Fikra za Imam Hadi AS katika kubainisha Tauhidi na Uimamu
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujumuika nami katika kipindi hiki maalumu cha makala ya wiki ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Hadi AS.
Nyoyo za waumini zimejawa na furaha kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Hadi (as), ambaye ni mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw), aliyezaliwa tarehe 15 Dhul-Hijjah. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia taufiki ya kuweza kudiriki siku hii na kuweza kustafidi na bahari ya elimu adhimu ya mtukufu huyo. Sambamba na kutoa mkono wa baraka na fanaka kutokana na mazazi ya Imam Hadi (as) ninakuombeni muwe nami kwa dakika hizi chache ili niweze kukubainishieni sehemu ndogo tu ya fikra na maisha ya mtukufu huyo kupitia hidaya na uongozi wake (as), karibuni.
*****************
Maimamu na viongozi wa Mwenyezi Mungu ni shakhsia wakamilifu na wateule ambao maneno, mienendo, akhlaqi na maisha yao ya utukufu, ni somo tosha kwa mwanadamu. Imam Hadi (as) anawasifu viongozi hao wateule wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu kwa kusema: “Wao ni chemchemi ya rehma, hazina ya elimu, waasisi wa utukufu, viongozi wa uongofu na wachaji-Mungu.” Mwisho wa kunukuu. Imam Hadi alizaliwa mjini Madina katika eneo lililokuwa likiitwa ‘Swarya’ tarehe 15 Dhul-Hijjah mwaka 212 Hijiria. Mama yake alikuwa mwanamke mchaji-Mungu aliyeitwa kwa jina la Sammanah. Baba yake Imam Jawad (as) aliuawa shahidi mnamo mwaka 220. Ni kutokana na hali hiyo ndio maana uimamu wa Imam Hadi (as) ukaanza akiwa na umri mdogo huku ukiendelea kwa miaka 33 yaani hadi mwaka 254 Hijiria. Aidha Imam Hadi (as) alikuwa mashuhuri kwa lakabu tofauti, maarufu zaidi ikiwa ni jina la ‘Hadi’ likiwa na maana ya kiongozi. Imam Hadi aliishi katika zama za watawala sita wa Abbasiya ambao ni pamoja na: Muutaswim, Wathiq, Mutawakkil, Muntaswir, Mustaiin na Mu’utazz huku mtawala aliyekuwa na uadui zaidi kwa AhlulBayti wa Mtume (saw) akiwa Mutawakkil. Nafasi ya juu ya kielimu na kimaanawi ya Imam Hadi (as) baina ya Waislamu, ndiyo iliyopalilia zaidi chuki ya watawala wa Abbasiya suala ambalo lilikuwa sababu ya kumfanya mtukufu huyo kuvumilia machungu na matatizo mbalimbali kutoka kwa watawala hao dhalimu.
Kipindi cha uimamu wa Imam Hadi (as) kilikuwa kipindi kipya cha kielimu na kifikra. Harakati za jamii kuelekea kwenye ustawi wa kielimu na kiutamaduni kwa kutegemea mfumo wa fikra mpya za itikadi sanjari na kuingia shubha tofauti za kiakili na kifalsafa zilizoathiriwa na harakati za tarjama, ni hatua muhimu iliyowakabili Waislamu wa zama za Imam Hadi (as). Kila mrengo na kundi lilijishughulisha na nadharia na fikra zake, suala lililofungua mlango wa kuenea kwa fikra potofu katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo Ahlulbayti wa Mtume na licha ya kukabiliwa na mashinikizo kutoka kwa watawala waliweka misingi imara na ya kimantiki, ambapo kila kulipojitokeza shubuha yoyote kuuhusu Uislamu, basi watukufu hao walikuwa wakitoa majibu mwafaka ya kukabiliana na shubuha hizo. Katika kipindi hiki muhimu Imam Hadi (as) sanjari na kuchora ramani muhimu kwa ajili ya mustakbali wa ulimwengu wa Kiislamu, alikuwa akijishughulisha na kutoa darsa na maarifa sahihi kutoka kwa Mtukufu Mtume Muhammad (saw), ili kwa njia hiyo aweze kukidhi mahitaji ya kifikra ya vizazi vya baadaye.
Moja ya majukumu muhimu ya mtukufu huyo, ilikuwa ni kubainisha misingi sahihi ya itikadi ya Kiislamu. Hii ni kwa kuwa katika kipindi kile kulienea upotofu na shubuha kuu za kifikra hasa katika kadhia ya Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika jamii ya Kiislamu, suala ambalo lilihatarisha imani za Waislamu wa kawaida. Shubuha hizo zingeweza pia kubadili mwelekeo sahihi wa jamii ya Kiislamu sanjari na kuathiri malengo yaliyoainishwa na Mtukufu Mtume (saw). Aidha Tawhid na kumjua Mwenyezi Mungu, ni maudhui muhimu katika Uislamu na katika maktaba ya Ahlulbayti wa Mtume. Imam Hadi (as) akiwa mmoja wa wasimamizi walioiongoza meli ya uongofu ya umma wa Kiislamu kuelekea kilele cha ukamilifu, alifanya juhudi kubwa katika kubainisha suala hilo na kuweka wazi kwamba, itikadi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mmoja ni yenye kuathiri maisha ya kila mwanadamu duniani. Itikadi sahihi juu ya Tawhid, huinyoosha njia ya uchaji-Mungu ya mwanadamu kufikia kilele cha maisha ya Tawhid. Nukta muhimu inayopasa kuzingatiwa hapa ni hii kwamba, kamwe maisha ya Tawhid hayaondoki nje ya muhimili wa hidaya ya Mwenyezi Mungu na kwenda kwenye njia ya mafundisho yasiyo na maana. Huo ndio uongofu uliokuwa ukisisitizwa na Mtume na baada yake Maimamu wa Ahlulbayti (as).
Imam Hadi (as) alikuwa akisisitiza kuwa Uislmu ni dini yenye fikra na mtazamo sahihi na ulio chanya. Aidha aliwataka Waislamu kujiepusha na maneno yasiyo na faida na badala yake kujitahidi kuzungumza maneno yanayoendana na akili salama. Miongoni mwa juhudi kubwa za kielimu zilizotekelezwa na mtukufu huyo, ni uandishi wa risala juu ya misingi ya itikadi, risala ambayo ilijibu maswali kuhusiana na shubuha mbalimbali za kiitikadi kwa watu wa Ahwaz (kusini magharibi mwa Iran). Itakumbukwa kuwa katika kipindi cha Imam Hadi (as) kulikuwepo kundi la watu waliokuwa na itikadi kwamba Mwenyezi Mungu ana mwili. Imam alikabiliana vikali na fikra hizo potofu kwa kusema: “Wafuasi wa Ahlulbayti hawaitakidi juu ya Mwenyezi Mungu kuwa na mwili, kwani kuamini hivyo hupelekea kufananishwa Mwenyezi Mungu na vitu vingine vyenye mwili. Na kitu chenye mwili bila shaka kimetokana na kitu kingine na Mwenyezi Mungu ametakasika na ufananisho huo. Kwani kuwa na mwili humuwekea muhusika mipaka ya mahala, muda na mabadiliko mengine mithili ya uzee na ukuukuu, katika hali ambayo dhati ya Mwenyezi Mungu imetakasika na sifa hizo.” Tazama kitabu cha Tawhid Sheikh Swaduq ukurasa wa 97.
Kama vile ambavyo Tawhidi, ambao ni msingi muhimu wa mafundisho ya Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, ilikuwa ikipigwa vita na kuhujumiwa na fikra potofu, Qur’an nayo ilikabiliana na aina tofauti ya fikra na shubuha potofu. Katika kipindi fulani, shubuha ya tahrif ya Qur’an ilienea katika ndimi za watu kwa lengo la kutaka kukitia dosari kitabu hicho kitakatifu cha mbinguni, shubuha ambazo hadi leo zingali zinaenezwa na kundi fulani katika Uislamu kwa lengo la kuibua farqa baina ya Waislamu. Katika kipindi cha Imam Hadi (as) pia fikra hiyo ilishika kasi, suala lililomfanya mtukufu huyo kukitetea kwa nguvu zake zote Kitabu hicho kitukufu ambacho ni turathi ya pekee ya Utume wa Mtume Muhammad (saw). Imam alitumia dalili za aya kukadhibisha habari ya kuwepo tahrif ndani ya Qur’an Tukufu.
Imani ya jabri, yaani kuamini kuwa mwanadamu hana uhuru wala hiari katika matendo yake, ni miongoni mwa fikra potofu zingine zilizoenea katika kipindi cha Imam Hadi (as). Mara nyingi fikra hizo zilikuwa zikienezwa kati ya watu na watawala wa Bani Abbasi kwa lengo la kuwaondolea watawala dhima ya lawama katika utendaji kazi na maamuzi yao, suala ambalo lilikuwa likiwafanya wananchi kusalimu amri na kukubali dhuluma na ukandamizaji wa watawala hao. Katika kukabiliana na fikra hizo za jabri Imam Hadi (as) alisema kuwa mwanadamu hajalazimishwa moja kwa moja, wala kupewa uhuru wa moja kwa moja katika utendaji wake. Kwa utaratibu huo Imam alikuwa akiwabainishia watu kwamba, wanadamu ni wenye mchango mkubwa katika masuala ya kijamii, kisiasa na katika kuiainisha mustakbali wao wenyewe kinyume na fikra za jabri. Na hapo, imam akawa amewaondoa watu katika minyororo ya kujisalimisha mbele ya madhalimu.
Msingi wa jukumu la uimamu na uongozi baada ya Mtume (saw) ulikuwa ni kulinda misingi ya dini katika vipindi tofauti kutokana na hujuma ya shubuha. Tunaweza kusema kuwa, sababu kuu ya kuongezeka makundi potofu ndani ya umma wa Kiislamu, ni kutofahamika vyema nafasi ya uimamu wa Ahlulbayti wa Mtume. Suala ambalo kwa hakika ndilo limeuletea changamoto nyingi na matatizo chungu nzima umma wa Kiislamu. Kile ambacho kinashuhudiwa hii leo katika pembe mbalimbali za dunia, kinatokana na mtazamo binafsi kuhusu mafundisho ya Kiislamu na kutoyarejea mafundisho sahihi ya vizito viwili vilivyosisitizwa na Mtume Muhammad (saw) yaani Qur'an na Ahlulbayti wake. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana Imam Hadi (as) akachukua hatua muhimu ya kuainisha nafasi ya uimamu baada ya Mtume. Dalili ya wazi iliyowekwa na Imam katika kumuelekeza mtu kufahamu nafasi ya uimamu, ni Ziara ya 'Jamiat Kabirah' ambayo inahesabiwa kuwa miongoni mwa turathi adhimu za mtukufu huyo. Katika ziara hiyo, Imam Hadi (as) alitumia njia maalumu katika kubainisha suala la uimamu na wakati huo huo kubatilisha fikra ya ghuluwwu yaani kupindukia mipaka katika kuwapenda Ahlulbayti, na hata mara nyingine kuwafikisha katika daraja ya uungu. Allamah Majlisi, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu analielezea suala hilo kwa kusema kuwa, Imam alikusudia katika ziara hiyo kuwaonya wafuasi wa Ahlulbayti wasije wakakumbwa na ghuluwwu na wakaghafilika na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Sisitizo la Imam juu ya Tawhid linabainisha ukweli huu kwamba, uongozi na uongofu ni mwendenelezo wa njia ya Mwenyezi Mungu, na kwamba maimamu na viongozi wema wa Mwenyezi Mungu, ni waja Wake wateule ambao waliainisha na kuonyesha kwa kauli na vitendo, njia ya kufikia saada na ukamilifu.
Kwa mara nyingine tena Radio Tehran inatoa mkono wa heri na fanaka kwa kuzaliwa Imam Hadi (as) na tunamuomba Mwenyezi Mungu auongoze umma wa Kiislamu katika njia iliyobainishwa na Mtume na Ahlul Bait wake.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuhu.