Siku ya taifa ya teknolojia ya nyuklia
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Ni wakati mwengine umewadia wa kuwa nanyi katika kipindi hiki cha Makala ya Wiki ambacho kwa wiki hii kitazungumzia Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia, inayoadhimishwa hapa nchini tarehe 9 Aprili, inayosadifiana na tarehe 20 Farvardin, kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia. Endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa mnasaba huo.
Tarehe 20 Farvardin mwaka 1385 Hijria Shamsia inayosadifiana na tarehe 9 Aprili mwaka 2007 Miladia ni siku muhimu sana itakayobakia katika kumbukumbu za historia ya Iran katika uga wa mafanikio ya kielimu na kisayansi. Katika siku hiyo, Iran iliwatangazia walimwengu kuwa imepata mafanikio makubwa katika uga wa kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani. Siku hiyo, vyombo vya habari katika pembe mbalimbali za dunia vilitangaza habari ya kuzinduliwa majimui mpya ya pili ya mashinepewa, kwa kimombo centrifuges katika kiwanda cha nyuklia cha Natanz. Mafanikio hayo yaliashiria kufikia Iran hatua ya urutubishaji madini ya urani kiviwanda, na ndiyo maana yaliakisiwa na kuwa gumzo kubwa katika duru za kisiasa ulimwenguni.
Kufikia Iran hatua ya kukamilisha mzunguko kamili wa urutubishaji urani yalikuwa mafanikio makubwa na yenye taathira katika uga wa teknolojia ya nyuklia hapa nchini, ambayo yalifikiwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA); na kwa utaratibu huo Iran ikaingia rasmi kwenye orodha ya nchi zenye teknolojia ya kurutubisha urani.
Kuweza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukamilisha mzunguko kamili wa fueli ya nyuklia licha ya mashinikizo na vizuizi mbalimbali ilivyokabiliana navyo, kwa hakika lilikuwa ni jibu kwa vitisho na vikwazo ilivyowekewa; na hivyo kuwatangazia maadui kuwa Iran haitosalimu amri mbele ya vitisho na mashinikizo na wala haiyumbi katika kutetea haki zake.
Katika hatua zake za kuitaka kuikwamisha Iran isipige hatua katika uga wa teknolojia ya nyuklia, Marekani iliamua, mbali na hatua zake za upande mmoja, kuzishawishi nchi nyengine nyingi, ili nazo pia ziiwekee vikwazo Tehran na kushadidisha mashinikizo dhidi yake. Kwa kutumia njia hiyo ikaziwekea vigingi na vizuizi chungu nzima shughuli za amani za nyuklia za Iran na kushinikiza kupitishwa maazimio kadhaa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ilikuwa ni tarehe 8 Machi mwaka 2006 wakati Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ilipolipeleka faili la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; na kuanzia mwaka huo na kuendelea, yakapitishwa maazimio sita dhidi ya Iran ambayo hayakuhusiana na vikwazo tu. Katika maazimio yake kadhaa liliyopitisha kwa kutumia Sura ya Saba ya Hati ya Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama liliupiga marufuku mpango wa urutubishaji urani wa Iran baada ya kuutangaza kuwa ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa. Lakini baada ya kutangazwa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), hatimaye baraza hilo limekuja kupitisha azimio jipya ambalo limezitambua shughuli za nyuklia za Iran ukiwemo urutubishaji urani kuwa ni shughuli halali na ni haki ya kisheria ya taifa hili.
*******
Hivi sasa, na kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetambulika rasmi kuwa ni nchi inayoendesha shughuli za nyuklia kwa matumizi ya amani zinazojumuisha mzunguko kamili wa fueli na haki ya kurutubisha urani pamoja na kubakisha miundomsingi yake ya nyuklia; tab'an katika hatua ya kujenga hali ya kuaminiana, imekubali kupunguza kwa muda maalumu uendelezaji na ustawishaji wa shughuli zake za nyuklia.
Kwa mujibu wa Mkataba unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia (NPT), ni haki ya kisheria ya kila nchi mwanachama wa mkataba huo kutumia teknolojia ya nyuklia chini ya usimamizi wa wakala wa IAEA; na kutokana na jitihada ilizofanya, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo pia imeweza kunufaika na kuitumia haki hiyo ya kisheria. Kwa mujibu wa mkataba wa NPT, kuzisaidia nchi nyengine wanachama ziweze kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani, ni mojawapo ya malengo muhimu ya mkataba huo wa kimataifa.
Mafanikio katika uga wa teknolojia ya nyuklia hapa nchini Iran yalipatikana hatua kwa hatua. Katika muendelezo wa mchakato huo, mnamo mwaka 2009 wanasayansi wa nyuklia wa Iran walifanikiwa kufanya upambanuzi wa fueli na kuitayarisha ili iweze kutumika kwenye matanurinyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme. Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 2010, katika mafanikio mengine, ilitangazwa rasmi kuwa Iran imefikia hatua ya kujitegemea katika kuzalisha kwa wingi keki ya manjano ya nyuklia. Mwaka 2012, yalizinduliwa mafanikio sita mapya ya nyuklia ikiwemo uzalishaji wa urani asilia ya dioksaidi ambayo ni madaghafi za kinu cha nishati cha maji mazito cha Arak pamoja na aina mpya ya dawa za miali (Radiopharmaceutical); na kwa mara ya kwanza, wanasayansi wa nyuklia wa Iran kuweza kuzalisha fueli ya nyuklia iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20. Kwa kutumia taaluma hiyo, hadi sasa zimetengenezwa aina mbalimbali za dawa zinazotumika katika tiba na vilevile katika kubaini maradhi mbalimbali. Maradhi mengi sugu huweza kubainika na kutibika kwa kutumia dawa hizo za miali. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kupiga hatua kinyuklia katika nyanja za utafiti na ustawi wa miradi ya ujenzi wa vinu vipya vya nishati ya nyuklia. Aidha uendelezaji mpango kamili wa uvumbuzi kwa upande wa angani na ardhini na kubaini vyanzo vipya vya kudhamini madini ya urani, ni miongoni mwa hatua nyengine zinazochukuliwa na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (IAEO) katika kuendeleza maendeleo hayo.
********
Kwa muda wa karibu miaka miwili ya mazungumzo magumu baina ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1, hatimaye tarehe 14 Julai 2015, pande hizo mbili zilipiga hatua moja kubwa kwa ajili ya kufikia makubaliano ya kihistoria. Baada ya mazungumzo hayo na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yaani Russia, China, Marekani, Uingereza na Ufaransa pamoja na Ujerumani, timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran ilifanikisha kufikiwa makubaliano yaliyowezesha kutambuliwa na kupatikana haki za nyuklia za Iran kulingana na mkataba wa NPT, sambamba na kuheshimiwa kikamilifu mistari yake myekundu ikiwa ni pamoja na kuondolewa vikwazo vya kimataifa.
Katika makubaliano ya JCPOA, Iran iliweza kufikia malengo yake makuu kadhaa ikiwemo kubaki na uwezo wake wa kumiliki teknolojia ya nyuklia, kuondolewa vikwazo vya kidhalimu, kutenguliwa maazimio yote ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vilevile kuondolewa faili lake la nyuklia kwenye Sura ya Saba ya Hati ya umoja huo. Na hii ni pamoja na kwamba hakuna kinu wala kiwanda chochote cha nyuklia cha Iran kilichofungwa. Katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA msingi muhimu wa uhakiki na utafiti katika masuala ya nyuklia nao pia ulikubaliwa, na shughuli za kinu cha nishati ya nyuklia cha Arak, ambacho ni miongoni mwa matunda ya kujivunia ya teknolojia ya nyuklia nchini Iran kitaendelea na shughuli zake kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi na ya upeo wa juu zaidi.
Ni kutokana na yote hayo ndio maana Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia na kuorodheshwa kwake katika kalenda rasmi ya serikali inatambulika kama nembo ya jitihada na moyo wa kujiamini wa timu ya wataalamu wa Iran katika sekta ya nyuklia; na katika siku hii hukumbukwa na kuenziwa pia mashahidi wa nyuklia waliotoa mhanga roho zao katika njia hiyo.
Ukweli ni kwamba tangu miaka ya mwanzoni mwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu madola ya kiistikbari yamefanya kila njia ili kuuzuia Mfumo wa Kiislamu usiweze kupiga hatua za maendeleo. Lengo lao lilikuwa ni kutaka kuonyesha kuwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfumo dhaifu na usio na ufanisi, hata hivyo maendeleo na mafanikio iliyopata Iran katika teknolojia ya nyuklia yameyafanya madola hayo ya kibeberu na kiistikbari yashindwe kufikia lengo lao hilo. Kwa azma yake thabiti liliyonayo, taifa la Iran limeonyesha kuwa linao uwezo wa kufikia kilele cha ustawi wa sayansi na teknolojia.
Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu cha Makala ya Wiki kwa juma hili kimefikia tamati. Msiache kujiunga nasi tena wiki ijayo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa makala hii. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani.