Jun 12, 2023 22:48 UTC
  • Jumanne, Juni 13, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 24 Mfunguo Pili Dhulqaad 1444 Hijria, sawa na tarehe 13 Juni 2023.

Siku kama ya leo miaka 1244 iliyopita Imam Ali bin Musa Ridha (a.s) alianza safari yake kutoka Madina kuelekea Marv huko Kaskazini Mashariki mwa Iran ya zamani.

Imam Ridha (a.s) alifanya safari hiyo kwa kulazimishwa na kushinikizwa na Maamun, khalifa na mtawala wa saba wa ukoo wa Bani Abbas. Lengo la safari hiyo lilikuwa kumuweka Imam Ridha chini ya uangalizi.

Maamun alitoa pendekezo kwa Imam huko Marv kwamba akubali kuwa mrithi wake. Maamun alifanya hivyo ili kujionyesha kuwa ni mtu mwenye mapenzi na Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (s.a.w). Hata hivyo katika fursa mbalimbali Imam Ridha si tu kwamba alionyesha kuwa hakubali kushirikiana na  utawala wa Bani Abbas, bali pia aliutambua utawala huo kuwa ni wa kupenda makuu na wa kidhalimu.     ******

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita muwafaka na tarehe 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, ilianza harakati kubwa ya kwanza ya wananchi katika ardhi yote ya Palestina dhidi ya Wazayuni.

Harakati ya wananchi hao wa Palestina ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wakiishi Palestina.

Katika fremu ya sera hizo za Uingereza mwaka 1923 kulikuwa na Wazayuni 35 elfu huko Palestina na kabla ya kuundwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 idadi hiyo ilikuwa zaidi ya laki sita.                                              ******

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.     ******

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi la Kiutamaduni.

Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.   ******

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin, faqihi na mfasiri mkubwa wa Qurani Tukufu alifariki dunia katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu na kufanikiwa kufasiri kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu katika juzuu 15 na kuandika vitabu vingine vingi. Miongoni ma vitabu vya msomi huyu ni Al Sayr Wassuluuk, Njia ya Saada na Nafahaat Rahmaniyya.