May 30, 2023 01:35 UTC
  • Jumanne, 30 Mei, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 10 Mfunguo Pili Dhulqaada 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Mei 2023

Miaka 279 iliyopita katika siku kama ya leo, Alexander Pope mshairi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiingereza aliaga dunia. Alizaliwa mjini London Mei 21 mwaka 1688 katika familia ya kitajiri. Hata hivyo kutokana na kuwa na ulemavu wa viungo, baba na mama yake walimlea nje ya mji katika nyumba moja. Alipofikisha umri wa miaka 15 Alexander Pope alikuwa tayari anazifahamu vyema lugha za Kigiriki, Kifaransa na Kitaliano. Alitoa mjumuko wake wa kwanza wa mashairi alipokuwa na umri wa miaka 23.

Alexander Pope

Siku kama ya leo miaka 245 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois - Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa.

Francois - Marie Arouet

Siku kama ya leo 99 miaka iliyopita, alifariki dunia Ali Akbar Khan Nafisi aliyejulikana kama Naadhimul Atibaa, daktari na mtaalamu wa lugha wa Kiirani, katika mji wa Tehran. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi alianza kujifunza masomo ya kidini na udaktari katika chuo cha Darul Funun cha Tehran. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Naadhimul Atibaa katika uwanja wa tiba vimetarjumiwa katika lugha za kigeni. Ali Akbar Khan Nafisi ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifanya jitihada kubwa katika kukusanya maneno ya lugha ya Kifarsi na kuandika kamusi inayoitwa 'Kamusi ya Nafisi.'

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita inayosadifiana na tarehe 30 Mei 1981, aliuawa Ziaur Rahman, Rais wa Bangladesh baada ya kupigwa risasi katika mji wa Chittagong ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Rais Ziaur Rahman aliuawa baada ya kuchungulia dirishani kwenye nyumba ya wageni ya serikali katika mji huo. Watu wanane waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi na walinzi wa rais huyo.