Utawala na uongozi katika fikra za kisiasa za Imam Baqir (as)
Katika siku hizi ambapo mamilioni ya Waislamu wanaelekea katika ardhi tukufu za Makka na Madina kwa ajili ya ibada ya Hija, jina la Mtume wetu Muhammad (saw) na Ahlu Baiti zake watoharifu linatajwa na kuhuishwa zaidi kuliko wakati wowote mwingine.
Siku za ibada ya Hija na kuwepo mahujaji katika miji hiyo mitakatifu kunakumbusha jihadi kubwa ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlul Bait (as) katika kulinda mipaka ya itikadi na dini tukufu ya Kiislamu.
Tarehe 7 Dhulhija inasadifiana na siku aliyouawa shahidi Imam Muhammad Baqir (as), mmoja wa Watu wa Nyumba ya Bwana wetu Muhammad (saw) ambaye katika siku kama hizi za Hija umati mkubwa wa Waislamu ulikuwa ukikusanyika kandokando yake na kufaidika na bahari yake kubwa ya elimu na maarifa yake.
Katika zama hizi ambapo mwamko wa Kiislamu umeyahamasisha mataifa mbalimbali kusimama dhidi ya watawala madikteta na madhalimu, kuzungumzia mitazamo ya Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume Mtukufu kunaweza kufungua upeo mpya na wa wazi zaidi kwa mataifa yanayoendelea kukandamizwa na kudhulumiwa. Hapana shaka kwamba, utawala na uongozi wa umma au taifa lolote una taathira kubwa ambayo haiwezi kupuuzwa katika ufanisi au maangamizi na nakama ya mataifa mbalimbali. Hii ni pamoja na kuwa, ushahidi umethibitisha kwamba, matatizo yanayozisumbua jamii nyingi za wanadamu wa leo ni matokeo ya uongozi mbaya na tawala zisizofaa zinazojali maslahi ya kundi dogo na kupuuza mataifa na umma zao.
Imam Muhammad Baqir (as), kama walivyokuwa Ahlul Bait wengine wa Mtume Muhammad (saw), aliishi katika kipindi kilichotawaliwa na viongozi madhalimu na wasiofaa. Kwa msingi huo moja ya ajenda za kiongozi huyo ilikuwa kupanga stratijia na mkakati wa muda mrefu wa kuweka wazi fikra ya utawala na uongozi katika jamii ya Kiislamu. Alikosoa utendaji wa makhalifa na watawala wa wakati huo na kubainisha wajibu na majukumu ya utawala bora.
Kipindi cha Uimamu wa Muhammad Baqir (as) kilianza mwaka 95 Hijria na kuendelea kwa muda wa miaka 19 na miezi kadhaa. Kutokana na sababu za kihistoria ikiwa ni pamoja na ushindani mkali wa kugombea madaraka kati ya watawala wa Bani Umayyah na Bani Abbas, kulitokea uasi katika maeneo mbalimbali ya mamlaka ya Kiislamu, suala ambalo lilimpa fursa Imam Baqir (as) ya kubainisha na kuweka wazi maarifa sahihi ya Kiislamu wakati watawala wakishughulishwa na vita vya kugombea madaraka. Kipindi hiki cha Imam Baqir na kile cha mwanae mtukufu, Ja'far Swadiq (as), kinaweza kutambuliwa kuwa ni zama za kuchanua utamaduni na maarifa ya Kiislamu. Kwani hakuna Imam yeyote mwingine wa kizazi cha Mtume (saw) aliyepata fursa kama hiyo ya kueleza na kuweka wazi fikra na itikadi sahihi za Kiislamu. Katika kipindi hiki mashinikizo ya kisiasa yaliyokuwa yakiwabana Ahlul Bait wa Mtume yalipungua kidogo licha ya kwamba Imam na wafuasi wake waliendelea kuwa chini ya usimamizi na udhibiti wa watawala wa wakati huo. Katika kipindi cha uimamu wake walitawala makhalifa wanne wa Bani Umayyah, jambo ambalo liliakisi mazingira tofauti ya kisiasa na hali mbaya ya kijamii.
Imam Muhammad Baqir (as) alitumia kipindi hiki kwa ajili ya kufanya mabadiliko na ukarabati katika utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na vilevile kupanga na kuratibu upya mfumo wa kifikra wa Ahlul Bait (as). Lengo hilo lilitimia kupitia mbinu ya kufanya midahalo na mijadala ya kielimu na makundi mbalimbali ya kifikra. Baadhi ya midahalo na mijadala hiyo ilifanyika katika kipindi cha ibada ya Hija huko Makka na Madina, jambo ambalo peke yake linaonesha uhodari wa Imam katika kulingania dini ya Mwenyezi Mungu na umuhimu wa mlinganiaji kutambua mahala na zama bora zaidi kwa ajili ya kazi hiyo.
Msimu wa ibada ya Hija ulikuwa wakati wa kukusanyika wasomi na maulamaa wa makundi mbalimbali mjini Makka. Imam Baqir (as) alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Waislamu masuala ya dunia na Akhera yao; na katika kubainisha masuala ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni alizingatia misingi ya kidini ili wanadamu wasighafilike na ujumbe wao asili hapa duniani ambao ni kufikia ufanisi katika ulimwengu wa Akhera.
Miongoni mwa masuala yaliyopewa umuhimu mkubwa na Imam Baqir katika kipindi hicho ni kubainisha fikra za kisiasa za Uislamu katika medani ya utawala na uongozi. Alisisitiza kuwa, juhudi za marekebisho haziwezi kuzaa matunda katika jamii ambayo hatamu za uongozi wake zinashikwa na watu majahili na wasiofaa. Iwapo tutatazama suala la uongozi na utawala kwa mtazamo huo tutabainikiwa na hakika nyingi kuhusu misimamo ya kisiasa ya Ahlul Bait wa Mtume (saw) na kuelewa ni kwa nini watukufu hao walisimama kidete kwa nguvu zao zote kupambana na watawala madhalimu na waovu.
Imam Baqir (as) amenukuliwa akisema: "Wanadamu wanahitajia kuwepo Mtume na Imam kwa sababu ndio nguzo za masuala yote ya kiroho na kimaada ya dunia." Anasema katika hadithi nyingine kwamba: "Naapa kwa jina la Mola Muumba kwamba tangu Nabii Adam alipofariki dunia, Mwenyezi Mungu hakuiacha dunia hivihivi bila ya kuwa na Imam na (kiongozi) anayewaongoza wanadamu kwenye njia Yake na yeye ndiye huja ya Mwenyezi Mungu kwa watu; hakika dunia haiwezi kubakia bila ya kuwa na huja wa Mola kwa walimwengu." Makusudio ya Imam Baqir katika hadithi hizo ni umuhimu wa uongozi wa kifikra, kijamii na kisiasa katika jamii. Ni kwa sababu hiyo pia ndiyo maana mafundisho ya Uislamu yamesisitiza na kutilia mkazo sana suala la uimamu na uongozi wa jamii ya Kiislamu.
Imam Muhammad Baqir (as) alikosoa pia utendaji wa makhalifa wasiofaa kwa kuweka wazi sifa za viongozi wema na wale waovu. Amesema: "Uongozi wa jamii unamfalia mtu mwenye sifa tatu. Kwanza awe na sifa ya ucha-Mungu ambayo itamlinda kutumbukia katika haramu mbele ya misukosuko ya madaraka na uongozi. Pili awe na sifa ya subira na uvumilivu ambayo itamsaidia kudhibiti hasira na ghadhabu zake, na tatu awe kama baba mwema kwa watu anaowatawala na kuamiliana nao kwa mwenendo mzuri.
Moja ya stratijia za Imam Baqir katika kukabiliana na watawala madhalimu ni kuendesha mapambano hasi na yasiyokuwa ya moja kwa moja na watawala hao. Imam alikata uhusiano na tawala za viongozi wa aina hiyo na kuwanyima suhula ikiwa ni aina fulani ya kulalamika na kupinga utendaji kazi wao.
Imepokewa kwamba, siku moja Imam Baqir alimuusia mtu aliyejulikana kwa jina la Aqaba bin Bashir al Asadi ambaye alitaka mwongozo kuhusu suala la kutumika na kufanya kazi katika serikali ya watawala madhalimu akisema: "Kama hupendi Pepo huko Akhera, basi kubali cheo na nafasi hiyo. Kwa sababu utakuwa mshirika wa mtawala dhalimu anayemwaga damu za watu wasiokuwa na hatia yoyote."
Japokuwa Imam Baqir (as) hakupata fursa nzuri kwa ajili ya kuanzisha mapambano ya moja kwa moja dhidi ya watawala madhalimu na waovu wa zama zake, lakini alifanya jitihada kubwa za kuhuisha roho ya kupambana na watawala wa aina hiyo katika nafsi za wanafunzi na wafuasi wake. Hali hiyo ilimfanya Imam Baqir kuwa marejeo ya watu katika masuala yao ya kielimu, kiroho na kisiasa katika jamii ya Kiislamu; jambo ambalo liliwakasirisha watawala wa Bani Umayyah ambao walianza kutafuta mbinu za kuondoa kizuia hicho mbele yao. Kwa msingi huo mtawala Hisham bin Abdul Malik alipanga njama ya kumuua shahidi mtukufu huyo na katika siku ya terehe 7 Dhilhija mwaka 114 Hijria mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi kwa kupewa sumu.
Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi na wafuasi wa Ahlul Bait (as) kwa mnasaba huu mchungu na wa kusikitisha.