Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha (AS)
(last modified Sat, 18 Nov 2017 16:41:59 GMT )
Nov 18, 2017 16:41 UTC
  • Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha (AS)

Assalaam Alaykum. Tuko katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar, siku ambayo ni kumbukumbu ya kukumbuka siku ya kuuawa shahidi Imam Ali bin Mussa Ridha (as) mmoja kati ya watu wa Nyumba tukufu ya Mtume Mtukufu Muhammad (saw).

Imam Ali bin Mussa Ridha (as) ana lakabu nyingi, lakini iliyokuwa mashuhuri ni ile ya 'ar Ridha', yaani shakhsia huyo aliridhia matakwa ya Mwenyezi Mungu SW, marafiki zake walimridhia na maadui zake hawakueleza sababu za kutomridhia yeye. Imam Ali bin Mussa Ridha (as) alikuwa na lakabu nyingine yenye maana ya 'mgeni', ambapo shakhsia huyo alilazimishwa na Maamun mtawala wa Kiabbasi, aondoke katika ardhi ya mababu zake watoharifu huko Madina na kuelekea kwenye makao ya Maamun yaliyokuwa Khorassan Kuu na hatimaye kuuawa shahidi akiwa ugenini.

Maamun kwa kutumia hila na udanganyifu wake alimlazimisha Imam Ridha (as) akubali kuwa mrithi wa kiti cha utawala wake, ili aweze kuzuia hatari ya kutokea harakati na mwamko wa wafuasi wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) dhidi ya utawala wake usiokuwa wa kisheria, na hatimaye alitumia jina la Imam Ridha (as) kwa lengo la kuhalalisha utawala wake kwa wananchi. Lakini Imam Ridha (as) kwa weledi na umaizi mkubwa aliweza kuitumia fursa hiyo kwa lengo la kuhuisha dini tukufu ya Kiislamu na kuwaongoza Waislamu. Imam Ridha wakati alipoondoka Madina na kuelekea Khorassan, karibu watu wote wa Madina walikuwa wanajua jinsi alivyochukizwa na kutoiridhia safari hiyo. Imam Ali bin Mussa Ridha (as) aliianza safari yake kwa kulizuru kaburi la Mtume Mtukufu(saw) pamoja na makaburi mengine ya Watu wa

Haram ya Imam Ridha AS, Mash'had, Iran

 

Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) huku akitokwa machozi na kuomba dua, suala ambalo lilithibitisha kwamba safari yake hiyo ilikuwa ni safari yake ya kifo na kuwekwa wazi njama chafu za Maamun. Imam Ridha (as) hakukubali haraka kuchukua wadhifa wa kuwa mrithi wa kiti cha utawala wa Maamun hadi pale alipoona wazi maisha yake yamo hatarini, kwani watu wote walitambua jinsi Imam (as) alivyopinga kuchukua jukumu hilo ingawa alikubali kuchukua jukumu hilo baada ya kushinikizwa na kulazimishwa na Maamun kukubali kuchukua wadhifa huo. Msimamo huo wa Imam Ridha (as) wa kukubali kuwa mrithi wa kiti cha mtawala, hatuwezi kusema kwamba ulikuwa siyo sahihi. Msimamo huo wa kimantiki wa Imam Ridha (as) licha ya kuzima njama za Maamun, ulitoa fursa kwa Ahlul Bayt na wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume SAW kupata nguvu na ari, ambayo ilikuwa vigumu kupatikana hapo awali. Kwa vile Imam Ridha (as) alikuwa mrithi wa kiti cha utawala wa Maamun, wapenzi na maashiki wa Ahlul Bayt (as) walipata nguvu zaidi na hata kupungua mashinikizo yaliyokuwa yakiwakabili. Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) daima walikuwa wakiteswa, kusumbuliwa na kukabiliwa na vitisho na tawala wa kidhalimu, lakini kwa baraka za Imam Ridha (as) walikuwa wakipewa heshima na kutajwa kwa upendo na wale watu ambao walikuwa hawatambui fadhila za Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) walianza kuzitambua na maadui wakaanza kudhoofika na hatimaye kushindwa kabisa.Maamun alipanga hila na njama nyingine ya kuitisha mdahalo na kikao cha kielimu na kidini kwa lengo la kuidhofisha nafasi ya juu aliyokuwa nayo Imam Ridha (as).

Maamun aliamua kumualika kila mtu aliyemuona kwamba angelikuwa na uwezo wa kumshinda kielimu Imam Ridha (as) kwenye madahalo huo. Imam (as) aliweza kuwashinda shamkhsia mbalimbali walioalikwa kwenye vikao vya kielimu na midahalo ya kidini na madhehebu mbalimbali. Hapo ndipo Maamun alipohisi kufeli na kushindwa mbele ya Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na hivyo kufikiria kuchukua maamuzi na mbinu zilezile chafu zilizokuwa zikitumiwa na watawala madhalimu wa kabla yake, nayo ni kumuua shakhsia huyo mtukufu. Kwa utaratibu huo baada ya kupita mwaka mmoja na kitu, Maamun aliamua kutenda jinai kubwa na isiyoweza kusahaulika pale alipotoa amri ya kuuawa Imam Ridha (as). Maamun ambaye alimuua kaka yake mwenyewe na maelfu ya watu kwa ajili ya kuwa khalifa, vipi alitoa pendekezo kama hilo kwa mtu mkubwa na mtukufu kama Imam Ridha AS ambaye kauli yake ni hujja hadi leo hii, awe mrithi wa kiti chake na ampe uwanja wa kusikiwa na watu wengi zaidi? Ili kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo, ni vyema tukigusia malengo ya Khalifa Maamun ya kutoa pendekezo hilo kutoka katika maneno yake mwenyewe Maamun.Wakati Maamun alipotoa rasmi pendekezo kwamba Imam Ridha AS awe mrithi wa kiti chake, alilaumiwa mno na watu wengi wa Bani Abbas. Walimwambia, kwa nini unafanya kosa hili la kuutoa ukhalifa wenye fakhari kubwa mikononi mwa Bani Abbas na kuwapatia wana wa Ali? Hatua yako hii imewafanya watu wazidi kumjua Ali bin Musa Ridha na kujua ustahiki na utukufu wake, ukhalifa wako umeutia hatarini na umaarufu wako nao umeushusha chini.Maamun ambaye alikuwa mjanja sana kisiasa aliwajibu akiwaambia: Kuna mambo mengi yamenifanya nichukue hatua hii. Kwa kumuingiza kwangu (Imam Ridha as) ndani ya utawala wangu, kutamlazimisha autambue rasmi ukhalifa na utawala wetu. Aidha wafuasi na wapenzi wake watamchukia na kujitenga naye kwani wataamini kuwa yote aliyokuwa akiwaambia huko nyuma kuwa ukhalifa wetu si halali, hayakuwa ya kweli. Vile vile nimeogopa kwamba, kama nitamwachia vivi hivi Ali bin Musa bila ya kumdhibiti kwa kumuweka karibu yangu, atanisababishia matatizo kwani watu wengi watavutika kwake na mimi nitashindwa cha kufanya. Hivyo si busara hata kidogo kumdharau.

Msafara wa kwenda kumzuru Imam Ridha AS

 

Ni lazima tupunguze heshima na umaarufu wake pole pole na hatimaye tumtoe thamani kikamilifu mbele ya watu, wamuone kuwa hana ustahiki wowote wa kuwa khalifa. Hivyo sidhani kwamba kwa vile nimeshamteua Ali bin Musa kuwa mrithi wa kiti changu, kutakuwa na hatari zozote zitakazoukabili utawala wangu kutoka kwa kizazi cha Abu Talib.Imam Ridha AS alitambua vyema ujanja na hila hizo za Maamun na alijua kuwa amemlazimisha awe mrithi wa kiti chake ili kuimarisha utawala wake. Lakini pamoja na hayo, mtukufu huyo alikubali pendekezo hilo alilolazimishwa kulikubali na Maamun akielewa vyema kuwa jambo hilo halitadumu muda mrefu na Maamun hatovumilia kuona Imam Ridha as anafanya kazi zake inavyopasa. Aidha kwa ajili ya kuvunja njama za Maamun, wakati Imam Ridha as alipokuwa anaondoka Madina kuelekea kwenye makazi ya Maamun huko Marw, alizungumza na watu kwa namna ambayo wote walielewa kuwa Maamun alikusudia kumfukuza Imam Ridha as kutoka mjini kwake Madina kulikokuwa na wafuasi wake wengi na kumbaidisha mbali kabisa yaani Marw. Harakati zote zilizofanywa na Imam Ridha as wakati anazuru Haram ya Bwana Mtume Muhammad SAW kumuaga, na wakati alipokuwa anawaaga familia yake na wakati anaondoka Madina na hadi anafika Makkah na kutufu Alkaaba, zote ziliwathibitishia watu kuwa hiyo ilikuwa safari yake ya kwenda kuuawa shahidi ambapo kuteuliwa kuwa mrithi wa Khalifa Maamun ilikuwa ni kisingizio tu cha kumtoa Madina na kumbaidishia sehemu za mbali.Hali hiyo ya kulazimishwa na kutenzwa nguvu iliendelea katika hatua zote nyingine alizofanya na mara zote alikuwa akisema, mimi nimetishiwa kuuawa ndio maana nimekubali kuwa mrithi wa Khalifa. Aidha wakati alipopendekezewa jambo hilo alitoa masharti kwamba hayuko tayari kutoa amri kwa mtu yeyote yule, wala kuzuia kutendeka jambo lolote lile, wala asitoe fatwa na hukumu za kisheria kwa mtu yeyote yule na wala asimuuzulu wala kumteua mtu yeyote yule.

Hivyo ni jambo lililo wazi kuwa, ukitoa anwani ya kulazimishwa kukubali jina la mrithi wa Khalifa, Imam Ridha as hakushiriki kwa namna yoyote ile katika matendo yote ya utawala wa Khalifa Maamun. Yote hayo yalionesha kuwa alitenzwa nguvu kukubali pendekezo hilo, kwani mtu asiye na nafasi katika jambo lolote lile, hawezi kuwa mfuasi wa utawala husika. Khalifa Maamun naye alitambua vyema jambo hilo na alifanya kila ujanja kuhakikisha kuwa Imam Ridha AS anajihusisha na masuala ya utawala, lakini Imam alikataa. Kwa mfano kuna wakati Maamun alimtaka Imam Ridha AS awaandikie barua wapenzi wake ambao walikuwa wanaendesha mapambano na kuutia misukosuko utawala wa Maamun, waache kufanya hivyo, lakini Imam alimwambia: Mimi nilishurutisha kuwa sitojihusisha kabisa na masuala ya utawala na tangu nilipokubali anwani hii ya mrithi wa ukhalifa, hakuna faida yoyote niliyoipata.

Siku aliyouawa shahidi, Imam Ridha alisali kwa khushuu na unyenyekevu mkubwa sala yake ya asubuhi. Hali yake ilionyesha kana kwamba alikuwa anajua kuna tukio kubwa linataka kutokea. Nuru ya sura yake ilikuwa kubwa zaidi kuliko siku zote na machoni mwake mlibubujika mapenzi na mawimbi ya amani. Tahamaki, mjumbe wa Maamun akagonga mlango na kusema: "Khalifa Maamun anamwita kwake Abal Hasan yaani Imam Ridha'. Imam akafuatana na mjumbe huyo, Maamun alinyanyuka mahala pake na kumkaribisha Imam katika sehemu yake maalumu, Wawili hao wakasimama kuangaliana. Imam Ridha akahisi moto wa chuki uliotokana na jinsi alivyomuangalia na akaingiwa na wasiwasi wa siri ya moyo wake. Maamun alikuwa amekata tamaa kwamba licha ya kufanya njama nyingi, lakini ameshindwa kuwazuia watu wasimpende Imam Ridha na kumfuata kwa kila jambo. Aidha alikuwa anajuwa vyema kwamba Imam Ridha hakuwa mtu wa kuvumilia dhuluma na ukandamizaji na kwamba licha ya kuwa Maamun alikuwa Khalifa, lakini hakuwa na nafasi kama ya Imam Ridha ndani ya nyoyo za Waislamu.

Njiwa katika Haram ya Imam Ridha AS

 

Sasa akawa anajisemea mwenyewe chini kwa chini: 'Naam, njia bora kabisa ni kumuondoa katika uso wa dunia Abal Hassan'. Maamun alipiga hatua chache mbele na bila ya kuangalia akachukua vishada kadhaa vya zabibu kutoka kwenye chombo kikubwa na akaanza kubugia na kubwakia tembe zake. Baadaye akaenda mbele ya Imam akambusu kwenye kipaji cha uso na kumkaribisha ale zabibu akimwambia: "Yaa Ibna Rasulillah! Ewe mwana wa Mtume SAW sijawahi kuona zabibu tamu safi na za kuvutia kushinda hizi'. Imam akamjibu kwa majibu yake yasiyotetereka akisema: 'Lakini zabibu za peponi ni safi na za kuvutia zaidi'. Maamun akamwambia,'Karibu ule zabibu hizi tamu'. Lakini Imam alikataa. Hata hivyo Maamun akashikilia na kumlazimisha ale zabibu hizo zilizokuwa zimetiwa sumu kwa hali yoyote ile. Imam akatoa tabasabu chungu. Tahamaki rangi ya sura yake ilibadilika na hali yake ikawa mbaya. Kishada cha zabibu kikamuanguka mkononi na sasa hali ikazidi kuwa mbaya, akaanguka chini taabani. Aba Swilat, mmoja wa wafuasi wa karibu wa Imam Ridha alishtuka mno alipoona hali hiyo. Alikuwa amejaa furaha kwa kuwa karibu na mtukufu huyo na alikuwa akinufaika kwa kila sekunde na nuru ya mjukuuu huyo wa Bwana Mtume. Alikuwa amezama kwenye mawazo akikumbuka miongozo ya Imam Ridha as aliposema: 'Imam na kiongozi ni wawakilishi waaminifu duniani, ni hujja zake kwa waja Wake...Ni walinganiaji wa njia ya Allah na ni walinzi wa mipaka Yake Allah. Imam hutakaswa kuokana na aibu na madhambi. Hupambika kwa elimu na anasifika kwa ucha Mungu. Imam ni chimbuko la istikama ya kidini, heshima na fakhari kwa Waislamu...' Aba Swilat alikuwa amezama kwenye mawazo hayo, ghafla akamuona Imam Ridha akiwa katika hali ya kusikitisha. Hapo alifahamu kwamba Maamun ametekeleza hila na njama zake za mwisho na wakati ulikuwa umepita, kwani sumu ilikuwa imeshaenea mwilini. Muda haukupita Imam Ridha as akauawa shahidi. Siku hiyo ilikuwa mwishoni mwa Mfunguo Tano Safar mwaka 203 Hijria.Sasa tunawaleteeni moja kati ya hadithi za Imam Ridha (as) ambaye ameelezea mambo matano yanayoonyesha sifa njema za mja mwema wa Allah SW, ambayo ni taa na mwongozo kwetu sisi sote.

Imam Ridha (as) amesema kuwa, Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jambo jema hufurahia. Imepokelewa hadithi kwamba, mtu mmoja alimuendea Mtume Mtukufu (saw) na kusema: Mimi ninaficha elimu yangu, na sipendi mtu atambue hilo na kwa bahati imetambulikana nami nimefurahi kuona kwamba jambo hilo limejulikana kwa watu. Mtume (saw) akasema; Wewe una malipo mawili, malipo ya kuficha na malipo ya kudhihirisha'. Bila shaka, furaha hii kama ilikuwa kwa ajili ya kujionyesha tu itabatilisha matendo yako. Amma inawezekana mtu akafanya jambo jema bila ya hata ya watu kulitambua, lakini mtu huyo huingiwa na furaha kwa kupata radhi ya Mwenyezi Mungu. Basi furaha hiyo siyo ya kujionyesha, kiburi au kujiona, bali ni hali ya kimaanawi ambayo huipata mtu baada ya kutekeleza amali njema na kuwa karibu na Mwenyezi Mungu (SW). Sifa ya pili ya mja mwema wa Allah kwa mtazamo wa Imam Ridha (as) ni pale kila mtu anapotenda kosa huomba msamaha kutokana na makosa aliyotenda kwani ni nani anayetoa msamaha asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 135 ya Surat al Imraan: 'Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao, na nani anayefuta dhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu? Na wala hawaendelei na waliyoyafanya na hali wanajua'. Sifa ya tatu ya mja mwema wa Allah iliyoelezwa na Imam Ridha (as) ni ya mtu ambaye inapomfikia neema hushukuru. Kwa hakika, mja mwenye kushukuru ipasavyo, ni yule ambaye licha ya kumshukuru Muumba na muumbwa kwa kutumia ulimi wake, huwa na imani ndani ya moyo wake kwamba kila neema iliyoko katika ulimwengu huu, hutolewa na Mwenyezi Mungu na kumfikia mja kutokana na rehema zake.

Moja kati ya mambo ya kushukuru ni hili la kutumia neema za Mwenyezi Mungu kwa lengo la kupata radhi zake, kwa mfano viungo na mwili ambavyo ni neema ya Mwenyezi mungu, vitumike kwa ajili ya kutii na kutekeleza ibada za Mwenyezi Mungu na wala siyo kufanya mambo maovu. Sifa ya nne ya mja bora kwa mtazamo wa Imam Ridha (as) ni kusubiri wakati mja anapokumbana na mitihani na masaibu ya kidunia. Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 155 na 156 za Suratul Baqarah:'Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie waosubiri. Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea'. Amma sifa ya tano ya mja mwema kwa muono wa Imam Ridha (as) ni kusamehe wakati anapoghadhibika. Imam Jaafar Sadiq AS anasema: Hakuna mja yeyote anayezima ghadhabu zake, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu amemzidishia izza na utukufu wake duniani na akhera'.

Tags