Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra SA
(last modified Tue, 29 Mar 2016 17:15:58 GMT )
Mar 29, 2016 17:15 UTC
  • Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra SA

Tarehe 20 Jamadu Thani Hijiria imepambwa kwa uzawa wa Bibi Fatimat az-Zahra (sa) Binti ya Mtume Mtukufu (saw). Uzawa wa mtukufu huyo lilikuwa tukio muhimu lililotokea katika miaka ya ujumbe wa Mtume (saw).

Miaka mitano baada ya kubaathiwa Mtume Mtukufu (saw) na katika siku kama ya leo, nyumba ya Mtume ilijaa manukato na uturi wa Peponi. Katika siku hiyo Bibi Fatima (sa) alizaliwa na hivyo kujaza nyoyo za Muhammad (saw) pamoja na mkewe mpendwa Khadija (sa) kwa furaha na bashasha. Uzawa huo ilikuwa zawadi kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume (saw) na mkewe wake Khadija (sa). Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hiyo yenye thamani kubwa, Mtume alimkumbatia Fatima, kumbusu kwenye paji la uso na kisha kumtazama usoni. Uso huo uliokuwa umejaa nuru ulimtuliza Mtume (saw). Kwa kuzaliwa Fatima, ni kana kwamba Mtume alikuwa amepewa hazina ya dunia na kwa hakika kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, Fatima (sa) alikuwa 'Kauthar', yaani kheri nyingi kwa Mtume (saw), kama inavyosema Qura'ni yenyewe katika Surat al-Kauthar: Hakika tumekupa kheri nyingi. Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako. Hakika anayekubughudhi ndiye aliyekatikiwa.

Aya hizi ziliwajibu wale maadui waliokuwa wakimbughudhi Mtume (saw) kwa kunkejeli na kumwambia kuwa alikuwa amekatikiwa na kizazi. Kwa hakika aya hizo zilimtuliza Mtume, kumpa matumaini na kumhakikishia kwamba ukweli wa mambo ulikuwa kinyume kabisa na walivyokuwa wakidai maadui wake. Bibi Fatima alizaliwa ili kuwa kigezo na fahari ya wanawake duniani na wakati huohuo kuwa mama na chanzo cha kizazi cha wabeba bendera wongofu kwa ajili ya kutetea dini ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na vigezo vya maadili mema na utu. Mtume Mtukufu alimpa jina la Fatima kwa maana kuwa Mwenyezi Mungu alimuweka mbali na maovu pamoja na moto. Salamu ziwe kwa Fatima (sa)! Mbora wa wanawake wa ulimwengu. Salamu ziwe kwa mtu aliyependwa zaidi na Mtume (sa)! Salamu kwa kheri na rehema nyingi! Salamu kwa Fatima (sa) ambaye ni mfano halisi wa mtu bora na aliyekamilika. Tunatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa wapenda na watetezi wote wa haki duniani kwa mnasaba wa kuwadia siku hii adhimu ya kuadhimishwa uzawa wa Bibi Fatima (sa).

**********

Licha ya kuwa Bibi Fatima (sa) aliishi kwa muda mfupi sana na mama yake mzazi Bibi Khadija (sa), lakini alisikia visa vingi vya kuvutia kuhusu mapambano katika njia ya Mwenyezi Mungu kutoka kwa mama yake huyo. Alipokuwa akiutazama uso wa mama yake, ni kana kwamba alikuwa akisoma ukurasa mpya wa mapambano hayo ambayo yalikuwa yakiendelea hadi katika zama hizo za uhai wa Bibi Fatima (sa). Fatima (sa) alijifunza masuala muhimu ya maisha kutoka kwa baba yake, Mtume Mtukufu (saw) na alikuwa na nafasi muhimu kwake. Mapenzi na upendo aliouonyesha Mtume kwa binti yake huyo yalikuwa makubwa zaidi kuliko mapenzi ya kawaida yanayoonyeshwa na mzazi kwa mtoto wake na hilo lilionyesha wazi nafasi, ukamilifu na utukufu aliokuwa nao Fatima (sa). Mtume alikuwa akimpenda sana binti yake huyo na akisema: "Binti yangu mpendwa Fatima, ni fahari ya wanawake wa dunia katika zama na vizazi vyote."

Bibi Fatimat az-Zahra alizaliwa katika jamii ambayo ilikuwa tupu katika mtazamo wa thamani za kiutu. Tabia na tamaduni potovu kama vile vita, umwagaji damu na kuwazika hai mabinti ambao hawakuwa na hatia yoyote zilikuwa zimefikia kilele katika zama hizo. Kwa kudhihiri Uislamu, Mtume alipambana vikali na mila hizo za kuchukiza. Katika zama ambazo akina baba walikuwa wakichukizwa na kuhuzunishwa sana na kubarikiwa watoto wa kike, Mtume alikuwa akiibusu mikono ya Fatima ili kukabiliana na fikra mbovu za kijahili zilizokuwa zimeenea katika zama hizo dhidi ya watoto wa kike.

Fatima az-Zahra alizaliwa katika nyumba ya Wahyi na mtu adhimu katika historia ya mwanadamu, ambaye hakuwa mwingine bali ni Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu na hapo akapata maarifa na elimu muhimu kuhusiana na Mola Muumba wa mbingu na ardhi. Kila mara Wahyi ulipokuwa ukimteremkia Mtume naye kuamrishwa kuwabainishia watu hakika na mambo mapya, Fatima (sa) alikuwa akijifunza mengi kutokana na hotuba hizo za Mtume (saw) zilizojaa hekima na busara kuhusiana na ulimwengu. Kwa kuwa na maarifa kama hayo Bibi Fatima (sa) aliweza kupitia njia ya ukamilifu na kufikia maarifa muhimu ya Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi pamoja na mambo mengine yote yaliyo mazuri. Akiwa katika kilele cha ibada na ucha-Mungu Fatima (sa) anasema: "Ninashuhudia kwamba Mungu wa ulimwengu ni mmoja tu na hakuna mungu mwingine asiyekuwa Yeye." Bibi Fatima alikuwa na mapenzi makubwa kwa Mwenyezi Mungu kiasi kwamba hakuwa akifikiria jambo jingine isipokuwa kumridhisha Yeye tu. Mtume anathibitisha jambo hilo kwa kumwambia mmoja wa masahaba zake wa karibu: "Ewe Salman! Mwenyezi Mungu ameujaza moyo na uwepo wote wa Fatima kwa imani kiasi kwamba hafikirii wala kufanya jambo lolote isipokuwa kuabudu na kumtii Yeye tu."

Akiwa na mtazamo huo, Bibi Fatima alishiriki vilivyo katika medani za familia na jamii na kuwa mfano bora wa kuigwa na wote katika masuala ya mke na mama mzazi na hivyo kudhihiri kuwa mfano halisi wa mwanamke wa Kiislamu katika jamii. Fatima (as) aliyekuwa na huruma kubwa, daima alikuwa chanzo cha uchangamfu na utulivu kwa mumewe Ali (as). Alikuwa akiichukulia familia kuwa chimbuko halisi la jamii na msingi muhumu uliopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu. Aliyahesabu mazingira ya nyumbani na familia kuwa sehemu ya kutekelezwa malezi bora. Nyumba yake ndogo iliwalea watu wakubwa ambao walikuwa chanzo cha matukio muhimu katika historia ya Kiislamu na ya wanadamu wote. Katika mbinu yake ya malezi, Fatima (sa) ambaye yeye mwenyewe alikuwa chemchemi ya elimu na imani alipanda mbegu ya upendo, tabia njema na maadili mengine mema katika nyoyo za watoto wake. Mfano mmoja bora wa malezi hayo muhimu maishani ni kuwa wakati mmoja Imam Ali na Fatima (as) walifunga kwa siku tatu mfululizo na kuwapa masikini, fakiri na mfungwa chakula chao cha futari na kuamua kufuturu kwa maji pekee katika siku hizo za funga ya nadhiri. Jambo hilo lilipelekea na kuwashajiisha watoto wao kufuata tabia na mkondo huo wa kuvutia maishani ambapo walijitolea na kujinyima mambo mengi kwa ajili ya kutetea na kuhuisha haki na thamani tukufu za mbinguni. Nyumba ya Fatima ilikuwa nyumba ambayo wakazi wake walifikiria tu jinsi ya kumridhisha Mwenyezi Mungu na kuichukulia ridhaa hiyo kuwa msingi wa matendo yao.

Kwa mtazamo wa Bibi Fatima (sa), mwanamke kushughulikia masuala ya nyumbani na familia hakuna maana ya kumzuia kujishughulisha na masuala mengine ya kijamii, lakini anapasa kutahadhari suala hilo lisije likamfanya asahau utambulisho wake na kuanza kujifananisha na wanaume kwa njia isiyofaa. Fatima (sa) anawafundisha wanawake kwamba ubora wa wanawake haupatikani katika kujifananisha kusikofaa na wanaume bali ni kutekeleza ipaswavyo majukumu yao ambayo wameainishiwa na Mwenyezi Mungu, ambayo kwa hakika wanaume hawana uwezo wa kuyatekeleza. Kwa mtazamo huo Bibi Fatima (sa) aliyapa kipaumbele majukumu yake ya kuwa mke na mama na wakati huohuo kujishughulisha pia na masuala ya kijamii na kisiasa. Historia inashuhudia kuwepo kwa bibi huyu mtukufu katika medani mbalimbali na muhimu za Uislamu. Uwepo muhimu wa mtukufu huyo katika matukio tofauti tokea hijra hatari ya Mtume (saw) kutoka Makka hadi Madina, kuchangia masuala ya kusaidia na kuwapa moyo wapiganaji wa Kiislamu katika medani za vita na vilevile katika matukio ya baada ya kuaga dunia Mtume, yote hayo yanathibitisha wazi mchango mkubwa alioutoa bibi huyo katika nyanja za kijamii na kisiasa. Bibi Fatima (sa) alikabiliana na kupinga vikali watu waliokuwa na nia mbaya ya kutaka kuharibu na kukanyaga thamani za Kiislamu. Hakuwa akihubiri thamani za Kiislamu kwa maneno tu bali alikuwa akizitekeleza kivitendo na kupambana vilivyo na wale wote waliojaribu kuzikanyaga.

Mtazamo wa kina wa Fatima kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa katika zama zake ulitokana na mafundisho aali ya Qur'ani Tukufu ambayo yalimshajiisha kusimama na kupambana na dhulma, uonevu, ufisadi na ubaguzi katika jamii. Alikuwa akizingatia na kutekeleza kivitendo thamani za kiakhlaki na kimaanawi. Kwa mtazamo wa Fatima (sa), uzingatiaji wa Qur'ani unatimia katika kufahamu na kutekeleza mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu. Alikuwa akisema: 'Ikiwa mtu ataifuata Qur'ani, bila shaka atafikia saada na wokovu.' Ni kutokana na dalili hiyo ndipo, baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw), na ili kuzuia kutokea mfarakano na mgawanyiko miongoni mwa Waislamu, Bibi Fatima akawakumbusha watu nafasi muhimu ya Qur'ani kwa kuwaambia: "Ni kwa nini mnapotea njia hali ya kuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu kiko miongoni mwenu? Mafundisho yake yako wazi na hukumu zake kung'ara. Alama zake za uongozaji ziko wazi na tahadhari zake kubainika. Je, mnavutiwa na Qur'ani ilihali mnatafuta muamuzi asiyekuwa Qur'ani?" Mbali na kuienzi Qur'ani kwa maneno, Bibi Fatima pia alikuwa mtekelezaji mkubwa wa mafundisho aali ya kitabu hicho kitakatifu cha Mwenyezi Mungu.

Siku ya kuzaliwa Bibi Fatimat az-Zahra (sa) huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Mwanamke na Mama.Tunatumai kwamba wanawake na akina mama Waislamu duniani watafanya juhudi za kuufahamu vyema Uislamu na kuiga mifano ya wanawake wema kama Fatima (sa) katika kufikia nafasi yao halisi katika familia na jamii na hivyo kuishi katika mazingira bora wanayostahiki.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi Fatimat az-Zahra (sa) binti ya Mtume Mtukufu (saw). Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags