Jun 07, 2023 21:59 UTC
  • Alkhamisi tarehe 8 Juni 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Mfunguo Pili Dhilqaada 1444 Hijria sawa na Juni 8 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 726 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Kamaluddin Farsi mwanahisabati mashuhuri wa Kiirani.

Kamaluddin Farsi aliyekuwa amebobea pia katika elimu ya fizikia, alifanya safari wakati wa ujana wake katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Licha ya kuwa umri wake hapa duniani ulikuwa mfupi, lakini ameacha athari zenye thamani kubwa katika elimu ya hisabati na utambuzi wa nuru.

Kitabu cha Tadhkirat al-Ahbab ndio kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu. 

Sanamu la Kamaluddin Farsi

Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita inayosadiafiana na tarehe 8 Juni 1830, Camberz mbunifu wa Kijerumani alivumbua utengenezaji wa kiberiti. Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na hiki kinachotumiwa hivi sasa, ni uwakaji wake uliokuwa wa taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine kadhaa waliofanya utafiti wao kuhusiana na kiberiti, na hatimaye Phillips raia wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama hiki ambacho kinatumika leo hii.

Tarehe 8 Juni miaka 168 iliyopita, mji wa Lisbon ambao ni mji mkuu wa Ureno uliharibika kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo. Karibu wakazi elfu arubaini wa mji huo walipoteza maisha yao na theluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo zilibomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngalawa nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi kuwahi kuikumba Ureno.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, shirika la kijasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO huko Paris, Ufaransa.  Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo.

Atef Bseiso