara kukabiliana na washirikina wa Kikureishi. Lakini baada ya kufariki dunia Abu Talib washirikina walishadidisha maudhi na manyanyaso yao dhidi ya Bwana Mtume (saw), kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alilazimika kuhama Makka na kwenda kuhamia Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1243 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ma'mun, khalifa wa utawala wa Bani Abbas alimlazimisha Imam Ridha (as) kukubali matakwa yake ya kuwa mrithi wa kiti cha ufalme baada yake. Ni vyema kuashiria kuwa uadui wa watawala wa kizazi cha Bani Umayyah na Bani Abbas dhidi ya Ahlul Bait wa Mutume (saw) ni wa muda mrefu. Vizazi hivyo viwili ni maarufu kwa dhulma, ukandamizaji na utesaji dhidi ya Ahlul Bait wa Mtume, ambapo havikusita hata kuwaua maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume wa Allah. Baada ya Ma'mun kutwaa madaraka ya ukhalifa alihofia sana taathira chanya ya Imam Ridha (as) kwa watu na kwa kuwa alikusudia kumuweka mtukufu huyo chini ya uangalizi wake mkali, huku akijionyesha kuwa ni mwenye mapenzi kwa Watu wa Nyumba ya Mtume, hivyo alitoa amri ya kumuondoa Imam Ridha kutoka mjini Madina na kumpeleka Khorasan (Mash'had ya leo) na kisha akamlazimisha kukubali kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. Siku kama ya leo, yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka 201 Hijiria, khalifa huyo aliwasilisha mbele ya mtukufu huyo suala hilo ambapo hata hivyo alilipinga. Baada ya kulipinga, mtawala huyo dhalimu alitumia vitisho dhidi ya Imam Ridha (as) ambapo baadaye alikubali tu kwa kutikisa kichwa huku mtukufu huyo akisisitiza kuwa jambo hilo halitofikiwa. Baada ya hapo mtukufu huyo alitumia fursa hiyo kueneza mafundisho sahihi ya dini ya Uislamu suala ambalo baadaye lilimfanya Ma'mun kuchukizwa na hatua yake ya kumtoa mjini Madina na ni baada ya hapo pia ndipo alipopanga njama ya kumuua, njama ambayo ilitekelezwa siku ya tarehe 30 Safar mwaka 203 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 450 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti. Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo. Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.
Miaka 347 iliyopita katika siku kama ya leo vita baina Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa Ufalme huo na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland.
Siku kama ya leo miaka 251 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden. Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo na badala yake akaongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi. Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake.
Na katika siku kama hii ya leo miaka 121 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 alizaliwa mwandishi wa Kifaransa, Marcel Ayme. Awali Ayme alisomea uhandisi, hata hivyo aliachana na taaluma hiyo kutokana na kupatwa na maradhi. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo. Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa kama "Beautiful Image", na "The Green Mare".