Aprili Mosi, Siku ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
(last modified Wed, 30 Mar 2016 15:24:39 GMT )
Mar 30, 2016 15:24 UTC
  • Aprili Mosi, Siku ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Leo tumeamua kukuandalieni makala fupi kuzungumzia tukio la mwaka 1979 la wananchi wa Iran la kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kujiamulia wenyewe mfumo wanaoutaka wa utawala, ambapo kwa kauli moja waliamua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu yaani mfumo unaotegemea maoni ya wananchi lakini kwa misingi ya dini tukufu ya Kiislamu, uwaongoze.

 Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Leo tumeamua kukuandalieni makala fupi kuzungumzia tukio la mwaka 1979 la wananchi wa Iran la kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kujiamulia wenyewe mfumo wanaoutaka wa utawala, ambapo kwa kauli moja waliamua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu yaani mfumo unaotegemea maoni ya wananchi lakini kwa misingi ya dini tukufu ya Kiislamu, uwaongoze.  

*******

Tarehe 12 Farvardin 1358 Hirjia Shamsia iliyosadifiana na tarehe Mosi Aprili 1979 wananchi wa Iran walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua mfumo wanaoutaka, na kwa kauli moja walichagua Jamhuri ya Kiislamu kuwa mfumo wa utawala wao wa kidemokrasia uliojengeka juu ya mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Kura ya maoni ya tarehe mosi Aprili ilikuwa na umuhimu katika pande mbili. Kwanza ni kuwa katika siku hiyo wananchi wa Iran walichagua kwa wingi mutlaki wa kura mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu uliochukua nafasi ya utawala wa kidikteta wa kifalme. Pili ni kuwa kura hiyo ya maoni iliweka misingi imara ya moja kati ya thamani za kajamii katika upande wa kisiasa yaani haki ya wananchi ya kuchagua na kujiamulia mambo yao kupitia masanduku ya kura.

Kura hiyo ya maoni ilifanyika katika kipindi cha chini ya miezi miwili baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mhandisi wa Jamhuri ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi alitilia mkazo udharura wa wananchi kushiriki kwa wingi katika medani mbalimbali za kuamua mustakbali wan chi yao na alikuwa akisema kuwa wananchi ambao ndio wamiliki halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanapaswa kushiriki katika medani mbalimbali ikiwemo medani hiyo ya kuainisha mustakbali wa nchi yao wenyewe.

Kwa utaratibu huo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini kwa mara ya kwanza kabisa kulianzishwa utawala wa kisiasa kwa mujibu wa kura za wananchi ambao sifa yake kuu ni kuoanisha pamoja utawala wa Mwenyezi Mungu na matakwa ya wananchi.

Kabla ya kufanyika kura ya maoni ya tarehe Mosi Aprili, Imam Khomeini alitoa ujumbe maalumu akieleza nukta mbili muhimu ambazo ni udharura wa wananchi wote kushiriki kwenye kura hiyo na kuwa huru katika kuchagua mfumo wanaoutaka wa kisiasa. Imam alisema katika ujumbe huo kwamba: "Kura hii ya maoni itaainisha hatima ya taifa letu na itawapa uhuru na uwezo wa kujitawala wananchi au kama ilivyokuwa hapo awali, itawatumbukiza tena katika ukandamizaji na kuwa tegemezi kwa mataifa mengine. Wananchi wote wanapaswa kushiriki katika zoezi hili na mnaweza kuchagua mfumo wowote mnaoutaka. Mna haki ya kuchagua jamhuri ya kidemokrasia, utawala wa kifalme au utawala wowote mwingine. Mnao uhuru na khiari ya kuchagua..."

*******

Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo imesisitiza juu ya haki ya wananchi ya kupiga kura, kushiriki katika chaguzi na utawala wa wananchi na mamlaka yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe, inatilia mkazo nafasi maalumu ya uchaguzi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na umuhimu huo unatokana na kuthaminiwa sana kura na mitazamo ya wananchi. Kifungu cha kwanza cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinasema kuwa serikali ya Iran ni ya Jamhuri ya Kiislamu kwa maana kwamba muundo wa serikali utakuwa wa "jamhuri" yaani maoni ya wananchi na mhimili wake ni wa "Kiislamu"; kwa maana ya kwamba maoni hayo ya wananchi yasiende kinyume na mafundisho ya Uislamu. Kwa msingi huo uhalali wake unatokana na misingi miwili ambayo ni dini na kura za wananchi. Kwa maneno mengine ni kuwa, uchaguzi ndiyo njia ya kudhihirisha demokrasia na kwa hapa Iran demokrasia hiyo imedhihiri kwa sura yake kamili zaidi kupitia uchaguzi.

Hapana shaka kuwa ili wananchi waweze kushiriki kwa wingi katika nyuga za kisiasa hapana budi kushirikishwa wananchi hao katika masuala ya kijamii sambamba na yale ya kisiasa. Kadiri wananchi watakavyoshirikishwa kwenye masuala hayo ndipo watakapozidi kuwa na welewa kuhusu mfumo wao wa utawala na kuzidi kuimarika utawala wa Jamhuri ya Kiislamu.

Wana nadharia wa masuala ya kisiasa na kijamii wanaamini kuwa, kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi kwa hamu na shauku kubwa bila ya kutenzwa nguvu, ni kielelezo cha kukubalika mfumo unaotawala. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kura ya maoni ya kuchagua mfumo tawala hapa nchini, kulitokea mabadiliko yaliyokuwa na taathira kubwa katika miaka ya baadaye ya Iran ya Kiislamu. Miongoni mwa matunda ya mabadiliko hayo ni ustawi wa kisiasa wa jamii uliopatikana kupitia njia ya wananchi kujiamulia mambo ya nchi yao wao wenyewe.

Katika kipindi chote cha miaka 37 iliyopita tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, karibu kila mwaka kumekuwa kukifanyika uchaguzi hapa nchini, suala ambalo limeimarisha misingi ya demokrasia, uwezo wa wananchi na kiwango cha kushiriki kwao katika maamuzi muhimu ya nchi yao. Kiwango cha ushiriki wa wananchi katika zoezi la uchaguzi pia kimekuwa na taathira kubwa katika masuala ya kijamii na kiuchumi ya ndani ya nchi na katika kuimarisha umoja ambao ni nguzo muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu katika medani za ndani na kimataifa.

Wakati huo huo taifa la Iran limelifanya suala la kushiriki kwa wingi katika chaguzi na kwenye medani mbalimbali kuwa ni fursa nzuri ya kuimarisha umoja wa kitaifa, kidini, kiutamaduni na kikaumu na wenzo wa ustawi na maendeleo ya kisiasa katika masuala ya demokrasia. Kura ya maoni ya tarehe tarehe Mosi Aprili 1979 iliyofanyika miezi miwili tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni kielelezo cha ukweli huo. Kwani licha ya kwamba wananchi walishasisitiza kwamba wanataka utawala uliosimama juu ya misingi ya thamani na sheria za Kiislamu na pamoja na kuwa hapakuwa na haja tena ya kuitisha kura kama hiyo ya maoni kwani tayari wananchi walishaonesha msimamo wao, lakini Imam Khomeini alisisitiza kuwa wananchi wapewe nafasi ya kuthibitisha uhakika huo kivitendo ili kuwaonesha walimwengu kuwa mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu unatokana na irada, matakwa na rai za moja kwa moja za taifa zima la Iran.

Katika kura hiyo ya maoni ya kuainisha aina ya mfumo wa utawala na serikali baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu asilimia 98.2 ya wananchi wa Iran walichagua mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ambao ni sehemu moja ya kaulimbiu tatu kuu za wananchi yaani "kujitawala", "uhuru" na "Jamhuri ya Kiislamu." Kuanzishwa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran kulikuwa na taathira kubwa na za muda mrefu kieneo na kimataifa. Athari hizo zinaonekana vizuri zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima kiujumla ikiwa ni pamoja na mwamko wa Kiislamu uliojitokeza katika pembe mbalimbali duniani.

Kiujumla ni kuwa, kura ya maoni ya kuanisha aina ya mfumo wa utawala nchini Iran katika kipindi hicho nyeti ambapo kulikuwa na uwezekano wa kufanyika njama za aina mbalimbali dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ndiyo kwanza yalikuwa yamepa ushindi, ilionesha ufahamu mkubwa wa masuala ya kisiasa wa wananchi wa Iran katika kujiamulia wenyewe mustakbali wa nchi yao kwa kutegemea thamani aali za mafundisho ya Uislamu.

*******

Mpenzi msikilizaji, hii leo pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imepata ushawishi mkubwa katika medani za kieneo la kimataifa, imekuwa kigezo bora cha kuigwa cha mfumo wa utawala wa kidemokrasia chini ya kivuli cha thamani na mafundisho ya dini na moja ya sababu kuu za jambo hilo ni bahati waliyopata wananchi wa Iran ya kuwa na kiongozi mwanachuoni wa dini anayeangalia na kuona mbali, Imam Khomeini MA. Si vibaya hapa mpenzi msikilizaji tukamalizia makala hii kwa kutupia jicho nafasi ya uongozi katika kuimarika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akizungumzia nafasi ya uongozi wa muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomein MA, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema: "Katika kipindi ambacho viongozi wa kisiasa walikuwa wakijishughulisha na njama za kuitenga na kuiweka pembeni dini, umaanawi na matukufu yote ya kiakhlaqi katika maisha ya kila siku ya mwanadamu, Imam Khomein MA alifanikiwa kuleta utawala ambao umejengeka juu ya misingi ya dini, umaanawi na matukufu ya kimaadili na kuasisi dola la Kiislamu nchini Iran."

Naam, uhakika wa mambo ni kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwani nafasi ya Imam Khomein MA katika Mapinduzi ya Kiislamu ya nchni Iran na kuimarika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hadi leo hii, ni dhihirisho la uongozi wake bora. Imam Khomein alianza kuweka misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu tangu katika shule za kidini. Wakati alipokuwa anatoa darsa, Imam Khomeini alikuwa akibainisha nafasi muhimu ya Uislamu katika kuongoza jamii. Hotuba za kuvutia za Imam Khomein ambazo zilikuwa zikisambazwa kupitia mikanda ya sauti au matangazo yaliyokuwa yakitolewa misikitini na kwenye Husseiniya, ziliimarisha uhusino kati ya kiongozi huyo na wananchi.

Kwa kweli harakati hizo ambazo hazikuwa na mfano kwa kuzingatia kiwango cha taathira zake, zilizaa matunda mazuri baada ya kupita karibu miaka 14 ambapo mwaka 1978 wananchi wa Iran walianza kubeba picha za Imam Khomein MA na mabango yaliyokuwa yameandikwa maneno yake na kuandamana katika miji kadhaa ya Iran na hatimaye kufanikiwa kuuangusha utawala wa kiimla wa kibaraka mkubwa wa Magharibi, Shah na kuasisi mfumo imara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo yalisimamia hadi kupata ushindi chini ya uongozi imara na uliojaa busara wa Imam Khomein MA, ni mapinduzi ya kweli na yaliyokamilika kila upande, kwa kuwa yalikusanya mambo yote ya lazima na ya dharura yanayohitajika katika mapinduzi yoyote yale.

Tunamalizia makala hii kwa kukunukulieni maneno ya mwanafikra mkubwa wa Kiiran Shahid Mutahhari ambaye amesema: "Niliona mambo matatu muhimu mno katika shakhsia ya Imam Khomein MA ambayo bila ya shaka yaliimarisha imani yangu. 1- Kuamini malengo, yaani kuwa imara katika kushikamana na malengo yake hata kama dunia nzima itasimama dhidi yake. 2- Kuamini nguvu za wananchi, na 3- ambalo ni muhimu zaidi ni kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila jambo."

Mpenzi msikilizaji, muda wa makala hii iliyozungumzia Aprili Mosi, Siku ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo ndani yake tumezungumzia mambo mengine ikiwemo nafasi ya uongozi katika kufanikisha na kuyadumisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, umeisha kwa leo. Tunakutakieni kila la kheri maishani.



Tags