May 22, 2023 11:50 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 848 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 42 ya sura hiyo ambayo inasema:

اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapo kufa. Na zile zisizo kufa wakati wa kulala kwake. Huzishika zilizo hukumiwa kufa, na huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.

Kama aya tuliyosoma inavyoeleza, Mwenyezi Mungu Mtukufu huzichukua roho za wanadamu wakati wanapofikwa na mauti; na hufanya hivyo pia kwa roho za walio hai wakati wanapolala. Lakini kwa wale ambao ameamuru wafikwe na mauti, huzizuia roho zao na kwa hiyo wanakufa, na kwa wale ambao amewahukumia waendelee kuishi hadi muda maalumu, huzirejesha roho zao viwiliwilini mwao. Katika mjadala kuhusu tauhidi na shirki, moja ya masuala ambayo Qur'ani inayatilia mkazo ni kwamba, uhai na mauti ya wanadamu viko mikononi mwa Allah SW pekee, na hakuna yeyote aliye mshirika wa Allah katika suala hilo. Katika aya hii ya 42 ya Suratu-Zumar, Qur'ani tukufu inaashiria pande mbili za mwanadamu, yaani kiwiliwili na roho yake. Wakati wa mauti, muunganiko ulioko baina ya roho na kiwiliwili chako unakatika. Kiwiliwili kinatoweka, lakini roho yako inachukuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na inabaki kwake Yeye mpaka Siku ya Kiyama itakapoungana na kiwiliwili mithili ya kiwiliwili chako. Tab'an katika muda wote wa maisha yako, kila siku huwa unakipitia kifo na mauti ya muda; na hilo linajiri pale unapokuwa usingizini. Wakati unapokuwa umelala, muunganiko uliopo baina ya roho yako na kiwiliwili chako unafikia kiwango cha chini kabisa, kiasi cha kukufanya uwe kama umekufa; na unapoamka unakuwa hai tena. Kwa kawaida, watu wote huota ndoto wanapokuwa usingizini; na si hasha katika ulimwengu huo wa ndoto, wakasafiri hadi pembe mbali mbali za dunia, wakafurahika na kucheka, au wakahuzunika na kulia. Jambo hilo ni ishara pia ya roho kutokuwa na utegemezi kwa kiwiliwili; kwa sababu matukio yote hayo huwa yanajiri bila ya kiwiliwili kutikisika wala kwenda popote pale. Kwa hiyo usingizi ni moja ya ishara za qudra na uwezo wa Allah SW, ambayo kama tutaamali na kuitafakari, kwa upande mmoja inatoa somo la ibra na mazingatio kwa mtu, la kumtaka ajue kuwa, wametokezea watu wengi waliokuwa wamelala na hawakuamka tena, kwa hiyo yamkini kulala kwake yeye pia kukaishia kwenye mauti. Na kwa upande mwingine, ni hoja ya kuelewa upande usio wa kimaada wa mwanadamu, ambao katika aya na hadithi, umeelezwa kuwa ni roho. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kiwiliwili na roho ni hakika mbili zinazojitegemea na zenye muunganiko unaokatika wakati wa kifo au usingizi. Wakati mtu anapokufa kiwiliwili chake hutoweka, lakini roho yake inaendelea kubaki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, usingizi ni ndugu wa mauti. Anapokuwa usingizini, mwanadamu hupitiwa na hali nyepesi ya mauti. Vile vile aya hii inatufunza kwamba, kulala na kuamka ni mambo yanayowatokezea watu wote kila siku, lakini ni wale wenye busara na wanaofikiri, ndio wanaotaamali na kuyazingatia mawili hayo na kupata funzo ndani yake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 43 na 44 ambazo zinasema:

أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ شُفَعَاءَ ۚ قُلْ أَوَلَوْ كَانُوا لَا يَمْلِكُونَ شَيْئًا وَلَا يَعْقِلُونَ

Au ndio wanachukua waombezi badala ya Mwenyezi Mungu? Sema: Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote, wala hawatambui lolote?

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا ۖ لَّهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Ni wake Yeye tu ufalme wa mbingu na ardhi. Kisha mtarejeshwa kwake.

Kwa mtazamo wa historia, washirikina walikuwa wakiyaitakidi masanamu kuwa ni wasita na kiunganishi baina yao na Mwenyezi Mungu; na wakisema kwamba: Sisi tunayaabudu masanamu ili yatuombee na kutushufaia kwa Mungu. Kwa hakika washirikina walikuwa wakiyachukulia masanamu hayo ya mawe na miti kuwa nembo ya mambo matakatifu; na kwa hiyo wakiyanyenyekea ili yaweze kuwasaidia. Katika aya hizi tulizosoma, Qur'ani inaibatilisha fikra na imani hiyo potofu kwa kusema: Kwamba ni mtu au kitu gani kinaweza kuwa kiunganishi baina yenu na Mwenyezi Mungu, hilo liko mikononi mwa Yeye Mola, sio nyinyi muamue kukifanya chochote kile mtakacho kiwe wasita baina yenu nyinyi na Yeye. Na hasa mnapoviabudu vitu visivyo na uhai kama masanamu, ambayo hayana akili, hisia wala uwezo wa kufanya jambo lolote lile. Kama nyinyi mnakubali kwamba ulimwengu wote umeumbwa na Allah SW, na Yeye tu ndiye mwenye kuumiliki na kuutawala, kwa nini tena mnaviendea viumbe vyake visivyo na uhai na kutaka shufaa kwao? Alaa kulli hal, mshufaiaji na muombezi yeyote yule lazima apate idhini hiyo kwa Allah. Kwa mujibu wa aya za Qur'ani tukufu, Mitume walikuwa wanaweza kuwa viunganishi baina ya watu na Mwenyezi Mungu; na hilo likifanyika kwa idhini ya Yeye Allah, kama ilivyotokea katika kisa cha Nabii Yusuf (as), ambapo kaka zake waliomtendea ubaya, mwishowe walijuta kwa waliyoyafanya, na wakamuomba baba yao Nabii Yaaqub (as) awe wasita baina yao na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuomba waghufiriwe madhambi yao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur'ani haiukatai msingi wa shufaa na uombezi, bali inapinga uombezi wa masanamu na vile walivyokuwa wakiviabudu washirikina. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wasita na kiunganishi baina yetu na Allah lazima awe bora kuliko sisi, si aliye duni kulinganisha na sisi. Awe na hisia na uelewa na pia awe na uwezo wa kutusaidia na kukidhi matilaba yetu. Vipi mtu anataraji kusaidiwa na masanamu na viumbe vyengine ambavyo havina akili wala hisia yoyote? Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mfumo wa uumbaji umesimama juu ya msingi wa chanzo na sababu; lakini taathira ya vyanzo na sababu hizo, iko mikononi mwa Allah pia.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 45 ambayo inasema:

وَإِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَحْدَهُ اشْمَأَزَّتْ قُلُوبُ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ ۖ وَإِذَا ذُكِرَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

Na anapo tajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyoyo za wasio iamini Akhera huchafuka. Na wanapo tajwa wenginewe asiye kuwa Yeye basi wao hufurahi.

Katika aya hii wamezungumziwa washirikina na wakanushaji wa kufufuliwa viumbe jinsi wanavyochukizwa na suala la tauhidi. Aya inasema: Wakati linapotajwa jina la Allah, Mola pekee wa haki, nyoyo za watu wasioamini akhera huchafuka na kuchukia; lakini wakati wanapozungumziwa waabudiwa wengine, watu hao hujawa na furaha. Mushirikina na watu wenye imani dhaifu, wanaoiona dunia tu wala hawana imani ya akhera, kila anapozungumziwa Mwenyezi Mungu na elimu na uwezo wake mutlaki usio na kikomo, hukereka na kuudhika; na sababu ni kwamba, nyoyo za watu kama hao hazina imani madhubuti kwa Allah. Wao wanadhani kuwa, wengine wasiokuwa Allah ndio wanaoweza kuwatimizia mambo yao. Wanamuelekea na kumtaaradhia shida zao kila mtu katika maisha yao, lakini hawako tayari kutawakali na kumtegemea Allah SW. Wao hawamnyenyekei Mwenyezi Mungu, ambaye ni Muumba wa ulimwengu, lakini wanawanyenyekea na kuwapigia magoti wale ambao ni viumbe na wanadamu kama wao. Kwa wao, ni fahari kutaja majina ya watu wenye hadhi na vyeo vya juu, na huwa na furaha zaidi kadiri wanavyoweza kujikurubisha kwao na kujihisi kuwa wamepata fanaka na saada. Mkabala na wao, ni waumini ambao wanaposikia jina la Allah SW, Muumba pekee wa ulimwengu linatajwa, nyoyo zao husisimkwa kwa shauku na mapenzi na huwa tayari kujitolea katika njia yake kwa kila walichonacho. Jina la Mwenyezi Mungu linawapa furaha, linaburudisha nafsi zao na kuzing’arisha nyoyo zao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, moja ya alama za kutambua kama tuna imani ya kweli, ni kujiangalia kama tunapata utulivu na furaha ya moyo linapotajwa jina la Allah, au wanapotajwa wasiokuwa Yeye. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama tutayadogesha na kuyapuuza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuzitukuza sheria na kanuni zilizotungwa na wanadamu, tujue kwamba tumeingia kwenye shirki, hata kama tunadai kuwa tumemuamini Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 848 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atujaalie kuwa waumini wa kweli na atuepushe na kila aina ya shirki. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/