Ali AS, dhihirisho la dua na kumtaradhia Allah
(last modified Thu, 15 Jun 2017 13:39:39 GMT )
Jun 15, 2017 13:39 UTC
  • Ali AS, dhihirisho la dua na kumtaradhia Allah

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika makala hii maalumu inayokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib AS. Ni matumaini yangu kwamba mtaendelea kuwa kando ya redio zenu kusikiliza niliyokuandalieni.

Katika usiku ule ulioahidiwa, Amiri wa mema na matukufu, Ali bin Abi Twalib AS alikuwa akitoka nje ya nyumba mara kwa mara na kuangalia mbingu. Alionekana akifanya istighfari na kusoma Suratu Yasin. Usiku ule sala, dua na maombi ya Ali AS yalitofautiana na ya usiku nyingine na daima alikuwa akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Nibarikie mimi mauti."

 

Baadhi ya waumini walikuwa wamenza kuelekea msikitini kwa ajili ya sala ya asubuhi. Ali kama kawaida yake, alitoka haraka na kuelekea msikitini. Baada ya kuingia msikitini mjini Kufa, Iraq katika hali ya giza alisali rakaa kadhaa na kisha akapanda juu ya mnara wa msikiti na kuanza kutoa adhana. Allahu Akbar... Allahu Akbar

Muda mfupi baadaye Imam Ali AS alisimama kwa ajili ya sala ambayo ilitawaliwa na hali isiyokuwa ya kawaida. Hakika siku iliyoahidiwa ilikuwa imewadia. Ibn Mujlim, mwanadamu muovu zaidi kuliko wote, alikuwa amezama katika fikra za giza na upotovu. Alijongea kwa Imam aliyekuwa katika sala na kumpiga kichwani panga lililokuwa na sumu kali. Upanga huo wenye sumu ulizama katika kichwa cha Imam Ali hadi sehemu ya mbele ya kusujudia. Hakika upanga huo ulitayarisha mazingira ya kutenganisha umma na kiongozi wake kipenzi na kuwatia simanzi na majonzi yasiyokuwa na kifani waumini waliokuwa wakimzunguka kama nyuki watafutao asali.

Katika kipindi hicho ambapo Imam alikuwa amelala katika damu juu msala wa mahaba na kumpenda Mwenyezi Mungu, alionja ladha ya uhuru wa kuondoka katika dunia hii finyu na ya kupita na kuwasiliana na Mola Mlezi wake. Hakika alikuwa amevuka kipindi cha maumivu ya kimwili na kuona ahadi aliyokuwa amepewa na Bwana Mtume Muhammad SAW ikitimia. Aliinua kichwa mbinguni na kusema: "Ninaapa kwa jila la Mola wa al Kaaba kwamba hakika nimefuzu."

Marqad ya Imam Ali AS mjini Kufa, Iraq

 

Imepita miaka bali karne nyingi sasa ambapo wasomi, wanazuoni na wahakiki wamekuwa wakizungumza na kuandika mengi kuhusu shakhsia ya Imam Ali bin Abi Twalib AS. Vitabu vingi vya nathari na mashairi vimeandikwa katika kutaja wasifu wa mtukufu huyo ambaye ndiye wa kwanza kuzaliwa ndani ya nyumba tukufu ya al Kaaba. Ali bin Abi Twalib alikuwa mwanaume wa kwanza kukubali wito wa Nabii Muhammad na wa kwanza kumfuata Mtume katika sala ya jamaa. Tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi alikuwa akienda pamoja na Mtume SAW katika jangwa la kandokando ya Makka na kunong'ona na Mola Muumba, na mwenendo huo wa kumtaradhia na kumuomba Mwenyezi Mungu kwa siri aliuendeleza hadi alipopigwa upanga kichwani akiwa katika sala msikitini.

Mtume Mtukufu Muhammad SAW alifupisha sifa na matukufu ya Ali bin Abi Twalib katika sentensi fupi pale aliposema: "Ali amevutwa na kuzama katika upendo wa dhati ya Mwenyezi Mungu." Katika sehemu nyingine Mtume saw anasema: "Lau kama mbingu na ardhi zote vitawekwa katika upande mmoja wa mizani na imani ya Ali bin Abi Twalib ikawekwa katika upande wa pili, basi upande wa imani ya Ali utakuwa mzito zaidi."

Mwanahistoria na alimu mashuhuri wa madhehebu ya Suni Ibn Abil Hadid ameandika yafuatayo kuhusu ibada na dua za Ali bin Abi Twalib. Anasema: "Alikuwa akifanya ibada zaidi ya watu wote na kusali swala za usiku na kufunga saumu nyingi kuliko wengine. Aliwafunza watu kusali sala za usiku na jinsi ya kusali sala za suna.... Kipaji chake cha uso kiliota nundu kutokana na kusujudu sana." Ibnu Abil Hadid anaendelea kusema kuwa: "Unapotafakari katika dua na minong'ono yake na Mola Muumba na kuzama katika maana za kina zilizomo katika dua hizo kuhusu jinsi anavyomuadhimisha Mwenyezi Mungu na kunyeyekea mbele ya haiba yake, ndipo utakapoelewa kiwango cha ikhlasi ya mtukufu huyo. Hapa utapata kuelewa dua na maombi hayo yalikuwa yakitoka katika roho kubwa kiasi gani ..."

 

Maarifa na elimu kubwa ya Ali bin Abi Twalib kuhusu Mwenyezi Mungu SW ndio chanzo cha upendo na hisi yake ya kupigania uadilifu na haki. Aliitambua vyema nafsi yake na huu ulikuwa msingi wa maarifa aali yaani kumjua Mola Muumba na mkamilifu mutlaki. Ali AS alikuwa akisema: "Dunia na vilivyomo haiwezi kufikia nafasi aali ya mwanadamu, na hadhi ya mwanadamu iko juu kiasi kwamba haiwezi kuuzwa kwa thamani ya dunia, kwani dunia ni wenzo na chombo cha kutumia kwa ajili ya kufikia makazi halisi ya mwanadamu." Alikuwa akisema: "Sikuona kitu chochote ila nilimuona Mwenyezi Mungu kabla yake, baada yake na pamoja nacho."

Ni maarifa haya ya kina ndiyo siri ya dua na minong'ono ya Imam Ali AS na Mola wake Mlezi. Pamoja na hayo dua na ibada hizo za Imam hazikumzuia kufanya kazi na bidii ya kustawisha nchi, kupigana jihadi katika njia ya Allah, kupambana na dhulma na kupigania haki na uadilifu. Si hayo tu, bali Imam aliyatambua hayo kuwa ni ibada kubwa zaidi. Alimkumbuka Mwenyezi Mungu katika hali zote na hakughafilika na Mola wake hata lahadha moja. Katika moja ya hotuba zake ndani ya Nahjul Balagha, Imam Ali anataja sifa za wacha-Mungu ambaye yeye mwenyewe ni kinara wao akisema: Wameonja tamu ya maarifa ya Mwenyezi Mungu na kukata kiu yao kwa bilauri ya upendo na mahaba ya Mola wao, matokeo yake wamejielekeza katika twaa na uja kiasi kwamba migongo yao imepinda kutokana na wingi wa ibada.

Imepokelewa kwamba Imam Ali AS alijeruhiwa vitani kiasi kwamba mshale ulizama ndani ya mfupa wake na kusababisha maumivu makali. Waganga na matabibu walijitahidi kadiri ya uwezo kuondoa mshale huo katika mguu wa Imam lakini hawakuweza. Tabibu mmoja alisema mshale huu hauwezi kutoka bila ya kupasua nyama na eneo hili. Jamaa wa Imam na watu wa karibu yake walisema, kama hapana budi ya kupasua sehemu mshale huo ulipoingia, basi subirini hadi atakapoingia katika ibada ya sala na kunong'ona na Mola wake, wakati huo mtaweza kutoa mshale huo. Walisisitiza kwamba Imam Ali AS anapokuwa katika ibada ya sala hughiriki katika ibada na kuondoka kabisa katika dunia hii. Waganga na matabibu walisubiri hadi Imam alipoanza kuswali na kughiriki katika ibada, wakati huu ndipo walipoweza kuondoa mshale ule bila hata ya Imam mwenyewe kuhisi.

 

Wapenzi wasikilizaji tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi na wafuasi wa Ahlul Bait na Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume wetu Muhammad saw kwa mnasaba wa kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam wa Wachamungu Ali bin Abi Twalib AS. Wassalamu Alaukum Warahmatullah Wabarakatuh.

Tags