May 15, 2023 10:00 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (16)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 16 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 16.

تَذِلُّ الْأُمُورُ لِلْمَقَادِیرِ حَتَّى یَکُونَ الْحَتْفُ فِی التَّدْبِیرِ 

Mambo yako chini ya qadar na majaaliwa, hata huwa kuna mauti na maangamizi ndani ya tadibiri.

Wasikilizaji wapenzi, mara nyingi huwa tunapangilia mambo yetu kwa ajili ya kufanikisha kazi maalumu na kufikia lengo na makusudio yetu, lakini pamoja na mipango yote hiyo, jitihada zetu huwa hazifiki popote na wakati mwingine majibu yake yanakuwa kinyume na tulivyotarajia. Mfano wa wazi kabisa na halisi wa jambo hilo, ni kisa cha Firauni na njama zake nyingi za kutaka kumwangamiza Mtume wa zama zake, yaani Nabii Musa AS.

Usiku mmoja, Firauni aliota usingizini kuna moto umewaka upande wa Mashariki. Pole pole, ndimi za moto huo zilifika kwenye nyumba za wazee na magwiji wa Misri na kuziteketeza mara moja na haraka nyumba hizo zote. Kisha moto huo ukashika majumba yote, mabustani na kumbi zote za kifalme na kuzigeuza kuwa rundo la majivu.

Firauni alikurupuka usingizini akiwa na hofu ya ajabu, majonzi na huzuni. Wachawi wake, makuhani na wataalamu wa kuagua ndoto waliitwa mara moja mbele yake na kuwataka wamuagulie ndoto yake hiyo.

Mmoja wao alisema: Inaonekana kwamba hivi karibuni mtoto mchanga atazaliwa kutoka kwa Wana wa Israili, na kupindua kiti cha enzi cha Firauni na kuangusha chini taji lake. Silisila ya wafalme wa kizazi cha Firauni nayo itaangamizwa kupitia mtoto huyo.

Firauni aliogopa kupindukia. Aliamuru maafisa na wakunga wote wawafuatilie kwa karibu watu wa Banii Israili na wakati wowote wakiona kuna mtoto wa kiume amezaliwa, wamkate mara moja kichwa chake na kumwangamiza. Kwa ukatili wake huu wa kupindukia, Firauni alidhani angeweza kumwangamiza mtoto huyo ambaye ndiye angeleta mapinduzi makubwa na kumpindua Firauni na nguvu zake zote alizokuwa nazo. Lakini qadar ya Allah ilikuwa ni kitu kingine. Firauni alishindwa kuelewa kuwa Allah anapoamua kitu, lazina kinakuwa na hakuna kiumbe yeyote anayeweza kukizuia. Kwa ufinyu wake wa mawazo, alishindwa kuelewa kuwa fikra zake hizo za kikatili na za kitoto, zisingeweza kamwe kuzuia qadar na maamuzi wa Muumba. 

Kwa hofu na kupenda kwake dunia, Firauni aliamua kuichafuko mikono yake kwa damu za maelfu ya watoto maasumu na malaika wa Mungu wasio na chembe ya hatia. Mwisho wa siku lakini, ujinga wa Firauni ulioonekana, baada ya mtoto huyo kuzaliwa karibu na kasri na jumba lake la kifalme. Mama wa Nabii Musa AS alipewa ilhamu na Mwenyezi Mungu amnyonyeshe mwanawa, amtie kwenye kisusu na amuweke kwenye mto akokotwe na maji. 

Kikapu hicho kilifuata mkondo wa maji na kwenda hadi kwenye jumba la kifalme la Firaun. Mke wa Firaun ambaye hakujaaliwa kuzaa, alipokiona kitoto hicho kichanga chenye nuru na bashasha alikipenda mara moja, alikibeba na kukimbatia kwa nguvu. Matokeo yake ni kwamba Nabii Musa AS alilelewa na kukulia ndani ya jengo lenyewe la Firaun na akafaidika na suhula zote za kifalme katika kukua na kuimarika kila upande. 

Nabii Musa AS hatimaye akawa kijana shababi mwenye nguvu sana. Alikuwa muda wote anachukiwa mno na kifuri cha Firauani na ukatili wake, mpaka Firaun alishindwa kumvumilia. Kwa muhtasari ni kwamba, Nabii Musa AS alishindwa kuendelea kuishi kwenye dhulma na ukatili wa Firauni. Kama kisa chake kilivyo maarufu, kuanzia kuelekea katika mji wa Madyan hadi kurejea tena Misri na miujiza akiwa ni Mtume pamoja na kaka yake Nabii Harun AS. Mwishowe na baada ya matukio mengi, Nabii Musa AS aliamua kuondoka nchini Misri na wafuasi wake, kwenda kutafuta sehemu salama kwao. Lakini Firauni kwa kiburi chake cha kupindukia, alishindwa kuvumilia Nabii Musa na wafuasi wake wanaondoka Misri. Hivyo alikusanya jeshi kubwa na watu wote muhimu wa utawala wake, kumfuata Nabii Musa AS na watu wake ili wawaangamize kabisa. Lakini qadar ilikuwa kitu kingine kabisa. Mwenyezi Mungu aligawanya sehemu mbili Mto Nile ili Nabii Musa AS na wana wa Israili wavuke na wakauvuka salama. Lakini Firauni na jeshi lake na watu wote wakubwa na muhimu wa utawala wake, walipofika katikati ya mto huo, Mwenyezi Mungu aliyaamuru maji yarejee kama kawaida na wote wakaangamia kwenye gharka hiyo akiwemo Firauni mwenyewe na mwili wake kuwekwa kuwa funzo kwa watu wa baada yeke.

Baada ya kusimulia kisa hiki chepesi cha Qur'ani Tukufu, sasa tunaweza kupata picha halisi ya hima hii ya 16 ya Nahjul  Balagha inayosema: Mambo yako chini ya qadar na majaaliwa, hata huwa kuna mauti na maangamizi ndani ya tadibiri

Yaani mambo ya ulimwengu yanatawaliwa na amri za Mwenyezi Mungu zenye hikma na busara sara za hali ya juu kiasi kwamba hakuna mpango wowote unaoweza kuzuia matakwa na maamuzi ya Allah. Kukabiliana na amri za Allah, ni kujiangamiza mwenyewe tu mtu. Tab'an hii inatofautiana kabisa na mtu kufanya uzembe kwa kisingizio cha qadar.