Soka: Iran yaishinda Kenya japo kwa mbinde mchuano wa kirafiki
Timu ya taifa ya soka ya Iran Jumanne ya Machi 28 ilikuwa mwenyeji wa timu ya Kenya, Harambee Stars katika mchuano wa kirafiki uliopigwa katika Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran, ambapo mwenye aliambulia ushind wa mabao 2-1.
Kipindi cha kwanza kilimalizka kwa sare tasa, huku timu zote mbili zikikabana koo. Hata hivyo Team Melli kama inavyofahamika hapa nchini, ilitoka nyuma na kuambulia ushindi dhidi ya mgeni Kenya kwenye mchuano huo, japo kwa mbinde.
Nahodha wa Harambee Stars, Michael Olunga ambaye anacheza soka la kulipa huko Qatar, aliiweka Kenya kifua mbele kwenye mechi hiyo kwa bao lake la ufundi kunako dakika ya 51.
Hata hivyo Wairani walijikusanya na kuimrisha safu yao ya mashambulizi, na hatimaye jitihada zao zikazaa matunda kwa bao la kufanya ngoma kuwa droo la Mohammad Mohebi katika dakika ya 76 ya mchezo. Ramin Rezaeian alizamisha kabisa jahazi la wageni kwa goli la ushindi katika dakika ya 84.
Hii ilikuwa mechi ya kwanza ya kimataifa ya Kenya, baada ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA kuondoa marufuku dhidi ya timu hiyo kutokana na mizozo na mivutano ya uongozi wa kandanda katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Aidha ulikuwa mchuano wa kujiweka sawa mkufunzi mpya wa Harambee Stars, raia wa Uturuki, Engin Firat, na kupima uwezo wa vijana wake. Firat alisema kucheza dhidi ya mpinzani mkali wa aina hiyo kutawasukuma wachezaji kufika kiwango cha juu, na kuwaonyesha tofauti ya walipo na pale wanapotaka. Hii kwa kutilia maanani kuwa, Iran kwa sasa iko katika nafasi ya 24 katika Orodha ya FIFA ya Wanaume Duniani na ni miongoni mwa timu bora zaidi katika bara Asia.