Kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatimatuz Zahra SA
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatima Zahra SA binti mtukufu wa Bwana Mtume SAW na mwanamke bora duniani na Akhera, mwanamke ambaye ni kigezo na ruwaza njema.
Amani iwe juu yako Ewe Fatmatuz Zahra mwanamke bora wa duniani na Akhera, Bibi wa wanawake wa peponi, Mtukufu as-Sidiqah at-Twahirah Fatimatuz Zahra (Salaamullahi Alayha). Ni matumaini yetu kuwa mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki maalumu kutegea sikio yale tuliyokuandalieni kwa leo.
Mwezi 3 Mfunguo Tisa Jamaduth Thani mwaka wa 11 Hijria yaani ikiwa imepita miezi mitatu tu na ushei tangu kufariki dunia Bwana Mtume SAW, ilikuwa ni siku ambayo Bibi Fatmatuz Zahra AS alizidiwa na maradhi na huzuni kubwa kutokana na masaibu na mabalaa aliyokumbana nayo tangu alipoaga dunia baba yake kipenzi na kurejea kwa Mola wake. Kwa hakika hizi zilikuwa lahadha na nyakati za mwisho za umri uliojaa baraka wa binti huyu wa Bwana Mtume ambaye ni mke wa Imam Ali AS na mama wa Imam Hassan na Hussein AS.
Huzuni na ghamu ya kuondokewa na baba yake kipenzi kwa upande mmoja, na masaibu aliyokumbana nayo baada ya kifo cha baba yake mtukufu kwa upande wa pili, yalimlemaza kiafya na kumfanya ashindwe kuamka kutoka katika tandiko lake. Katika lahadha hizi za mwisho za maisha yake, kitu pekee kilichokuwa kikimpa utulivu ni ile ahadi ya Bwana Mtume (rehema za Allah ziwe juu yake na Aal zake) kwake wakati anaaga dunia ambapo alimwambia: “Ewe binti yangu kipenzi! Baada yangu wewe ndiye utakayekuwa mtu wa kwanza kutoka katika familia yangu ambaye atanifuata.”
Katika masiku ya baada ya kufariki dunia baba yake, Bibi Fatimatuz Zahra SA alikuwa na majukumu na masuuliya makubwa. Kwa hakika Fatimatuz Zahra alikuwa mwanamke aliyejipamba kwa sifa za kipekee ambazo zilimtofautisha na wanawake na wanaume wote isipokuwa Mtume SAW na Imam Ali bin Abi Twalib AS. Mwanamke mwema huyu alijipamba na sifa zote njema na kufikia daraja ya juu ya uchaji Mungu. Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema:
“Kila mara Fatima alipokuwa akisimama katika mihrabu na mbele ya Mwenyezi Mungu, nuru yake ilikuwa ikiwaangazia Malaika mbinguni kama vile nuru ya nyota inavyowaangazia watu wa ardhini; na Mwenyezi Mungu husema: Enyi Malaika Wangu mtazameni mja wangu Fatima, kiongozi wa waja wangu ambaye amesimama mbele yangu na mwili wake unatetemeka kwa khofu juu yangu na anafanya ibada kwa ajili yangu hali ya kuwa moyo wake umejaa khofu, unyenyekevu na khushui. Ninakushuhudisheni kwamba, nimewapa amani wafuasi wake mbele ya moto wa Jahanamu.”
Baada ya kufariki dunia mbora wa viumbe Bwana Mtume SAW, Bibi Fatimatuz Zahra SA siku baada ya siku alikuwa akidhoofika. Imam Swadiq AS amenukuliwa akisema kuwa, ghamu na huzuni ya kuondokewa na baba yake ilimzidi nguvu na kumlemea mwili wake. Malaika Jibril AS alikuwa akimjia na kumpa mkono wa pole kutokana na msiba wa kuondokewa na baba yake kipenzi na alikuwa akimpa khabari kuhusiana na baba yake, daraja na nafasi yake peponi na vile vile matukio ambayo yataikumba familia yake baada ya mbora huyo wa viumbe kurejea kwa Mola wake. Imamu Ali AS alikuwa akiandika kile alichokuwa akisikia kutoka kwa Jibril AS.
Aidha kabla ya hapo, Bibi Fatima SA alikuwa akizungumza na Malaika na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akapewa lakabu ya Muhaditha. Imam Jaafar Swadiq AS amenukuliwa akisema: Fatima AS aliitwa Muhaditha kutokana na kuwa Malaika kutoka mbinguni walikuwa wakishuka na kuja kuzungumza naye kama ilivyokuwa kwa Mariam bint Imran AS.
Kwa hakika Fatimatuz Zahra AS alikuwa mtoto wa pekee wa Mtume wakati mbora huyo wa viumbe anaaga dunia na kurejea kwa Mola wake. Bibi Fatima alikufa shahidi na kuaga dunia akiwa na umri wa miaka 18 na akiwa ni mama asiye na mithili kwa watoto wanne. Kwa hakika binti huyu wa Mtume anajulikana katika historia ya Uislamu kuwa ni mwanamke wa kipekee, ruwaza na kiigizo chema ambaye aling’ara katika nyanja mbalimbali. Adhama na utukufu wa Bibi Fatima unadhihirika wazi katika riwaya na hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu watoharifu AS. Bibi Aisha mke wa Mtume SAW amepokea hadithi kutoka kwa Mtume SAW inayosema: Viongozi wa wanawake wa peponi ni wanne: Mariam bint Imran, Fatima bint Muhammad SAW, Khadija bint Khuwailid na Asia bint Muzahim mke wa Firauni.
Kwa upande wa ibada na uchaji Mungu, Bibi Fatima alikuwa amekwea na kufikia daraja ya juu kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu anamhutubu Mtume SAW akimwambia: Ewe Mtume SAW lau usingelikuweko wewe basi nisingeliumba ulimwengu, na kama Ali asingekuweko nisingekuumba wewe na kama Fatima asingekuweko basi nisingelikuumbeni nyinyi watu wawili.”
Bibi Fatimah AS anazingatiwa kuwa ni mwanamke wa kutolewa mfano katika dini ya Kiislamu, na pia ni kiigizo chema kwa kila mwanamke anayetafuta mafanikio katika maisha yake. Bibi Fatima binti Muhammad SAW ndiye mwanamke bora ulimwenguni aliyezaliwa na kupata malezi katika nyumba iliyokuwa ikishuka ndani yake Wahyi kutoka mbinguni. Aliyepata malezi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye ndiye kiumbe bora kabisa kuliko viumbe wote duniani, kwa umbo na kwa tabia. Amepata malezi kutoka kwa Bwana Mtume Mtukufu ambaye Mwenyezi Mungu amesema katika Qur’ani Tukufu: “Hakika yako wewe Muhammad uko juu ya tabia bora kabisa” na pia amesema: Hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote.
Naam, Bibi Fatima alihitimu mafunzo ya Uislamu katika madrasa ya Utume, na kutokana na mafunzo hayo aliweza kufikia daraja ya juu na tukufu. Katika kuthibitisha ubora wa Bibi Fatima, Mtume Muhammad (rehema za Allah ziwe juu yake na Aal zake) amenukuliwa akisema, "Hakika Mwenyezi Mungu huwa radhi kwa kuwa radhi Fatimah, na huchukia kutokana na kuchukia kwa Fatima.”
Kutokana na daraja kubwa aliyo nayo Bibi Fatimah katika umma wa Nabii Muhammad SAW, imekuwa ni wajibu kwa kila mwanamke duniani kuiga mwenendo wa Bibi huyu mtukufu katika maisha yake, ajing'arishe kwa nuru yake nzuri na afuate nyayo zake ambazo zitamuelekeza kwenye mafanikio na utukufu. Hakika Bibi Fatima AS, ni mfano wa kila utukufu na kila jema. Mwanamke yeyote atafanikiwa iwapo ataamua kufuata mwenendo wa Bibi Fatmah SA, na kinyume chake ni kuwa, kila mwanamke ataangamia iwapo ataamua kujichagulia mwenendo wake au kuiga usiokuwa mwenendo wa Bibi Fatima AS.
Kwa upande wa maswahaba wa Mtume Muhammad (radhi za Allah ziwe juu yao) pia kumenukuliwa maneno mengi kuhusiana na utukufu wa Bibi Fatimatuz Zahra (Alyhas Salaam). Wanafikra mbalimbali nao hata wasio Waislamu wamezungumzia utukufu wa bibi huyo mbora.
Louis Massignon mmoja wa wanafikra wa Kifaransa na mtaalamu wa masuala ya Mashariki amenukuliwa akisema: "Dua za Nabii Ibrahim AS zilitabiri kuja nuru 12 ambazo zote zinatokana na Faatima... Taurati ya Musa imetoa bishara njema ya kuja Muhammad SAW na binti yake mwenye baraka nyingi na ndugu wawili wa kiume kama Ismail na Ishaq (yaani Hasan na Husain)... Na Injili ya Isa AS imetabiri kuja Ahmad SAW ambaye atazaa binti mwenye Baraka nyingi." Mwisho wa kunukuu.
Bibi Fatimatuz Zahra alikuwa ni mke wa Imam Ali AS aliyejitolea kikamilifu kwa ajili ya mumewe, na mama mwenye busara na hekima nyingi wa Hasan na Husain, mabwana wa vijana wa peponi. Moja ya lakabu za Bibi Faatimatuz Zahra SA ilikuwa ni Mardhiyyah. Huyo ni bibi mtukufu ambaye katika muda mfupi wa umri wake alikuwa ni chimbuko la baraka nyingi kwa Uislamu na Waislamu. Bila ya shaka yoyote kusoma sira na maisha ya mtukufu kama huyo kuna umuhimu na ibra nyingi kwa kila mtu. Maisha yaliyojaa baraka ya bibi huyo mtukufu ni kigezo bora katika kila nukta yake.
Kabla ya kunukuu kauli mbalimbali zilizotolewa kuhusu binti huyo mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW tunapenda kusema tena machache kuhusu bibi huyo mtukufu. Fatima, alikuwa binti mdogo zaidi na kipenzi zaidi wa Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW kimebakia hadi leo hii kupitia kwa binti yake huyo. Faatimatuz Zahra SA alizaliwa na kukulia kwenye nyumba ya wahyi na Utume. Mwalimu wake wa Qur'ani alikuwa ni baba yake, Bwana Mtume Muhammad SAW na mlezi wake alikuwa ni mwenyewe Mtume Mtukufu aliyemjenga binti yake huyo kwa sifa bora kabisa za kibinaadamu na akawa msingi wa hekima na mafundisho mengi matukufu.
Fatimatuz Zahra alipambika kwa elimu na sifa bora ambazo hajawahi kuwa nazo mwanamke mwengine yoyote na ndio maana Bwana Mtume Muhammad SAW akanukuliwa akisema, Fatima ni mbora wa wanawake wote wa dunia mbili. Fauka ya hayo, Bibi Faatimatuz Zahra alikuwa ameimarika kwa fani na elimu zote zilizokuweko wakati huo katika bara Arabu. Alikuwa akipoza majeraha ya baba yake kwa njia bora kabisa katika medani za vita na mara nyingi alifanya kazi zake zote za nyumbani bila ya kuhitaji msaada wa mtu mwingine na katika upande wa malezi ameitunuku jamii ya mwanadamu vijana bora kabisa Hasan na Husain AS. Hakuwa akizungumza ila panapokuwa na haja ya kuzungumza na hakunena ila neno la haki. Hakuwa akisema kitu madhali hajaulizwa. Huyo kwa ufupi ndiye binti wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Bibi Faatimatuz Zahra SA.
Amma tukija katika mitazamo ya watu wengine kuhusu Siddiqatul Kubra yaani Bibi Fatimatuz Zahra SA kwa hakika kuna kauli nyingi zimenukuliwa kutoka kwa Masahaba wa Bwana Mtume Muhammad SAW, kutoka wa wanavyuoni wakubwa wa Kiislamu na kutoka kwa wanafikra wengine hata wasio Waislamu.
Abu Abdullah Muhammad bin Ismail al Bukhari amenukuu hadithi katika kitabu chake maarufu cha Sahih Bukhari kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW akisema: Fatima ni sehemu ya mwili wangu. Yeyote atakayemkasirisha Faatima amenikasirisha mimi. Katika sehemu nyingine Imam Bukhari ananukuu hadithi ya Bwana Mtume akisema: Faatima ni Bibi wa mabibi wa peponi.
Imam Ahmad bin Hambal, mmoja wa wanavyuoni wakubwa wa Kisuni na Imam wa Madhehebu ya Hambal na ambaye mwaka 780 Milaadia alikuwa mwanafunzi wa Imam Shafi amenukuu hadithi kwa sanadi yake maalumu kutoka kwa Malik bin Anas akisema: "Miezi sita kamili Bwana Mtume Muhammad SAW kila siku alipokuwa anatoka msikitini kwenye sala ya Alfajiri alikuwa akipita mbele ya nyumba ya Faatima na akisema: Sala! Sala! Ee Ahlulbayt." Na baada ya hapo alikuwa anasoma aya ya 33 ya Suratul Ahzab inayosema: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Ahlul Bayt (watu wa nyumba ya Mtume), na kukusafisheni barabara.
Na katika hadithi nyingine Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema: Hakuna mtu yeyote aliyefanana na Mtume katika kuzungumza kuliko Faatima. Kila alipokuwa anakuja kuonana na baba yake, Bwana Mtume alikuwa akisimama mahala alipokuwa amekaa ili kuonyesha heshima yake kwa Faatima, akimshika mkono wake na kuubusu na akimuweka kwenye sehemu maalumu karibu naye, na kila wakati Bwana Mtume alipokuwa anakwenda kwa Bibi Faatima naye alikuwa akifanya vivyo hivyo.
Mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu Fakhrur Razi, swahib wa tafsiri maarufu ya Qur'ani Tukufu yaani Tafsirul Kabir amenukuu mitazamo tofauti wakati alipotoa tafsiri na ufafanuzi kuhusu sura tukufu ya al Kawthar. Ameandika: Miongoni mwa maana za neon Kawthar ni wana wa Bwana Mtume Muhammad SAW kupitia kwa Bibi Fatimatuz Zahra SA. Ameandika kama ninavyonukuu: Madhumuni ya kushuka aya hii ilikuwa ni kujibu matusi yaliyokuwa yanatolewa na washirikina wa Makka dhidi ya Bwana Mtume SAW ambao walikuwa wanamwita "Abtar" yaani mtu aliyekatikiwa na kizazi. Lengo la aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu atakitia baraka kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW na kitabakia muda wote bila ya kuathiriwa na kupita siku na nyakati. Angalieni ni idadi kubwa kiasi gani ya watu wa kizazi cha Bwana Mtume wamewaua lakini hadi leo hii dunia imejaa watu wa kizazi hicho. Lakini pia angalia kizazi cha Bani Umayyah, licha ya idadi kubwa ya watu waliokuwa nao lakini hivi sasa hakuna mtu hata mmoja kati yao wa kuweza kuzingatiwa. Ila angalia kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW utapata kuna shakhsia, maulamaa na wanafikra wakubwa kama (Maimam) Baqir, Sadiq, Kadhim, Ridha na mithili yao." Mwisho wa kunukuu.
Ruwaza na kigezo chema cha malezi kutoka kwa Bibi Fatimatuz Zahra SA kwa wanadamu wote duniani kimezungumziwa na watu wa kila namna wawe ni Waislamu wa Kishia na Kisuni, Wakristo, wataalamu wa masuala ya Mashariki, wataalamu wa masuala ya Kiislamu na wengineo. Henry Corbin, mwanafikra wa Kifaransa ambaye ni miongoni mwa wanafalsafa wakubwa wa Magharibi amefanya uchunguzi wa kina kuhusu Bibi Fatimatuz Zahra SA. Amesema, Bibi Fatima ni kigezo cha ukamilifu wa kibinaadamu na maarifa ya Mwenyezi Mungu. Corbin anatoa ufafanuzi wa kina wa nadharia yake kuhusu binti huyo wa Bwana Mtume katika kitabu chake alichokipa jina la Ardhi ya Malakuti.
Naye Dk Ali Ibrahim Hasan mmoja wa wahadhiri wa historia wa Chuo Kikuu cha Cairo nchini Misri amesema kuhusu bibi huyo mtukufu katika Uislamu kwamba: Maisha ya Bibi Faatima ni ukurasa mtukufu na muhimu sana kati ya kurasa za historia. Ndani ya ukurasa huo kunaonekana sura mbalimbali kubwa, tukufu na adhimu. Bibi Faatima si sawa na Bilqis (Malkia maarufu wa Sheba) na wala Cleopatra (Malkia maarufu wa Misri) ambao nguvu na mvuto wao ulitokana na utawala mkubwa na mali nyingi na ujamali wa aina yake wa sura waliokuwa nao na ushujaa wa kudhibiti majeshi makubwa na kuyaongoza kwenye mapambano vitani bali Faatima ni shakhsia mkubwa zaidi ambaye ameweza kupanua nguvu zake katika kila kona ya dunia kwa hekima na utukufu wake ambao haukutokana na nguvu za utawala wala utajiri wa mali, bali ulitoka ndani ya moyo na kwenye kina kirefu cha fuadi...
Naye Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Wanawake wa Kiislamu wanapaswa kumfanya Bibi Faatimatuz Zahra kuwa kigezo chao kikuu katika maisha yao ya kawaida, maisha yao ya kijamii, maisha yao katika familia, na wastafidi vilivyo na hekima zake, busara zake, akili na maarifa yake. Vile vile wajifunze kutoka katika sifa zake za ucha Mungu, jihadi, kuweko katika medani mbalimbali na katika maamuzi mazito na muhimu ya kijamii, malezi ya watoto, maisha ya mume na mke na harakati za kijamii...
Hatimaye Bibi huyo mwema ambaye kwa mujibu wa hadithi sahihi ya Mtume Muhammad AS ni 'Mbora wa wanawake duniani' alikufa shahidi mwezi 3 Mfunguo Tisa Jamadi Thani kwa mujibu wa mapokezi ya baadhi ya wanahistoria akiwa na umri wa miaka 18 tu kwa mujibu wa nukuu mashuhuri zaidi. Aliswaliwa kwa siri na kundi dogo la waumini na kuzikwa usiku wa manane kwa mujibu wasia wake ambapo alitaka watu waliomdhulumu wasishuhudie jeneza na mazishi yake.
Wasikilizaji wapenzi muda uliotengewa makala hii umeisha kabisa. Kwa mara nyingine tunatoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kufa shahidi Bibi Faatimatuz Zahra SA Binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na tunamalizia kwa maneno ya hekima ya mtukufu huyo aliposema: Mtu yeyote anayefanya ibada kwa ikhlasi ya nia na kwa ajili tu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamlipa mja huyo malipo bora kabisa anayostahiki kulipwa na yenye maslahi zaidi kwake. (Rehema na Amani ziwe juu yako ewe kipenzi cha Bwana Mtume).
tamati