Jumamosi, Mosi Aprili, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 10 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1444 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Aprili 2023.
Siku kama ya leo miaka 1447 iliyopita yaani tarehe 10 Ramadhani miaka mitatu kabla ya Hijra, alifariki dunia Bibi Khadija binti Khuwailid mke mwema na kipenzi wa Mtume Muhammad (saw) katika mji wa Makka. Bibi Khadija ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri na tajiri wa Makka, aliolewa na Mtume Muhammad (saw) miaka 15 kabla ya kubaathiwa mtukufu huyo. Bibi Khadija alikuwa mtu wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) na alitumia uwezo na utajiri wake katika kuisaidia dini ya Uislamu. Kuweko Bibi Khadija (as) pamoja na Mtume wa Uislamu kulikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba Mtume (saw) alikitaja kifo cha mkewe huyo kipenzi kuwa ni msiba mkubwa. Mtume aliutaja mwaka aliofariki dunia Bibi Khadija na msaidizi wake mwingine mkubwa yaani Abu Talib, kuwa mwaka wa majonzi na huzuni. Hii ni kwa sababu Abu Talib, ami yake Mtume (saw), pia alifariki dunia mwaka huo huo. ***

Siku kama ya leo miaka 959 iliyopita waziri msomi na maarufu wa silsila ya utawala wa Seljuk, Khwaja (Khoja) Nizam al-Mulk, aliuawa na wapinzani wake. Alizaliwa mwaka 410 Hijiria katika mji wa Tous, kaskazini mwashariki mwa Iran ambapo alihudumu kwa kipindi cha miaka 40 katika utawala huo. Katika kipindi hicho Khwaja Nizam al-Mulk aliweza kuasisi shule kama vile Nidhamiyah ya mjini Baghdad na baada ya kuasisi shule hiyo alianza na kazi ya kuwafundisha elimu za fiqhi, tafiri ya Qur'ani na elimu nyingine karibu wanafunzi elfu sita. Athari maarufu ya Nizam al-Mulk ni kitabu cha 'Siyasat Nomeh' au 'Siyarul-Muluuk' chenye vipengee 50 kinachozungumzia mada tofauti zikiwemo za Qur'ani Tukufu, riwaya na sira ya Mtume Muhammad (saw), visa vya Mitume, hekaya na misingi ya uongozi wa nchi. ***
Miaka 445 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa nchini Uingereza William Harvey, tabibu na msomi wa elimu ya tiba. Harvey alianza kufundisha katika chuo kikuu baada ya kuhitimu mafunzo ya tiba na baadaye akaendelea kufanya utafiti katika uga huo. Mwaka 1616 tabibu Harvey aligundua namna damu inavyozunguka mwilini na kuandika makala kuhusu utafiti huo. William Harvey alifariki dunia mwaka 1657. ***
Tarehe Mosi Aprili miaka 78 iliyopita vikosi vya jeshi la Marekani vilifanya mashambulizi makubwa katika kisiwa cha Okinawa huko Japan. Mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia yanahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa kati ya Marekani na Japan. Meli 1300 na karibu ndege elfu 10 za kivita za Marekani zilishiriki kwenye vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa siku 83. Hata hivyo Wajapani walipambana ipasavyo katika vita hivyo kwa ajili ya kulinda nchi yao kwa kadiri kwamba meli 36 za kivita za Marekani ziliharibiwa kikamilifu na nyingine 369 kutiwa hasara. Vilevile ndege za kivita 763 za Marekani zilitunguliwa. Wajapan pia walipata hasara kubwa katika vita hivyo kwani wapiganaji laki moja na elfu kumi kati ya wapiganaji wote laki moja na elfu ishirini wa kisiwa cha Okinawa waliuawa au kujeruhiwa. ***
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi, faqihi, mfasiri wa Qur'an Tukufu na hatibu mkubwa wa Iran. Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi alizaliwa mwaka 1309 Hijiria, mjini Qum na katika familia ya elimu na maarifa ya dini. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alijiunga na masomo ya hawza kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Ayatullah Mirza Abul-Qasim Kabir Qumi, Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi, huku akisoma pia elimu ya falsafa na theolojia kwa Ayatullah Mirza Ali Akbar Mudares Yazdi ambapo alifanikiwa kufikia ngazi ya juu ya kielimu. Alikuwa miongoni mwa shakhsia waliochangia katika uhamisho wa Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi kutoka mjini Arak kwenda mjini Qum na hatimaye kuasisiwa hawza ya kielimu mjini hapo. Mbali na kubobea katika utafiti na kujibu shubuha mbalimbali za dini nyingine, alikuwa mjuzi katika masuala ya historia na jografia ya dini mbalimbali ambapo alitoa nadharia katika uwanja huo. Aidha maulama mbalimbali na maraaji walikuwa wakiheshimu nadharia zake hususan katika uga wa fiqhi huku Imamu Khomein (MA) akimpa lakabu ya 'Sheikh al-Twaifa'. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Risaalatu al-Dharar' 'Mantwiqul Hussein' na 'Maqswadul-Hussein.'
Tarehe 12 Farvardin miaka 44 iliyopita baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kushiriki kwa wingi wananchi katika kura ya maoni, taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kihistoria wa kupasisha mfumo wa utawala wa Kiislamu hapa nchini. Zaidi ya asilimia 98 ya walioshiriki waliupigia kura ya ndiyo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na tarehe 12 Farvardin kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Jamhuri ya Kiislamu. ***