Imam Jawad, Imam wa Tisa kutoka kizazi cha Bwana Mtume SAW
(last modified Thu, 01 Sep 2016 18:08:45 GMT )
Sep 01, 2016 18:08 UTC
  • Imam Jawad, Imam wa Tisa kutoka kizazi cha Bwana Mtume SAW

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni leo hii kwa mnasaba wa kukumbuka siku alipouawa shahidi Imam Jawad AS. Tumeona ni vyema katika dakika hizi za kipindi hiki kuzungumzia fadhail na sifa bora za mtukufu huyo.

Siku ya mwisho ya mwezi wa Mfunguo Pili, Dhulqaad, ulimwengu wa Kiislamu ulishuhudia tukio chungu lililojaa majonzi. Siku hiyo katika mwaka wa 220 Hijria, Imam Muhammad Bin Ali AS anayejulikana kwa lakabu ya Jawad aliuawa shahidi kwa amri ya Muutasim, khalifa wa Bani Abbas. Tunatoa mkono wa pole kwa mnasaba huo tukikuombeni muwe nasi katika makala hii fupi itakayozungumzia baadhi ya mambo muhimu katika maisha yaliyojaa baraka ya mtukufu huyo. Karibuni.

*****

Katika aya ya 40 ya Suratul Ahzab, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamtaja Bwana Mtume Muhammad SAW kuwa ndiye Mtume wa Mwisho. Yaani Utume ulimalizika kwa kuja Bwana Mtume Muhammad SAW. Kutangazwa kumalizika Utume kulikuwa na maana ya kwamba wanadamu wasitarajie kujiwa na Mtume mwingine yeyote baada ya Bwana Mtume Muhammad SAW na wanadamu wote wauane pamoja chini ya bendera ya Uislamu kwani Mwenyezi Mungu hakubali dini yoyote isipokuwa Uislamu. Qur'ani Tukufu nayo ndio mhimili mkuu wa mafundisho ya kidini kwa Waislamu wote. Kiongozi na Imam wa Waislamu naye anateuliwa na Mwenyezi Mungu kupitia Mtume Wake. Abd al-Malik ibn Yusuf al-Juwayni al-Shafi'i maarufu kwa jina la Imamul Haramayn, ambaye ni mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kisunni na mpokezi maarufu wa hadith, amepokea hadithi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW akisema: Mimi ni Bwana wa Mitume, na Ali bin Abi Talib ni Bwana na ni mkubwa wa mawasii. Mawasii wangu baada yangu ni kumi na wawili. Wa kwanza wao ni Ali na wa mwisho wao ni Mahdi. Na katika hadith nyingine maarufu iliyopokewa na Jabir bin Abdullah al Ansari, mmoja wa masahaba wakubwa wa Bwana Mtume Muhammad SAW ambapo Sahaba Jabir anasimulia akisema: Wakati aya ya 59 ya sura ya an Nisaa iliposhuka na kuwataka Waislamu wawatii "ulul-amr" nilimuuliza Bwana Mtume kwamba: Ewe Mtume wa Allah! Tumeshamjua Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, ni wajibu kwetu sasa kuwatambua pia "ulul-amr." Bwana Mtume SAW akanijibu kwa kusema: Ewe Jabir! "Ulul-Amr" ni Maimamu na watu watakaokaimu nafasi yangu baada yangu. Wa kwanza wao ni Ali bin Abi Talib, na baadaye watafuatia wengine kwa utaratibu ufuatao: Hasan bin Ali, Husain bin Ali, Aliyubnil Husain, Muhammad bin Ali ambaye katika Taurati ametajwa kwa jina la Baqir na wewe Jabir utaonana naye ukishakuwa mzee, na wakati wowote utakapoonana naye, mpe salamu zangu. Baadaye watafuatia Jaafar bin Muhammad, Musa bni Jaafar, Ali bin Musa, Muhammad bin Ali, Ali bin Muhammad, Hasan bin Ali na hatimaye atafuatia mwanawe ambaye jina lake litakuwa ni Muhammad kama jina langu na moja ya kuniya yake yaani jina lake la ubaba litakuwa Abul Qasim kama kuniya yangu. Imam huyo atatoweka mbele ya macho ya watu na atakwenda katika ghaiba ya muda mrefu kiasi kwamba watu wenye imani thabiti pekee ndio watakaobakia katika imani yake.

 

Jina la Imam wa tisa ni Muhammad, kuniya yake ni Abu Jaafar na lakabu zake maarufu ni Taqi na Jawad ambazo zinaakisi sifa za taqwa ya kipekee na ukarimu mkubwa aliokuwa nao mtukufu huyo. Baba yake mtukufu alikuwa ni Imam Ridha AS na mama yake mtukufu alikuwa ni Khaizaran.Imam Jawad AS alichukua hatamu za Uimamu mwaka 203 Hijria, baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu. Alichukua Uimamu akiwa chini ya miaka saba. Kwa vile Imam Jawad AS alikuwa wasii wa kwanza kabisa wa Bwana Mtume Muhammad SAW aliyechukua Uimamu akiwa na umri mdogo zaidi, bila ya shaka watu wengi walijiuliza kwamba vipi Imam Jawad angeliweza kuwa Imam wa Waislamu akiwa na umri mdogo kiasi chote hicho tena katika kipindi nyeti na kizito sana walichokuwa wakiishi ndani yake Waislamu? Je, inawezekana mtu mwenye umri mdogo kiasi hicho aweze kuwa Imam wa Waislamu ambaye ni kaimu wa Bwana Mtume SAW? Je, katika nyumati zilizopita, iliwahi kutokezea kitu kama hicho?Majibu ya maswali hayo ni kama ifuatavyo: Ni jambo lisilo na shaka kuwa kipindi cha kuchanua na kukamilika akili na mwili wa mwanadamu kwa kawaida kina umri na miaka yake maalumu, lakini hakuna kizuizi chochote kwa Mwenyezi Mungu Muweza wa kila kitu na Mwingi wa hekima kufupisha muda huo kwa waja wake wateule na kwa kuzingatia maslahi maalumu. Tangu kuanza jamii ya mwanadamu hadi leo hii, kumetokezea watu waliofikia kwenye daraja za juu ya kuongoza umma wakiwa na umri mdogo kutokana na hekima na rehema za Muumba wa kila kitu. Katika Qur'ani Tukufu tunasoma visa vya Mitume kama Nabii Yahya AS kwamba walipewa Utume wakiwa bado wadogo. Aya ya 12 Surat Maryam ni ushahidi wa hayo. Katika sura hiyo hiyo kuna kisa cha miujiza cha Nabii Isa AS aliyezungumza akiwa kitoto kichanga ndio kwanza kimezaliwa. Alitamka maneno matukufu ikiwa ni pamoja na kusema kuwa Mwenyezi Mungu amemjaalia kuwa Nabii. Katika aya za 30 hadi 34 za sura hiyo tukufu tunasoma:30. (Nabii Isa) akasema: Mimi ni mja wa Allah. (Mwenyezi Mungu) amenipa Kitabu na amenijaalia kuwa Nabii.31. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai.32. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu.33. Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.34. Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.

*****

Naye Imam Jawad AS alifikia Uimamu wa kuongoza umma wa Kiislamu akiwa bado mdogo. Umri wake mdogo uliwashangaza watu wengi na hata maulamaa na wasomi wa zamani hizo na wengine hawakuamini. Hata hivyo hali ilikuwa tofauti kwa wafuasi na wapenzi wa Ahlul Bayt AS. Wengi wao waliamini kuwa suala la Uimamu linatoka kwa Mwenyezi Mungu, na suala la umri mdogo kwao wao halikuwa tatizo. Kama ambavyo pia imepokewa katika mapokeo ya kihistoria kwamba baada ya kuuawa shahidi Imam Ridha AS kuna baadhi ya watu walikusanyika katika mkutano mmoja ili kujadiliana kuhusu mrithi wa Imam Ridha AS. Yunus bin Abdurrahman ambaye alikuwa mtu anayeaminiwa na Imam Ridha AS alisema: Tunapaswa kufanya nini hadi mwana huyu wa Imam, yaani Imam Jawad AS atakapokuwa mkubwa? Mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Rayyan bin Salat alisimama na kupinga suala hilo akisema: Mwenyezi Mungu ndiye anayeainisha nani awe Imam, na Uimamu wa Imam Jawad AS unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama uhakika ni huo, basi hata mtoto wa siku moja anaweza kuwa Imam na kama hautoki kwa Mwenyezi Mungu, hata mtu awe na umri wa miaka elfu moja, hawezi kuwa Imam ataendelea kuwa kama watu wengine tu.Hivyo umri mdogo wa Imam Jawad AS haukutia dosari yoyote katika imani ya wafuasi wa kweli wa Ahlul Bayt AS, bali lililokuwa muhimu kwao ni ubora wa elimu na maarifa ambayo alipaswa kuwa nayo Imam. Amma ubora wa kielimu wa Imam Jawad AS ulithibitika mara nyingi wakati khalifa wa Bani Abbas, Maamun, alipoitisha mijadala ya kielimu ya kumpambanisha Imam Jawad AS na maulamaa wakubwa wa zama hizo, na kuwathibitikia wafuasi wa Ahlul Bayt AS ubora wa kielimu aliokuwa nao Imam Jawad AS. Ali bin Ibrahim amepokea hadithi kutoka kwa baba yake akisema: Baada ya kuuawa shahidi Imam wa Nane (Imam Ridha AS) sisi tulikwenda kuhiji Makkah na tulikwenda pia kwa Imam Jawad AS. Wafuasi wengi wa Ahlul Bayt AS nao walikuwa wamekusanyika hapo ili kumpisha Imam Jawad afanye ibada zake. Abdullah bin Musa, ami wa Imam Jawad AS ambaye wakati huo alikuwa mzee mwenye haiba na kipaji chake cha uso kilionyesha nuru ya ibada zake nyingi, alikwenda sehemu hiyo na kuonyesha heshima zake kubwa kwa Imam Jawad AS na kumbusu kipaji chake cha uso. Wakati huo huo alinyanyuka mtu katika kundi hilo na kumuuliza swali Abdullah bin Musa, ami wa Imam Jawad AS. Hata hivyo, Abdullah alitoa jibu lisilohusiana na swali hilo. Imam Jawad AS aliposikia jibu hilo alihuzunika na kumwambia Abdullah bin Musa: Ami yangu mpenzi! Muogope Mwenyezi Mungu! Litakuwa ni jambo zito sana Siku ya Kiyama, wakati mtu atakapokwenda mbele ya Mwenyezi Mungu na akaulizwa kwa nini ulitoa fatwa kwa watu katika mambo asiyo na elimu nayo! Abdullah akasema: Umesema kweli seyyidi yangu! Nitamuomba maghufira Mwenyezi Mungu. Watu waliokuwepo hapo walivutiwa na kushangazwa na majadiliano hayo. Wakamfuata Imam Jawad AS na kumwambia: Seyyid yetu! Je unaturuhusu tukuulize maswali kuhusu matatizo tuliyo nayo? Imam Jawad akasema: Ndio. Nao wakaanza kumuuliza maswali mengi Imam Jawad AS naye akayajibu yote papo hapo, kiukamilifu na bila ya kusitasita.

 

Zama za Imam Jawad AS zilikuwa zama za mapinduzi ya kiutamaduni na ustawi wa kipekee wa kielimu kiasi kwamba Vyuo Vikuu na madarasa na vikao vya kielimu vilienea katika kila kona ya ardhi ya ulimwengu wa Kiislamu. Nicolson, mmoja wa wataalamu wa Kimagharibi wa masuala ya Mashariki ameandika haya kuhusu zama hizo. Kulitokea mapinduzi ya kiutamaduni katika zama za utawala wa Bani Abbas kutokana na kuenea utajiri na kustawi masuala ya kibiashara, kiasi kwamba hadi wakati huo, eneo la Mashariki mwa dunia halikuwa limeshuhudia kitu kama hicho. Hali ilikuwa imestawi kiasi kwamba hima kubwa waliyokuwa nayo watu katika zama hizo ilikuwa ni kutafuta elimu na kufanya utafiti wa kielimu. Wakati huo watu walikuwa wakisafiri katika mabara matatu ya dunia ili kutafuta elimu na halafu walikuwa wanarejea katika maeneo yao kwa ajili ya kuwanufaisha watu wao wakiwa mithili ya mtende wenye matunda mengi. Imam Jawad AS alikitumia vizuri mno kipindi na zama hizo kueneza mafundisho sahihi ya Uislamu na alikuwa na elimu ya kipekee suala ambalo lilizidi kuwaamsha watu na kuonyesha utukufu na ustahiki wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa wakati huo ambao waliamua kumuua shahidi mtukufu huyo ili kuzua kuendelea mwamko huo. Kwa mara nyingine tena tunatumia fursa hii kutoa mkono wa pole kwa wapenzi wote wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW tukimuomba Mwenyezi Mungu aulinde umma wa Kiislamu na fitna za zama hizi. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags