Imam Baqir AS Chimbuko la Elimu na Maarifa
Mwaka 57 baada ya hijra ya Mtume SAW kuelekea Madina, katika siku ya kwanza ya mwezi uliojaa fadhila wa Rajab, ulimwengu ulipambazuka kwa kuzaliwa nuru. Katika siku hii yenye baraka, Mtoto kutoka Nyumba ya Mtume Muhammad SAW alizaliwa na sawa na Ahlul Bayt wengine wa Mtume SAW, akawa tawi katika matawi maridadi katika historia ya Uislamu. Yeye ni mwana wa Imam Sajjad AS na ni maarufu kwa jina la Baqir.
Jina la Baqir linamaanisjwa mwenye kunawirisha. Mtukuku huyo alitajwa kuwa mtu aliyechanua na kunawirisha elimu. Alikuwa stadi katika elimu mbali mbali na alitajwa kuwa bahari ya elimu. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za pongezi kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Baqir AS.
@@@
Baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Sajjad AS, Imam Baqir AS alichukua jukumu muhimu la uongozi wa Ummah wa Kiislamu kwa muda wa miaka 19. Kipindi hicho kiliambatana na matukio ya kisiasa na kubadlishwa utawala kutoka ukoo wa Bani Umayya hadi ukoo wa Bani Abbas. Katika kipindi hicho, Imam alitumia nafasi yake ili kueneza ukweli kuhusu elimu na utamaduni wa Kiislamu. Imam Baqir AS alianzisha harakati ya kiutamaduni na kisayansi katika ulimwengu wa Kiislamu na natija ya juhudi zake ilionekana katika duru zilizofuatata. Imam Baqir alijitahidi zana katika masuala ya elimu na utamaduni ili aweza kukabiliana kikamilifu na imani batili na potofu katika jamii. Aidha alikusudua kueneza fikra tukufu na a'ali ya Bwana Mtume na Watu wa Nyumba yake kupitia kuanzisha chuo kikubwa cha elimu na utamaduni.
Sheikh Tousi, mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu amewataja wanafunzi bingwa wa Imam Baqir AS kuwa ni watu 462. Vigogo na shakhsia wakubwa wa kisiasa wa zama hizo wote walifika mbele ya Imam Baqir AS ili kupata angalau tone moja la bahari yake pana ya elimu. Watu kama vile Jabir bin Yazid Jofi, Zohri , Abu Hanifa, Anas ibn Malik na Shafi ni kati ya wanazuoni walionufaika na hazina kubwa ya kielimu ya Imam Baqir AS. Muhammad Ibn Talha Shafi'i katika kuelezea sifa za Imam Baqir anaandika: "Alikuwa mwenye kunawirisha elimu. Hotuba zake zilikuwa fupi lakini zilijzojaa maana na moyo wake ulijaa mwanga. Alikuwa ni mwenye amali njema na zilizopambwa. Alikuwa na akhlaqi njema na alitumia umri wake katika kutii amri za Mwenyezi Mungu. Alikuwa amejikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na alistahiki uongozi."
Uimamu wa Imam Mohammad Baqir AS ulianza katika kipindi ambacho, Ummah wa Kiislamu ulikuwa unakabiliwa na changamoto za kina za kiitikadi na kifiqhi baina ya makundi mbali mbali ya Kiislamu. Kuwepo Imam Baqir AS katika medani kulipelekea kuchukuliwa hatua muafaka katika kubainisha mitazamo ya Ahlul Bayt wa Mtume SAW.
Katika kipindi cha muda mfupi, Imam aliweza kusambaratisha kwa kiasi kikubwa itikadi za makundi potofu. Katika zama za Uimamu wake na mwanawe mwenye adhama Imam Sadeq AS, hitilafu na mivutano katika utawala wa kisiasa zilifika kileleni na hali ya kisiasa na kijamii kukumbwa na ukosefu wa uthabiti. Natija yake ilikuwa ni kuwa Makhalifa walikuwa wakibadilishwa kwa kasi kiasi kwamba katika kipindi cha Uimamu wa Imam Baqir AS, makhalifa watano walitawala. Kwa hivyo Imam alipata fursa isiyo na kifani kwani alijiweka mbali na mashinikizo ya kisiasa ya watawala na kuwavuta karibu naye wanazuoni wakubwa pamoja na wasomi bingwa wa sayansi na hekima. Wanazuoni waliokuwa karibu na Imam waliweza kunufaika kwa njia ya moja kwa moja na mafundisho yake ya Kiislamu aliyokuwa akiyabainisha kwa lugha fasaha.
Katika kipindi cha Imam Baqir AS, hujuma ya kiutamaduni iliyokuwa imeratibiwa na Bani Umayyah ililenga kuvuruga itikadi za kidini za Ummah wa Kiislamu. Aidha katika kipindi hicho jamii ya Kiislamu ilishuhudia kuibuka nadharia zisizo sahihi za kifalsafa kuhusu misingi ya itikadi. Ni kwa sababu hii ndio baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu wakachanganyikiwa katika jitihada zao za kuutafuta ukweli. Imam Baqir AS kwa kutegemea dalili za kimantiki na zenye kupambanua alichambua fikra hizo potofu za kifalsafa na kuweza kubainisha nukta pofotu katika nadharia hizo mpya. Mtukufu huyo aliwatia kiti moto wanafalsafa wasiokuwa wa kidini na kuweza kubainisha mitazamo ya itikadi sahihi za Kiislamu. Kutokana na mazingira hayo, sayansi za kalam au misingi ya itikadi ziliweza kuvuma katika zama za Imam Baqir AS.
@@@
Imam Baqir AS alikuwa miongoni mwa watu na daima aliandamana nao. Pamoja na shani na adhama yote aliyokuwa nayo, mtukufu huyo alikuwa akiwahudumia watu wa tabaka dhaifu na waliotengwa katika jamii. Alikuwa akiketi na watu waliosahaulika kabisa, kuzungumza nao na kutatua matatizo yao. Muamala uliojaa ukarimu na unyenyekevu wa mtukufu huyo uliwapelekea watu wengi kumfuata. Imam Baqir AS hakumuacha bila jibu kila aliyekuja kwake kuomba msaada na aliwasisitizia wengine kuhusu umuhimu wa kuwasaidia na kuwaheshimu wahitaji. Kutokana na muamala wake mwema ulioambatana na adabu na mapenzi, Imam Baqir AS aliweza kuwavutia hata wapinzani wake. Katika historia tunasoma kuwa mtu mmoja kutoka Sham ambaye hakuafikiana kiitikadi na Imam Baqir AS alikuwa akifika katika vikao vya mtukufu huyo na kunufaika navyo. Mtu huyo anasema sababu ya maingiliano yake mazuri na Imam Baqir AS ni akhlaqi njema na muamala wake mzuri. Alikuwa akimwambia hivi mtukufu huyu: "Wewe unabainisha masuala kwa njia fasaha na ya wazi. Unatumia maneneo mazuri katika kauli zako. Ni kwa sababu hii ndio napata furaha ya kushiriki kwenye vikao vyako."
Pamoja na shughuli zake nyingi za kielimu na kiutamaduni, Imam Baqir AS hakughafilika na masuala ya kisiasa na alikuwa akiwakosoa sana watawala wa kiimla na madhalimu wa zama zake. Katika harakati zake za kuwazindua Waislamu kisiasa, Imam alibainisha sifa za viongozi wema ili watu waweze kuwatia kwenye mizani watawala na wafahamu udhaifu na upotofu wao.
Imam Baqir anasema: "Uongozi wa jamii unamustahiki mtu mwenye sifa tatu. Kwanza ni ucha Mungu ili takwa iweze kumkinga na mitihani ya madaraka kama vile kutumbukia katika mtego wa ufisadi. Pili awe mstahimilifu ili aweza kuzuia hasira zake. Tatu aamiliane na watu anaowatawala kama baba mkarimu na awe na tabia nzuri".
@@@
Wapenzi wasikilizaji kwa mara nyingine tunatoa mkono wa pongezi, kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Baqir AS na tunakamilisha kipindi cha leo kwa maneneo yafuatayo ya mtukufu huyo:
As'wad bin Kathiri anasema: "Nilimpelekea Imam Baqir AS malalamiko yangu kuhusu mambo niliyoyahitaji na upuuzaji wanaonifanyia ndugu zangu. Mtukufu huyo akasema: "Ni ndugu gani huyo anayekujali unapokuwa tajiri na mwenye uwezo lakini anakupuuza na kujiweka mbali nawe unapokuwa kwenye dhiki?" Kisha alitoa amri nipewe msaada wa dirhamu 700 ili nitatuwe nazo matatizo yangu na akaniammbia, "tujulishe hali yako itakavyokuwa."