Sura ya Ghaafir, aya ya 57-60 (Darsa ya 868)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 868 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 57 hadi 59 za sura hiyo ambazo zinasema:
لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ
Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui.
وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَلَا الْمُسِيءُ ۚ قَلِيلًا مَّا تَتَذَكَّرُونَ
Na hawawi sawa kipofu na mwenye kuona; na walio amini na watendao mema hawawi sawa na muovu. Ni machache mnayo yakumbuka.
إِنَّ السَّاعَةَ لَآتِيَةٌ لَّا رَيْبَ فِيهَا وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ
Hakika Saa (ya Kiyama) itafika, nayo haina shaka. Lakini watu wengi hawaamini.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, wapinzani wa dini walikuwa wakibishana na Bwana Mtume SAW na waumini na hawakuwa tayari katu kuyakubali maneno ya haki. Aya hizi tulizosoma zinasema: Waulize wanaokanusha kufufuliwa, je kuumbwa kwa mbingu na ardhi si kukubwa na kuzito zaidi kuliko kuumbwa tena wanadamu Siku ya Kiyama? Yule ambaye ni Muweza wa kuziumba na kuziendesha sayari na maumbo yote yenye wingi na adhama isiyo na kifani atashindwa kweli kuwafufua na kuwaumba tena wanadamu? Fikra ya aina hiyo inatokana na ujahili na ujinga walionao watu wengi ambao wanalinganisha nguvu na uwezo wa Allah na nguvu zao na wanadhani uwezo wa Allah SWT ni mdogo na wenye mpaka maalumu. Kisha aya zinaeleza kwamba, vipofu na wanaoona hawawi sawa. Mtu mjinga na jahili ni mithili ya kipofu, kwa hiyo hawezi kufahamu hakika ya mambo mengi. Utando wa kiburi na ghururi huyaziba macho yake na kumfanya asiweze katu kuona hakika ya mambo kama yalivyo. Lakini mtu mwenye macho yanayoona, huweza kuitambua na kuifahamu haki kupitia mwangwi wa elimu na maarifa. Makundi mawili haya yanaweza kuwa sawa?! Katu hayaewzi kuwa sawa. Mtu anayeona anaushuhudia na kuubaini udogo wake mwenyewe na vile vile ukubwa na adhama ya dunia iliyomzunguka. Kwa sababu hiyo anakijua cheo na nafasi yake. Lakini mtu jahili na kipofu wa moyo haitambui nafasi yake katika zama na mahali alipo wala haioni na kuifahamu dunia iliyomzunguka kando yake; kwa hiyo hukosea katika kuitathmini nafsi yake na kufanya matendo maovu na yasiyo ya sawa. Na bila shaka ni wachache miongoni mwa watu wanaokumbuka na kuaidhika kutokana na ukweli huu. Kutokana na ubishi na ukanushaji wa wapinzani kuhusu Siku ya Kiyama, katika sehemu inayofuatia ya aya tulizosoma, Mwenyezi Mungu SWT anawatangazia kinagaubaga na kwa uhakika watu hao kwamba, kujiri kwa Kiyama ni jambo la yakini, wala hakuna chembe ya shaka juu ya hilo. Hata kama akthari ya watu hawaamini hivyo, lakini ukanushaji wa wapinzani hao hauathiri chochote juu ya kuthbiti ahadi hiyo ya Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kama tutaitazama na kuielewa adhama ya ulimwengu wa maumbile katu hatutajikweza na kuingiwa na kiburi na ghururi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, moja ya sababu za kukanusha maadi na kufufuliwa viumbe ni ujinga na ujahili wa watu kuhusiana na elimu na uwezo wa Allah SWT. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ukafiri na ufasiki hupofusha akili ya mtu na kumfanya asiweze kuuona ukweli wa mambo ya ghaibu. Mtu wa aina hiyo huona mambo yanayohisika na ya kimaada tu. Vile vile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, qudra, hekima na uadilifu wa Mwenyezi Mungu vinahukumu kwamba ahadi yake Mola ya kujiri Kiyama lazima ithibiti na haifai kuwa na shaka juu ya hilo.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 60 ambayo inasema:
وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ
Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike.
Katika aya zilizotangulia imezungumziwa hakika ya kuthibiti kwa Kiyama ambayo ni ahadi isiyo na shaka ya Allah SWT. Aya hii inasema: Si wahalifu na wafanya madhambi peke yao watakaoingia motoni, lakini hata watu waliokuwa wakimjua Allah lakini wakakataa kumuabudu nao pia wataingia motoni. Na sababu ni kuwa, maana ya kufanya hivyo ni kutakabari mbele ya Muumba; na mtu anayejikweza na kutakabari katika kumuabudu Allah ataingia motoni Siku ya Kiyama katika hali mbaya kabisa ya unyonge na udhalili. Tab’an hii haimaanishi kwamba Allah SWT ni mhitaji wa ibada zetu, bali ni kwa sababu matokeo ya kuwa na hulka ya kiburi na kutakabari ni mtu kuishia motoni. Mtu kama huyo, badala ya kutii amri za Muumba wa ulimwengu hufuata hawaa na matamanio ya nafsi yake, ufuataji ambao hauna matokeo mengine isipokuwa kupotoka na kuwa mbali na haki. Sehemu ya kwanza ya aya hii ya 60 inabainisha moja ya vielelezo vya kumuabudu Mola Muumba, ambacho ni dua na kumuomba Yeye Mola. Hii ina maana kwamba, mbali na Sala na ibada zingine zilizoainishwa katika dini tukufu ya Kiislamu, Muislamu anatakiwa pia awe anamkumbuka Allah kila wakati na kumuomba Yeye katika kila hali. Amuombe amuondolee shida zake pale anapokuwa amekumbwa masaibu na afanye hivyo pia kushukuru neema zake pale anapokuwa kwenye raha na uneemevu. Na Yeye Allah SWT ametueleza wazi kwamba ni mwenye kuyasikia maombi na dua za waja wake na ataziitika na kuwakidhia wanayomuomba kwa namna mwafaka. Tab’an dua zinazotakabaliwa hasa ni zile ambazo, muombaji wake na yale ayaombayo huwa yamekidhi masharti yatakiwayo. Ijapokuwa elimu na uwezo wa Allah ni mutlaki na hauna kikomo, lakini kutokana na hekima yake huwa hawakidhii waja wake kila wanaloliomba. Kwa hiyo kwa kuzingatia maslaha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla humpa mwenye kuomba dua lile lililo bora ili apate yenye kheri zaidi kwake hata kama yumkini yeye mtu mwenyewe hataweza kulifahamu hilo. Lakini pia dua haitakiwi iwe chaguo mbadala la kuacha kufanya kazi; na kama mtu atajipweteka tu na kutofanya juhudi zozote, dua yake haitajibiwa na kutakabaliwa. Kimsingi ni kwamba, moja ya sababu za kutoitikiwa dua nyingi ni kwamba watu huinua mikono juu kuomba dua bila kufanya bidii na juhudi zozote. Kuna sababu na mambo mengine pia yanayozifanya baadhi ya dua zisitakabaliwe. Miongoni mwao ni mtu kukosea katika kufahamu yenye manufaa na madhara kwa nafsi yake; kwa hivyo humlilia na kumwomba Mwenyezi Mungu jambo lisilo na maslaha yoyote na yeye. Katika hali kama hiyo dua ya mtu huwa haitakabaliwi pia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, dua ni aina mojawapo ya ibada za kumwabudu Allah SWT; na kuiacha dua ni alama ya kutakabari na kujivua mtu sifa ya kuwa mja. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, katika dua tumuombe Allah peke yake, na yote tuyatakayo tuyaombe kwake Yeye tu bila kumshirikisha naye mtu yeyote. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu anazijua shida zetu; na kimsingi si mhitaji wa dua na ibada zetu. Ukweli ni kwamba amri ya kuomba dua iliyotolewa ndani ya Qur’ani ina athari na baraka kadha wa kadha kwa yeye mtu mwenyewe. Mojawapo ni kwamba dua humfanya mtu ajitambue kuwa yeye ni mwenye kumhitajia Allah katika kila hali na kwa hiyo hujivua na ghururi na kiburi ambavyo ni chanzo cha kuhasirika na kuharibikiwa. Vilevile aya hii inatutaka tujue kwamba, kuwa na kiburi na kutakabari kwa namna yoyote ile mbele ya Allah, hatima yake ni kufedheheka na kudhalilika Siku ya Kiyama. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 868 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azitakase nyoyo zetu na kila aina ya maradhi ya nafsi, ikiwemo ghururi, kiburi, kujikweza na majivuno. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/