Ghadir, hakika ing'arayo katika kitovu cha historia
Assalamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa miongoni mwa wenye kushikamana na Wilaya ya Ali bin Abi Talib na kizazi chake kitoharifu na maasumu; na mpaka pale roho zetu zitakapokuwamo viwiliwilini mwetu tutaendelea kuishukuru neema hii kwa kuikariri aya ya 43 ya Suratul A'araf isemayo:" Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingelikuwa Mwenyezi Mungu hakutuhidi.
Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Katika kuonyesha ushukurivu wetu kwa neema ya Idul-Ghadir, tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tunakukaribisheni wapenzi wasikilizaji kusikiliza kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba huo.
********
Katika kipindi cha miaka 23, Bwana Mtume SAW alisumbuka na kufanya jitihada kubwa mno hadi kuuwezesha kuchipua na kustawi mmea mchanga wa dini tukufu ya Uislamu. Katika muda wote huo alivumilia mateso, machungu na misukosuko mingi na hakufanya ajizi hata kwa lahadha ndogo katika kutekeleza jukumu na wajibu wake wa kufikisha risala na wito wa Mola wake. Katika mwaka wa kumi Hijria, ujumbe kutoka ulimwengu wa ghaibu ulimfikia kumjulisha kwamba muda si mrefu ataondoka katika ulimwengu huu. Kwa hivyo akafanya juhudi za mtawalia kuhakikisha anatekeleza kwa ukamilifu kila lile lenye ulazima kwa ajili ya utukukaji wa dini ya Uislamu na lenye maslaha kwa Waislamu. Suala la Ukhalifa na uongozi baada yake ni moja ya mambo muhimu zaidi yaliyokuwa yakimshughulisha Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa sababu yeye ni Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu na baada yake yeye hatokuja Mtume mwengine atakayetumwa na Yeye Mola. Kwa hiyo mtu ambaye atabeba jukumu la utawala na uongozi wa watu baada yake anapaswa awe mja mtiifu kwa Allah, dhihirisho la ukamilifu wa utu na aliyeepukana na kila aina ya upotofu ili awe na ustahili wa kuuongoza umma baada ya Bwana Mtume.
Kwa sababu hiyo katika Hija yake ya mwisho iliyojulikana pia kama Hijjatul-Wida'a, Bwana Mtume Muhammad SAW alimtangaza rasmi kwa Waislamu wote kiongozi wa umma baada yake.Tukio la kutambulishwa khalifa wa Bwana Mtume katika Hija yake ya kuaga limeelezewa katika vitabu na maandiko ya historia kama ifuatavyo: Baada ya kumalizika utekelezaji wa amali za Hija Bwana Mtume SAW alianza safari ya kuelekea Madina. Wakati alipofika eneo la Raabigh katika mahali paitwapo Ghadir Khum, Jibril mwaminifu alimteremkia na kumfikishia ujumbe unatoka kwa Mwenyezi Mungu usemao: "Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi". Bwana Mtume ambaye alikuwa akielewa unafiki wa baadhi ya watu, na akawa na wasiwasi juu ya mustakabali wa umma wa Kiislamu, alitaamali kidogo. Katika lahadha hiyo Jibril mwaminifu aliteremka ardhini kwa mara ya pili na kumsomea Bwana Mtume sehemu inayofuata ya aya inayosema: "Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. "Bwana Mtume alikuwa akitafakari ni vipi aufikishe ujumbe huo, malaika Jibrili akamteremkia kwa mara nyengine tena na ujumbe wa Allah usemao: "Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri. "Hapa linajitokeza swali hili, kwamba ujumbe huo ni muhimu kiasi gani ikiwa hautofikishwa kwa watu, Bwana Mtume atakuwa kwa kweli hajafikisha risala ya Mola wake?
Ni nukta gani muhimu ambayo lazima ielezwe na ambayo kwa ajili ya kufikishwa kwake Mwenyezi Mungu anamtoa wasiwasi Mtume wake mtukufu na kumpa hakikisho kuwa atamlinda na madhara ya watu? Bila ya shaka makusudio ya madhara ya watu si madhara ya kumdhuru kimwili au kimali n.k, kwa sababu Bwana Mtume alikuwa shujaa zaidi ya watu wote, kwani hakuwahi hata mara moja kuingiwa na chembe ya hofu katika medani za vita na wakati mapigano yalipokuwa yameshtadi na kupamba moto. Hofu aliyokuwa nayo mtukufu huyo ilikuwa ni ya kuchelea madhara kwa asili ya dini yenyewe yatakayosababishwa na baadhi ya watu waliokuwa wamezongwa na ujahili na hali ya unafiki. Ili kutekeleza amri hiyo ya Mwenyezi Mungu, na licha ya joto kali lenye kuunguza na lisiloweza kuhimilika la Ghadir Khum, Bwana Mtume alitoa amri msafara wa mahujaji usimame mahala hapo. Wakati umati mkubwa wa watu ulipokuwa umejumuika hapo Bwana Mtume SAW alipanda juu ya mahali palipoinuka, na baada ya kumhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu alisema: Hadi wakati huu Jibrili amesha nishukia mara tatu na kunipa amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kunitaka nisimame katika ardhi hii na kuhitimisha ufikishaji wa risala yake. Je mimi si bora zaidi kwenu kuliko nafsi zenu wenyewe? Wote wakajibu kwa kusema: Ndiyo. Bwana Mtume akaendelea kuwauliza: Je mimi si Mtume na kiongozi wenu? Wote kwa pamoja wakayathibitisha maneno hayo. Baada ya hapo akaushika mkono wa Ali bin Abi Talib, akauinua juu na kusema:"Yule ambaye mimi namtawalia mambo yake, basi huyu Ali anamtawalia mambo yake". Waandishi wa historia wameandika kuwa watu waliokuwa wamehudhuria mahala hapo walikuwa ni baina ya elfu 80 hadi laki moja na ishirini. Baada ya tukio hilo ndipo ilipoteremshwa aya ya tatu ya Suratul Maida isemayo:" Leo walio kufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Tukio hilo muhimu liliwafanya makafiri wakate tamaa. Watu ambao walikuwa wakingojea Bwana Mtume afariki dunia ili kwa kukosekana kiongozi atokanaye na uteuzi wa Mola waweze kutekeleza malengo yao maovu. Lakini katika tukio la Ghadir Khum, kwa kutangazwa ukhalifa wa Ali (AS), ambaye kama alivyokuwa Bwana Mtume, alikuwa amepambika kwa sifa za ushujaa, umaizi, subira na uthabiti, tamu ya matumaini waliyokuwa nayo makafiri iligeuka kuwa shubiri. Tukio hili adhimu lilionyesha kuwa kwa mtazamo wa Uislamu, mtawala na kiongozi wa umma wa Kiislamu anapaswa awe mtu mwema, mweledi, mudiri, mjuzi na mwenye uchungu wa dini; na si kila mtu anaweza kuteuliwa kushika wadhifu huo muhimu.Suala la ukhalifa na uongozi baada ya Mtume wa mwisho wa Allah lilikuwa na umuhimu mkubwa mno kiasi kwamba hata kabla ya tukio la Ghadir Khum, lilishawahi kuashiriwa na Bwana Mtume katika nyakati na minasaba tofauti. Kwa hakika tokea alipopewa jukumu na Mola la kuwatangazia na kuwalingania Uislamu jamaa zake wa karibu Bwana Mtume SAW alilizungumzia suala la khalifa baada yake.
Baada ya kuwalingania jamaa na watu wake hao wa karibu Bwana Mtume aliwaambia: "Enyi wana wa Abdulmuttalib, naapa kwa Mwenyezi Mungu simjui mtu yeyote miongoni mwa Waarabu ambaye ameieletea kaumu yake kitu bora kuliko kile ambacho mimi nimekeuleteeni nyinyi. Si kinginecho nilichokuleteeni ila ni kheri ya dunia na akhera, na Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikulinganieni jambo hilo. Basi yeyote kati yenu atakayenisaidia katika jambo hilo atakuwa ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu juu yenu." Katika hadhara ile ile Ali bin Abi Talib, pamoja na kwamba alikuwa kijana chipukizi alionyesha uaminifu na kujitolea kwake nafsi yake kwa ajili ya Bwana Mtume, akasema kuwa atamsaidia mtukufu huyo katika utekelezaji wa jukumu alililopewa na Mola. Na kwa hivyo katika majlisi na hadhara hiyo akatambulishwa kuwa khalifa wa Mtume wa Allah. Baada ya hapo pia katika kipindi kilichofuatia cha miaka ya baada ya hijra ya Bwana Mtume kuhamia Madina, suala la ukhalifa wa Ali (AS) baada ya Mtume lilikaririwa na Bwana Mtume kwa kiwango ambacho takribani watu wote wa Madina walikuwa na uelewa wa suala la ukhalifa wa Ali (AS).
Tukio la Ghadir ni tukio mashuhuri mno, na hakuna mtu yeyote awezaye kukadhibisha kujiri kwa tukio hilo muhimu la kihistoria. Sayyid Murtadha Alamal Huda, mwanazuoni mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu ameandika kuhusiana na suala hili kwa kusema:"Mtu atakayetaka ushahidi wa ukweli wa habari hii ni sawa na mtu anayetaka ushahidi wa ukweli wa habari ya vita na matukio maarufu yaliyotokea katika maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; na ni sawa na kusema kwamba anatilia shaka tukio lenyewe la Hijjatul-wida'a, kwa sababu yote hayo mawili yana umashuhuri wa kiwango kimoja". Maulamaa wakubwa wa Ahlu Sunnah, nao pia wameinakili hadithi ya tukio la Ghadir Khum kwa sanadi na mapokezi tofauti. Kwa kutoa mfano, Imam Ahmad bin Hanbal, mmoja wa maimamu wa madhehebu nne za Kisuni amemnukuu katika kitabu chake kiitwacho Al Musnad mmoja wa masahaba wa Mtume aitwaye Zaid bin Arqam akisema:"Tulikuwa tumekusanyika pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu katika bonde liitwalo bonde la Khum, kisha akatoa amri ya kusali. Hapo tukasali Sala ya Adhuhuri pamoja na mtukufu huyo, kisha akasoma khutba; na katika hali ambayo kitambaa kilikuwa kimetundikwa juu ya mti ili aweze kuwa kivulini na kutopigwa sana na mwanga wa joto la jua lenye kuunguza, Bwana Mtume alisema: Je hamjui? Je hamshuhudii kuwa mimi ni bora zaidi kwa kila muumini kuliko nafsi yake mwenyewe? Wote wakasema: Ndiyo! Akasema: Kila yule ambaye mimi ninamtawalia mambo yake, huyu Ali anamtawalia mambo yake, Ewe Mola mpende kila mwenye kumpenda na mfanye adui kila mwenye kumfanyia uadui".Hakim Naishaburi, naye pia amenukuu kutoka kwenye vitabu viwili vya maulamaa wakubwa wa Kisuni Bukhari na Muslim ya kwamba:"Wakati Mtume wa Allah alipokuwa anarejea kutoka kwenye Hijjatul-Wida'a alisimama Ghadir Khum na kutoa amri watu wakusanyike chini ya miti. Kisha akasema: Karibuni hivi Mola wangu ataniita na mimi nitaitika wito. Nimekuachieni vitu viwili vyenye thamani kubwa ambapo kimoja ni kikubwa zaidi ya kingine: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, basi angalieni mtaamiliana navyo vipi baada yangu. Hakika viwili hivi havitengani abadani hadi vitakapoingia kwangu katika hodhi". Kisha akasema, Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla ni mwenye kunitawalia mimi mambo yangu, na mimi ni mwenye kumtawalia kila muumini mambo yake. Kisha akaushika mkono wa Ali na kusema: Kila ninayemtawalia mambo yake, basi huyu Ali anamtawalia mambo yake. Ewe Mola! Mpende atakayeikubali Wilaya yake na mfanye adui kila atakayemfanyia uadui". Maulamaa wengine wengi wa Kisuni kama Tirmidhi, Ibnu Majah, Ibn Asaakir, Ibn Naiim, Ibn Athir, Kharazmi, Suyuti, Ibn Hajar, Haithami, Ghazali pamoja na Bukhari wamelitaja tukio la Ghadir katika vitabu vyao. Abu Sa'ad Mas'uud bin Nasir Sajistani, mmoja wa maulamaa wa Kisuni ameeleza katika kitabu chake kiitwacho Ad Dirayah fii Hadithil Wilayah kuwa ameinukuu hadithi hii kutoka kwa masahaba 120 wa Bwana Mtume. Kwa hivyo sanadi ya hadithi ya Ghadir ni madhubuti na ya yakini kwa kiasi ambacho hakuna mtu anayeweza kuikana na kuficha uhakika wake. Abdulfatah Abdul Maqsud, mwandishi na mhakiki wa Kimisri ameeleza haya katika kitabu chake alichoandika kuhusu Imam Ali (AS):" Hadithi ya Ghadir, bila ya shaka yoyote ni hakika isiyoweza kubatilishwa, inga'rayo na kuangaza mithili ya mwanga wa mchana". Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.