Kukumbuka siku ya kuzaliwa Bibi Fatima al Maasuma AS
(last modified Wed, 03 Aug 2016 15:48:12 GMT )
Aug 03, 2016 15:48 UTC
  • Kukumbuka siku ya kuzaliwa Bibi Fatima al Maasuma AS

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Bibi Fatima al Maasuma 'Alayhas Salam', mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (SAW).

Mtume Mtukufu (SAW), Maimamu Watoharifu (A.S) pamoja na watoto wao watukufu wana daraja na utukufu mkubwa miongoni mwa viumbe vyote. Mwenyezi Mungu SW amewafanya kuwa ruwaza njema na viigizo vya kweli kati ya wanaadamu. Kadiri ufahamu na maarifa kuhusiana na watukufu hao yanavyozidi kuongezeka, ndivyo mtu anavyohisi mapenzi na mahaba zaidi kwa watukufu hao moyoni mwake. Hapana shaka kuwa, mapenzi ya kweli hupatikana kutokana na kuwafahamu na kuwajua vyema watu wao watukufu. Moja ya njia za kuweza kuwafahamu mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kutwalii na kutafakari sira na mwenendo wa maisha yao, na pia kukumbuka nafasi ya kimaanawi na fadhila zao za kiakhlaki. Njia hiyo ya ufahamu mbali na kuwa kiasili huleta athari muhimu ya kujenga na kuzidisha mapenzi nyoyoni, pia humfanya mtu afuate mafundisho yao na kuiga mifano yao. Hii ni kwa sababu, hakuna mtu anayeweza kupata malezi sahihi, saada na kufikia ukamilifu, ila anakapokuwa tayari kufuata njia na kuiga watu ambao wamepata daraja ya kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa watukufu hao ni Bibi Fatima al Maasuma (A.S) binti wa Imam Mussa bin Jaafar (A.S), ambaye hii leo tunakumbuka siku ya kuzaliwa kwake. Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote duniani na haswa wapenzi wa Mtume Mtufuku (SAW) na watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa mjukuu wake huyo.

Kama tulivyoashiria hivi punde, Bibi Maasuma SA ni binti wa Imam Kadhim AS na ni mdogo wake Imam Ridha AS. Alizaliwa mwaka 173 Hijria. Alikuwa na umri wa miaka 10 tu wakati baba yake, Imam Kadhim AS alipouawa shahidi.

Licha ya kumpoteza baba yake akiwa bado mdogo, lakini cheche za matumaini zilibakia katika maisha yake kutokana na kuishi na Imam Ridha AS. Bibi Maasuma SA alikuwa na kiwango cha juu cha imani na utakasifu wa nafsi. Katika zama zake za utotoni alikuwa na fadhila kubwa za kielimu na kimaanawi. Imenukuluwa kuwa, bibi huyo mtukufu hata katika zama zake za utotoni alikuwa akijibu maswali mengi sana ya kielimu na kifiqhi.

Kwa kweli kwa mtazamo wa dini tukufu ya Kiislamu, kuwa mwanaume au mwanamke si kigezo cha kuwa mbora au kuwa mtukufu zaidi, kwani mafunzo ya Uislamu yanamlenga mwanadamu kama mwanadamu na wala si jinsia ya mtu. Kama ambavyo wanaume kama Mitume na Maimamu watoharifu (A.S) walikuwa ni mifano bora kwa wengine, wanawake watukufu pia kama vile Bibi Asya mke wa Firaun, Bibi Maryam, Bibi Khadija, Bibi Fatimatuz Zahra, Zainabul Qubra na Fatima al Maasuma (A.S) nao wanahesabiwa kuwa vigezo na mifano bora kwa wanawake wote duniani. Kwa msingi huo, kutwalii historia ya maisha, sira ya kivitendo na yaliyobainishwa kuhusiana na mienendo ya watukufu hao walioteuliwa na Mwenyezi Mungu, ni jambo muhimu sana kwa ajili ya kufikia saada, ukamilifu na maisha bora ya mwanadamu. Pia kuwafahamu vyema watu hao huwa kunatoa mwanga wa uongofu katika maisha ya watu wote. Ni wazi kuwa mche utakaomea katika bustani ya Uimamu na kupata nishati kwa kustafidi na nuru hiyo ya fadhila, kila muda unavyopita ndivyo yanavyozidi kustawi, ndivyo matawi yake huchanua na kupendeza zaidi, kutokana na shajara njema ya familia ya Mtume Mtukufu. Bibi Fatima al Maasuma (A.S) ni binti anayetoka katika familia hiyo, ambaye alizaliwa mjini Madina tarehe Mosi Dhil Qaadah mwaka 173 Hijiria. Bibi huyo alilelewa na kuishi katika nyumba aliyokuwa pia akiishi baba yake Imam Mussa al Khadhim (A.S) na kaka yake Imam Ridha (A.S). Bibi Fatima al-Maasuma 'Alayha Salaam' alikulia katika malezi ya ucha-Mungu na katika chemchemu ya maarifa, hekima, elimu na zuhdi na kupata utakasifu mkubwa wa mwili na roho. Kama tulivyoashiria katika utangulizi wa makala hii, akiwa bado mdogo, Bibi Maasuma AS alikumbwa na msiba mkubwa wa kuuawa shahidi baba yake kipenzi kwenye jela ya Harouna Rashid katika mji wa Baghdad wa Iraq ya leo. Hivyo kuanzia wakati huo akawa chini ya usimamizi na ulezi wa kaka yake Imam Ali bin Mussa ar Ridha (A.S).

Muonekano wa ndani wa Haram ya Bibi Maasuma AS mjini Qum, Iran

 

Hapana shaka kuwa chanzo kikuu cha saada na ukamilifu wa mwanadamu na kumkurubia Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni kuwa na imani thabiti juu ya dhati iliyotakasika ya Mwenyezi Mungu na kufuata vyema na ipasavyo maamrisho yake. Mwenyezi Mungu ametuambia kuwa maisha mazuri ni matokeo ya imana mwanamke atakayetenda amali njema, kuwa atapata maisha mazuri. Bibi Fatima al Maasuma (A.S) ni miongoni mwa wanawake, ambao imeelezwa kuwa waliwazidi wengine katika kufuata mwendo huo. Mtaalamu mashuhuri wa hadithi marhum Haji Sheikh Abbas Qumi ameandika maelezo ya kutosha kuhusiana na watoto wa kike wa Imam Mussa al Kadhim (A.S). Katika sehemu moja ya maelezo yake anasema: 'Kwa mujibu wa yale yaliyotufikia, wabora kati yao ni Bibi Jalilah Muadhama na Fatima binti wa Imam Mussa al Kadhim (A.S) maarufu kama Bibi Maasuma.' Bibi huyo mwenye fadhila alikuwa na utukufu mkubwa, na Maimamu Watoharifu walikuwa wakimtaja kwa utukufu na fadhila, kiasi kwamba hata kabla ya kuzaliwa kwake, baba yake mtukufu alikuwa tayari amelisikia jina lake kutoka kwa baadhi ya Maimamu, na tayari utukufu na nafasi yake adhimu ilikuwa imeshazungumzwa. Miongoni mwa fadhila za bibi huyu Mtukufu ni 'uwezo aliopewa na Mwenyezi Mungu wa kutoa shifaa.' Imenukuliwa kutoka kwa Imam Jaafar Swadiq (A.S) akisema: 'Mwanamke kutoka katika watoto wangu atafariki dunia katika mji wa Qum, ambaye jina lake ni Fatima binti Mussa. Wafuasi wangu wataingia peponi kwa shifaa yake.'

Fadhila nyingine ya Bibi Fatima al Maasum (A.S), ni uwezo wake wa kubainisha hadithi, na kutokana na kipaji hicho alijulikana kwa jina la 'Muhadditha.'

Jina la Fatima binti Mussa bin Jaafar pia linaonekana katika silsila ya sanadi za baadhi ya wapokezi wa hadithi, kiasi kwamba maulamaa wa Kisuni na Kishia wanazielezea riwaya zake kuwa ni sahihi na zenye kukubalika. Miongoni mwa hadithi hizo ambazo mapokezi yake yanaenda hadi kwa Bibi Fatimatuz Zahra (A.S) na Mtume Mtukufu (SAW) ni 'Hadith ya Ghadir' na 'Hadithi ya Manzila', hadithi ambazo zinaelezea utukufu wa Imam Ali (A.S).

Kwa mujibu wa riwaya mbalimbali, Bibi Maasuma SA alikuwa na lakabu nyingine mashuhuri ya 'Karima Ahlul Bait'. 'Karima' ni neno lenye maana ya mwanamke mkarimu na mwenye huruma. Bibi Maasuma SA alipitisha maisha yake yaliyojaa ufanisi akiwa anajishughulisha na kutoa darsa na mafunzo ya Kiislamu na tafasiri ya Qur'ani Tukkufu. Aidha alitumia wakati wake wote kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kutokana na mwenendo wake huu wa kufuata dini kikamilifu na kutotoka katika utiifu wa Imam na kiongozi wake, aliweza kufika daraja ya juu ya ukamilifu na ubora wa mwanaadamu. Katika kubainisha taqwa ya hali ya juu pamoja na utakasifu wa mdogo wake huyo Imam Ridha AS alisema kuwa, 'Maasuma' maana yake ni mwanamke aliyetakasika na anayejiweka mbali na madhambi.

Bibi Fatima al Maasuma (A.S) alikuwa akimpenda sana kaka yake Imam Ridha (A.S). Mapenzi na upendo huo haukutokana tu na uhusiano wa kinasaba kati ya kaka na mdogo wake, bali ulitokana na ufahamu wa bibi huyo mtukufu juu ya nafasi ya wilaya na uongozi katika Uislamu. Mapenzi hayo yalisababisha bibi huyo kufunga safari ambayo ilikuwa na nafasi muhimu mno katika maisha yake.

Muonekano wa nje wa Haram ya Bibi Maasuma SA mjini Qum, Iran

 

Safari ya Imam Ridha ya kubaidishwa kutoka mji wa Madina na kupelekwa Marw nchini Iran mwaka 200 Hijiria, ilifanyika kutokana na sisitizo na vitisho vya Maamun mtawala wa Bani Abbas, na mtukufu huyo alilazimika kwenda katika mji wa Khorasan nchini Iran tena bila ya kufuatana na mtu yoyote wa familia yake au watu wa nyumbani kwake. Mwaka mmoja baada ya kuhijiri kaka yake, Bibi Fatima al Maasuma alianza safari ya kuelekea Khorasan kwa ajili ya kumuona kaka yake huyo akiwa amefuatana na baadhi ya kaka zake na watoto wa kaka zake. Mbali na hilo, jambo muhimu zaidi lililomfanya mtukufu huyo afunge safari hiyo ndefu iliyojaa mashaka na matatizo mengi lilikuwa ni kutekeleza jukumu la kutetea nafasi ya wilaya na uongozi katika Uislamu.

Msafara wake ulipokelewa na kulakiwa na watu wengi katika kila mji waliopita. Bibi huyo mtukufu pia alifikisha ujumbe wa kudhulumiwa na kuachwa pekee kaka yake kwa waumini na Waislamu wa sehemu alizopitia, kama alivyofanya Bibi Zaynab (A.S), na kuonyesha upinzani wake na wa Watu wa Nyumba ya Mtume (A.S) dhidi ya utawala uliokuwa umejaa hila wa Bani Abbas.

Kwa ajili hiyo, msafara wa bibi huyo mtukufu ulipofika katika mji wa Save, baadhi ya watu waliokuwa wakiwapinga Ahlul Bait waliokuwa wakiungwa mkono na vibaraka wa utawala huo waliuzuia msafara huo, na kupigana na watu waliofutana na bibi huyo suala ambalo lilisababisha karibu wanaume wote wa msafara huo kuuwawa shahidi. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya Bibi Fatima al Maasum pia alipewa sumu na waovu hao. Alaa Kulli hal Bibi Fatima al Maasuma aliugua, labda kutokana na majonzi na huzuni kubwa iliyotokana na tukio hilo au kutokana na athari ya sumu aliyopewa, na kwa kuwa hakuweza tena kuendelea na safari yake kuelekea Khorasan, aliamua kwenda katika mji wa Qom. Alisema: 'Nipelekeni katika mji wa Qum, kwani nilimsikia baba yangu akisema kwamba, mji wa Qum ni kituo cha wafuasi wetu.'

Wapenzi wa Ahlul Bait AS kutoka kona mbalimbali za dunia hufanya ziara katika Haram ya Bibi Maasuma AS kwenye mji mtakatifu wa Qum kwa shauku kubwa kwani imepokewa kutoka kwa Imam Ridha AS akisema: Yeyote anayemzuri Bibi Maasuma AS ni kama aliyenizuru mimi.

Wakuu wa mji wa Qum walipofahamu kuhusu ujio wake waliharakisha kwenda kumlaki. Mussa bin Khazraj mmoja wa wazee wa mji huo aliwatanguliwa watu wote kwenda kumlaki bibi huyo mtukufu. Tarehe 23 Rabiul Awwal mwaka 201 Hijiria Bibi Fatima al Maasuma aliwasili katika mji mtukufu wa Qum. Aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubishwa kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW).

Kutokana na baraka ya safari ya bibi huyo mtukufu, hadi hii leo mji wa Qum ni moja ya vituo vikubwa vya elimu ya Ahlul Bait na dini tukufu ya Uislamu. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote duniani na haswa wapenzi wa Mtume Mtufuku (SAW) na Watu wa Nyumba yake tukufu kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa mjukuu huyo wa Mtume.

Sala na salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Mtume Muhammad na Watu wa Nyumba Yake. Sala na Salamu Zimfikie Bibi Fatima Maasuma SA mwanamke azizi ambaye kaka yake, Imam Reza AS alisema hivi kuhusu adhama yake: "Kila ambaye atafanya ziara katika haram ya Maasuma Alayha Salam mjini Qum, ni kama ambaye amenizuru mimi."

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags