Jumapili, tarehe 11 Juni, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 22 Dhulqaada 1444 Hijria sawa na tarehe 11 Juni 2023.
Siku kama ya leo miaka 1036 iliyopita yaani tarehe 22 Dhulqaada mwaka 408 Hijria Qamaria, alizaliwa Khoja Nizam al-Mulk, msomi na shakhsia muhimu wa kisiasa na kiutamaduni wa karne ya tano Hijiria mjini Tus, moja ya miji ya kaskazini mashariki mwa Iran. Nizam al-Mulk alikuwa mmoja wa wasomi ambao walikuwa na taathira kubwa katika mabadiliko ya kisiasa na kiutamaduni katika karne hizo. Katika kipindi cha silsila ya utawala wa Masaljuki, Khoja Nizam al-Mulk aliteuliwa kushika wadhifa wa uwaziri ambapo aliendelea kujishughulisha na masuala ya uongozi kwa kipindi cha miaka 30 na kufanikiwa kuiletea Iran ya wakati huo, maendeleo makubwa hususan katika uga wa utamaduni.
Miaka 908 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 22 Dhulqaada mwaka 536 Hijria Qamaria, kazi ya kuandika tafsiri mashuhuri ya Majmaul Bayan ilimalizika. Kitabu hicho kiliandikwa na Sheikh Tabarsi mmoja wa wafasiri wakubwa wa Qur'ani Tukufu na miongoni mwa maulamaa mashuhuri wa Iran aliyekuwa mashuhuri kwa jina la "Aminul Islam" kutokana na uaminifu na uchamungu wake. Kitabu hicho ni miongoni mwa tafsiri mashuhuri za Qur'ani kutokana na mbinu yake ya kuvutia katika mtazamo wa fasihi. Tafsiri hiyo imechapishwa mara kadhaa katika nchi za Iran, Lebanon na Misri.

Katika siku kama ya leo miaka 451 iliyopita sawa na tarehe 11 Juni mwaka 1572, alizaliwa Benjamin Jonson mshairi na mwandishi wa filamu wa Uingereza. Jonson kwa muda mrefu alikuwa mcheza tamthilia na rafiki wa Shakespare mwandishi maarufu wa Uingereza, ambapo urafiki wao ulikuwa na athari kubwa katika kukamilisha fasihi ya mshairi huyo. Baadhi ya athari zilizoachwa na Benjamin Jonson ni Mwanamke Aliyezimwa' pamoja na Historia ya Dunia. Malenga huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1637.
Siku kama ya leo miaka 168 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi. Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen. Si vibaya kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo linasababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Haitham na Qutbuddin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen.

Miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Khordad mwaka 1353 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Daktari Muhammad Khazaeli, mwasisi wa Tasisi ya Kuongoza na Kuwasaidia Vipofu ya Iran. Khazaeli alipokuwa mtoto alipoteza nguvu ya kuona kutokana na ugonjwa wa ndui, na alipata elimu katika shule maalumu ya vipofu. Dakta huyo kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi mambo, alipata mafanikio makubwa katika masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamilifu ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Khazaeli alifahamu vyema lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza na aliandika na kutafsiri vitabu mbalimbali. Miongoni mwa masuala aliyojishughulisha nayo ni kupigania kupatiwa huduma muhimu vipofu katika uga wa kimataifa na alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mashariki ya Kati katika Baraza la kitaifa la kuwahudumia vipofu na Jumuiya ya Kimataifa ya Vipofu.