Jumanne, tarehe 16 Mei, 2023
Leo ni Jumanne tarehe 25 Shawwal 1444 Hijria sawa na Mei 16, 2023.
Siku kama ya leo miaka 1296 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabiri bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Siku kama ya leo miaka 521 iliyopita, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake.

Tarehe 16 Mei miaka 235 iliyopita alizaliwa mjini Hamburg, Friedrich Ruckert, malenga na mtaalamu wa masuala ya Mashariki wa Ujerumani. Alifanya juhudi ya kutafsiri mashairi ya lugha za Kifarsi, Kiarabu na Kichina kwa lugha ya Kijerumani. Kadhalika alijifunza fasihi na tamaduni za Mashariki mwa dunia na kuzitumia katika utunzi wa mashairi. Friedrich Ruckert alikuwa mmoja wa malenga wa Kijerumani waliofasiri diwani ya mashairi ya Hafez (malenga mkubwa wa Kiirani) katika lugha ya Kijerumani. Miongoni mwa athari ya Friedrich Ruckert ni kitabu cha 'Spring of Love.'
Katika siku kama hii ya leo miaka 107 iliyopita Ufaransa na Uingereza ziligawana milki zao katika Mashariki ya Kati na maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na utawala wa Dola ya Othmaniyya chini ya mkataba wa Sykes-Picot, ambao ulikuwa umetiwa saini wiki moja kabla. Kutiwa saini kwa mkataba wa kikoloni wa Sykes-Picot Agreement baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kulitayarisha mazingira ya kisiasa ya kugawanywa ardhi ya Mashariki ya Kati na kusambaratisha dola la Othmaniyya. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi za Uingereza na Ufaransa ziligawana udhibiti wa nchi za Kiarabu ambazo zilizokuwa chini ya dola ya Othmaniyya. Kwa utaratibu huo, Iraq na Jordan ziliwekwa chini ya udhibiti wa Uingereza, Syria na Lebanon zikawa chini ya mamlaka ya Ufaransa. Maeneo ya kaskazini mwa Iraq na mashariki mwa Uturuki pia yalikabidhiwa kwa Urusi. Miongoni mwa matokeo mabaya sana ya makubaliano Sykes-Picot ni kuundwa kwa utawala wa kibaguzi wa Israel katika ardhi ya Palestina, jambo ambalo lilifanyika takriban miongo mitatu baada ya kutiwa saini makubaliano hayo.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti lilianza kuondoka nchini Afghanistan. Baada ya Nur Muhammad Taraki kupinduliwa, serikali ya kwanza ya kikomunsti iliyokuwa ikipata himaya ya moja kwa moja ya Urusi ya zamani ilianzishwa nchini Afghanistan. Utawala wa Taraki uliondolewa madarakani mwanzoni mwa mwaka 1979 kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na Hafidhullah Amin mmoja wa watu wake wa karibu. Lakini Warusi hawakumpenda Hafidhullah ambaye alikuwa akitaka kujikurubisha kwa Marekani na kuanzisha uhusiano kati ya Afghanistan na Mashariki na vilevile Magharibi na hivyo wakaipindua serikali yake.

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo DR kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na kuwa na utajiri mkubwa wa madini ikiwemo almasi, imekuwa ikizingatiwa sana na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi.
Na katika siku kama hii ya leo mwaka mmoja uliopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdullah Fateminia, mwanazuoni maarufu wa Kiislamu na mtaalamu wa akhlaki na maadili ya Kiislamu.
Sayyid Abdullah Fateminia alizaliwa mwaka 1325 Hijria Shamsia huko Tabriz, Kaskazini Magharibi mwa Iran. Baba yake Sayyid Ismail Asfiyai Shandabadi alikuwa mwanazuoni, arifu na mwalimu mashuhuri katika chuo cha kidini cha Tabriz. Sayyid Abdullah alianza kusoma sayansi ya kidini kwa baba yake, na baada ya hapo, kwa karibu miaka 30, alisoma akhlaki na maadili kwa Hassan Mostafavi Tabrizi, aliyekuwa miongoni mwa wanafunzi wa Sayyid Ali Qaazi. Pia alikuwa mwanafunzi wa Sayyid Mohammad Hussein Tabatabai, Sayyid Muhammad Hasan Elahi Tabatabai, Muhammad Taqi Behjat, Sayyid Reza Bahauddini, Muhammad Taqi Amoli na Muhammad Ali Araki.
Sayyid Abdullah Fateminia ni mmoja wa wafasiri wa al Sahifa al Sajjadiyyah na Nahj al-Balagha, na alikuwa pia mtaalamu wa elimu za rijal na irfan. Kazi zake nyingi zilijikita katika kutoa hotuba na kuhutubia kwenye mimbari, na alieneza elimu na maarifa yake katika mihadhara hiyo.
Miongoni mwa kazi za mwanazuoni huyo mkubwa ni: "Nukta za Maneno", "Utamaduni wa Kumngojea Imam wa Zama", "Mwisho wa Mapenzi", "Nukta Moja Kati ya Maelfu", "Zawadi ya Ghadir, Hadith Arubaini Kutoka Vyanzo vya Shia na Suni", na "Wimbo wa Ashiki".