Wairan waghariki katika kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Ridha AS
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i115990-wairan_waghariki_katika_kumbukizi_ya_kuuawa_shahidi_imam_ridha_as
Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tokea jana usiku wamezama katika maombolezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Ali Ridha (AS), mjukuu wa Mtume Mtukufu (SAW) miaka 1242 iliyopita.
(last modified 2024-09-04T03:32:12+00:00 )
Sep 04, 2024 03:32 UTC
  • Wairan waghariki katika kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Ridha AS

Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tokea jana usiku wamezama katika maombolezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Ali Ridha (AS), mjukuu wa Mtume Mtukufu (SAW) miaka 1242 iliyopita.

Barabara zote zinazoelekea katika Haram ya Imam Ridha (AS), Imam wa nane wa Waislamu wa Kishia, katika mji mtakatifu alikozikwa wa Mash'had, kaskazini mashariki mwa nchi, zimejaa umati wa waombolezaji waliovalia mavazi meusi na waliofika huko kutoka pembe zote za nchi na maeneo mengine ya dunia kwa ajili ya kuomboleza kifo cha mtukufu huyo wa Nyumba ya Mtume (SAW).

Katika usiku wa kuamkia leo, wananchi Waislamu wa Iran walikusanyika Misikitini na katika maeneo mengine ya ibada na marasimu ya kidini, na hasa katika kaburi lake huko Mash'had, kwa madhumini ya kutoa heshima zao na kumuomboleza mtukufu huyo, mjukuu wa Mtume (SAW).

Imam Ridha (AS) alizaliwa katika mji wa Madina nchini Saudi Arabia mwaka 148 Hijiria na kuuawa shahidi katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar mwaka 203 Hijiria.

Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash'had

Imam Ridha (AS) aliishi katika kipindi ambacho watu walikuwa na hamu kubwa ya kuwajua Watu wa Nyumba ya Mtume na kizazi chake kitoharifu (AS) na kuimarika nafasi yao miongoni mwa watu.

Kwa kuhisi hatari kutokana na mapenzi na uungaji mkono huo mkubwa wa watu kwa Ahlul Bait wa Mtume (SAW) Ma'mun, mtawala wa Bani Abbas katika kipindi hicho, alipanga njama ya kumpa sumu na kumuua Imam (AS).