Vita vya Gaza na Kitendawili cha Siku Zijazo
(last modified Thu, 21 Dec 2023 07:40:10 GMT )
Dec 21, 2023 07:40 UTC
  • Vita vya Gaza na Kitendawili cha Siku Zijazo

Hamjambo na karibuni kuwa nami katika kipindi chetu cha Makala ya Wiki ambacho kitaangazia vita vya Gaza na kitendawili kinachogubika mustakbali wa mapambano ya uhuru ya Wapalestina katika siku zijazo.

Zaidi ya miezi miwili imepita sasa tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanzishe mashambulizi ya kikatili katika Ukanda wa Gaza baada ya kushindwa kiusalama na kijeshi kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, tarehe 7 Oktoba. Benjamin Netanyahu, ambaye sasa anatambuliwa kwa jiina la mchinjaji wa Wapalestina, anataka kulipiza kisasi cha kushindwa huko kukubwa kwa kuua idadi kubwa zaidi ya wanawake na watoto wa Kipalestina. Katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili iliyopita nchi mbalimbali zimejaribu kuulazimisha utawala wa Kizayuni usimamishe mashambulizi na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Gaza kwa kupendekeza miswada katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakini bila mafanikio. 

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel 

Marekani ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel imepinga rasimu zote za maazimio yaliyopendekezwa kwa kutumia kura ya veto. Jaribio la mwisho la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kwa ajili ya kupasishwa azimio la kusitisha mapigano Gaza pia lilishindwa kwa kura ya turufu ya Marekani mnamo Ijumaa, Disemba 8. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametumia ibara ya 99 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni nadra sana kutumiwa na Katibu Mkuu wa umoja huo, kwa ajili ya kusitisha vita Ukanda wa Gaza. Guterres alisema: Ninaandika barua kwa Baraza la Usalama kwa kutumia kifungu cha 99 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa sababu tumefikia hatua ya kusambaratika. Hali inazidi kuzorota na kuwa janga lenye athari zisizoweza kurejeshwa katika hali ya awali kwa Wapalestina kwa ujumla na kwa amani na usalama wa kikanda."

Kifungu cha 99 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa hakijatumika kwa miaka mingi. Kifungu hicho kinasema, mkuu wa UN "anaweza kulijulisha Baraza la Usalama jambo lolote ambalo kwa maoni yake, linatishia amani na usalama wa kimataifa." 

Reza Nasri, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema kuhusu hatua hiyo ya Antonio Guterres katika Baraza la Usalama kwamba: Katika barua yake kwa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa na kuonyesha takwimu za maafa makubwa miongoni mwa raia wa Gaza, hali ya kusikitisha ya hospitali, kuporomoka mfumo wa afya, ugumu wa kutoa misaada ya kibinadamu na masaibu mengine mengi ya vita akiyataja mashambulizi yasiyosita ya Israel kuwa ndio sababu ya kuporomoka kabisa mfumo wa umma na kuonya juu ya uwezekano wa kutokea maafa yasiyoweza kufidika wala kurekebishwa."

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN 

Kura ya veto ya Marekani dhidi ya rasimu ya azimio la kutaka kusitishwa mapigano huko Gaza kwa kutegemea kifungu 99 cha Umoja wa Mataifa ni kushindwa kukubwa kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ngazi ya maoni ya umma wa dunia. Sambamba na mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu wa Gaza, Israel na waungaji mkono wake, Marekani na serikali za nchi za Ulaya, zimeanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya harakati ya kupigania ukombozi ya Hamas na watu wa Palestina kwa ujumla. Mara hii, Wazayuni wanajaribu kuhalalisha mauaji ya watoto na wanawake wa Kipalestina katika maoni na fikra za watu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na katika nchi za Magharibi kwa kutumia propaganda kali za vyombo vya habari kwamba Hamas ni kundi la kigaidi. Hata hivyo sera hiyo ya Wazayuni maghasibu ilikuwa na matokeo kinyume, ambapo wimbi la chuki na upinzani dhidi ya mauaji ya kimbari ya chinjachinja wa Wapalestina, yaani Netanyahu, linazidi kushamiri katika miji ya nchi za Ulaya na Marekani, sambamba na katika nchi za Kiislamu dhidi ya utawala bandia wa Israel.

Katika kukabiliana na wimbi hilo la maandamano ya kupinga jinai zinazofanywa na Israel huko Gaza, Marekani na nchi za Ulaya zimeshindwa kutaja uungaji mkono wa mataifa mbalimbali kwa wananchi wa Palestina kuwa ni chuki dhidi ya Uyahudi, na badala yake zinaendelea kuficha na kufunika jinai za utawala huo ghasibu kwa kutumia madai ya kujitetea. Katika ngazi ya taasisi za kimataifa, kwa mara ya kwanza, kumeanzishwa kampeni ya kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza. Kwa kawaida taasisi za kimataifa zilikuwa na misimamo ya upendeleo au kwa uchache zilinyamaza kimya kuhusiana na uhalifu wa  Israel kutokana na ushawishi wa serikali za nchi za Magharibi katika taasisi hizo. Lakini mara hii hali imekuwa tofauti kiasi kwamba, Umoja wa Mataifa na baadhi ya maafisa wa taasisi za kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, wamekuwa na mienendo tofauti, kadiri kwamba Antonio Guterres, ametumia Ibara ya 99 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa inayompa mamlaka maalumu kwa ajili ya kuitisha mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha vita na mauaji ya raia huko Gaza. Marekakani ilikuwa mpinzani wa kwanza wa ombi hilo la Guterres.

Maangamizi ya kizazi Gaza yanayofanywa na utawala wa Kizayuni 

Marekani imeutaja uamuzi huo wa Guterres kuwa ni aibu kubwa na inaamini kwamba, kutumia kifungu hicho katika duru za kimataifa (kuhusiana na Gaza) kunatafsiriwa kwamba, Umoja wa Mataifa umeitambua Israel kuwa ni mtenda jinai ya mauaji ya kimbari na kwamba nchi zinazoiunga mkono Israel, hasa Marekani, zinahusika katika mauaji hayo ya kimbari. Katika mkondo huo, Eli Cohen, Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Uongozi wa Guterres ni hatari kwa amani ya dunia."

Katika kukabiliana na hatua hiyo ya Antonio Guterres, Marekani na Israel, kama kawaida yao, zinafanya mikakati ya kupotosha ukweli na kubadilisha nafasi ya dhalimu na mdhulumiwa, muuaji na aliyeuawa. Ni vyema kuashiria hapa pia kwamba, Kati ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama la UN, ni Marekani pekee iliyopiga kura kupinga rasimu ya azimio la kutaka kusitishwa mapigano huko Gaza. Hata Uingereza, baba wa ubatizo wa utawala wa Kizayuni, ilijiepusha kupiga kura ya kupinga rasimu hiyo katika Baraza la Usalama. Kilichoilazimisha serikali ya Uingereza kutopiga kura katika kikao cha Baraza la Usalama ni mashinikizo ya umma katika nchi hiyo. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, maandamano mengi zaidi dhidi ya Israel na kuwatetea wananchi wa Palestina yamefanyika nchini Uingereza kuliko nchi nyingine yoyote ya Ulaya.

Maandamano ya London dhidi ya mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza 

Hata Ufaransa, ambayo awali iliyatambua mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza kuwa ni haki yake ya kujilinda, inajaribu kujivika sura ya kibinadamu, angalau kidhahiri tu. Nicolas de Rivière, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, amesema: "Kwa mara nyingine tena, Baraza la Usalama limeshindwa. Ufaransa ina wasiwasi mkubwa kuhusu maafa ya kibinadamu yanayotokea Gaza, na kwa sababu hiyo, imepiga kura ya ndio kwa azimio hili."

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekosa hata kuungwa mkono na watetezi wake wa jadi na washirika wa kibiashara kama vile Russia na China, nchi mbili zenye haki ya kura ya veto katika Umoja wa Mataifa.

Sasa na baada ya mauaji ya kimbari ya Wapalestina karibu elfu 20 wa Gaza, walimwengu wanamtambua Benjamin Netanyahu na jeshi la Israel kuwa ni wahalifu wa kivita. Nchi za Ulaya zinazodai kutetea ubinadamu haziwezi kuficha uhalifu huu, na kinyume na msimamo wao wa kuiunga mkono Israel, zimelazimika kubadili lugha yao.

Licha ya juhudi za Wazayuni za kuugeuza Ukanda wa Gaza kuwa ardhi iliyoteketezwa na moto, lakini bado Muqawama wa Palestina dhidi ya Netanyahu na jeshi la Kizayuni unaendelea, na nguvu bandia za jeshi la Israel haziachi alama yoyote isipokuwa ardhi iliyoungua na maafa makubwa ya binadamu katika Ukanda wa Gaza. Tukutane tena juma lijalo panapo majaliwa yake Mola Muumba.