Bibi Fatimatu-Zahra (SA), Mama wa Mema na Mazuri Yote
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Tarehe 20 Mfunguo Tisa, Jamadu Thani mwaka wa Hijria imepambwa kwa uzawa wa Bibi Fatimatu-Zahra (sa), binti wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Uzawa wa mtukufu huyo lilikuwa tukio muhimu lililotokea katika miaka ya ujumbe wa Bwana Mtume SAW.
Miaka mitano baada ya kubaathiwa Bwana Mtume SAW na katika siku kama ya leo, nyumba ya mtukufu huyo ilijaa manukato na uturi wa Peponi. Katika siku hiyo Bibi Fatima (sa) alizaliwa na hivyo kuzijaza furaha na bashasha nyoyo za Nabii Muhammad (saw) na mkewe mpendwa Bibi Khadija (sa). Mazazi hayo yalikuwa zawadi kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume (saw) na mkewe Khadija (sa). Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hiyo yenye thamani kubwa, Bwana Mtume alimkumbatia Fatima, akakibusu kipaji chake cha uso kisha akamtazama usoni. Uso huo uliokuwa umejaa nuru ulimpa utulivu mtukufu huyo. Kwa kuzaliwa Fatima, ni kana kwamba Mtume alikuwa amepewa hazina ya dunia na kwa hakika kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, Fatima (sa) alikuwa 'Kauthar', yaani kheri nyingi kwa Bwana Mtume (saw), kama inavyosema Qura'ni yenyewe katika Surat al-Kauthar ya kwamba: Hakika tumekupa kheri nyingi. Basi sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako. Hakika anayekubughudhi ndiye aliyekatikiwa.
Aya hizi ziliwajibu wale maadui waliokuwa wakimbughudhi Mtume (saw) kwa kumkejeli na kumwambia kuwa alikuwa amekatikiwa na kizazi. Kwa hakika aya hizo zilimtuliza Mtume, zikampa matumaini na kumhakikishia kwamba ukweli wa mambo ulikuwa kinyume kabisa na walivyokuwa wakidai maadui wake. Bibi Fatima alizaliwa ili kuwa kigezo na fahari ya wanawake duniani na wakati huohuo kuwa mama na asili ya kizazi cha wabeba bendera ya uongofu kwa ajili ya kutetea dini ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na vigezo vya maadili mema na utu. Bwana Mtume Muhammad SAW alimpa binti yake jina la Fatima kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu amemuweka mbali na maovu pamoja na moto. Amani ya Allah iwe juu ya Fatima (sa)! mbora wa wanawake wa ulimwengu. Amani iwe juu ya mtu aliyependwa zaidi na Mtume wa Allah! Amani na rehma za Allah ziwe juu ya Fatima (sa) ambaye ni kigezo halisi cha mja bora na aliyekamilika. Tunatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa wapenda na watetezi wote wa haki duniani kwa mnasaba wa kuwadia siku hii adhimu ya kuadhimisha uzawa wa Bibi Fatima (sa).
Licha ya kuwa Bibi Fatima (sa) aliishi kwa muda mfupi sana na mama yake mzazi Bibi Khadija (sa), lakini alisikia visa vingi vya kuvutia kuhusu mapambano katika njia ya Mwenyezi Mungu kutoka kwa mama yake huyo. Alipokuwa akiutazama uso wa mama yake, ni kana kwamba alikuwa akisoma ukurasa mpya wa mapambano hayo, ambayo yalikuwa yakiendelea hadi katika zama hizo za uhai wake. Fatima (sa) alijifunza masuala muhimu ya maisha kwa baba yake, Mtume Mtukufu (saw) na alikuwa na nafasi muhimu kwake. Mapenzi na upendo aliouonyesha Mtume kwa binti yake huyo yalikuwa makubwa zaidi kuliko mapenzi ya kawaida yanayoonyeshwa na mzazi kwa mtoto wake, na hilo lilionyesha wazi nafasi, ukamilifu na utukufu aliokuwa nao Fatima (sa). Mtume alikuwa akimpenda sana binti yake huyo na akisema: "Binti yangu mpendwa Fatima, ni fahari ya wanawake wa dunia katika zama na vizazi vyote."
Bibi Fatimatu-Zahra alizaliwa katika jamii ambayo haikuwa na chochote kwa mtazamo wa thamani za kiutu. Tabia na tamaduni potovu kama vile vita, umwagaji damu na kuwazika hai mabinti ambao hawakuwa na hatia yoyote zilikuwa zimefikia kilele katika zama hizo. Kwa kudhihiri Uislamu, Bwana Mtume SAW alipambana vikali na mila hizo chafu. Katika zama ambazo akina baba walikuwa wakichukizwa na kuhuzunishwa sana na kubarikiwa watoto wa kike, Mtume alikuwa akiibusu mikono ya Fatima ili kukabiliana na fikra mbovu za kijahili zilizokuwa zimeenea katika zama hizo dhidi ya watoto wa kike.
Fatimatu-Zahra alizaliwa katika nyumba ya Wahyi na mtu adhimu katika historia ya mwanadamu, ambaye hakuwa mwingine bali ni Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu na hapo akapata maarifa na elimu muhimu kuhusiana na Mola Muumba wa mbingu na ardhi. Kila mara Wahyi ulipokuwa ukimteremkia Mtume na yeye kuamrishwa awabainishie watu hakika na mambo mapya, Fatima (sa) alikuwa akijifunza mengi kutokana na hotuba hizo za Mtume (saw) zilizojaa hekima na busara kuhusiana na ulimwengu. Kwa kuwa na maarifa kama hayo Bibi Fatima (sa) aliweza kupitia njia ya ukamilifu na kupata maarifa muhimu ya Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi pamoja na mambo mengine yote yaliyo mazuri. Akiwa katika kilele cha ibada na ucha-Mungu Fatima (sa) anasema: "Ninashuhudia kwamba Mungu wa ulimwengu ni mmoja tu na hakuna mungu mwingine asiyekuwa Yeye." Bibi Fatima alikuwa na mapenzi makubwa kwa Mwenyezi Mungu kiasi kwamba hakuwa akifikiria jambo jingine isipokuwa kumridhisha Yeye tu. Mtume anathibitisha jambo hilo alipomwambia mmoja wa masahaba zake wa karibu: "Ewe Salman! Mwenyezi Mungu ameujaza moyo na uwepo wote wa Fatima kwa Imani, kiasi kwamba hafikirii wala kufanya jambo lolote isipokuwa kuabudu na kumtii Yeye tu."
Akiwa na mtazamo huo, Bibi Fatima alishiriki vilivyo katika medani za familia na jamii na kuwa mfano bora wa kuigwa na wote katika masuala ya mke na mama mzazi na hivyo kudhihiri kuwa mfano halisi wa mwanamke wa Kiislamu katika jamii. Fatima (as) aliyekuwa na huruma kubwa, daima alikuwa chanzo cha uchangamfu na utulivu kwa mumewe Ali (as). Alikuwa akiichukulia familia kuwa chimbuko halisi la jamii na msingi muhimu uliopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu. Aliyahesabu mazingira ya nyumbani na familia kuwa sehemu ya kujengea malezi bora. Nyumba yake ndogo iliwalea watu wakubwa ambao walikuwa chanzo cha matukio muhimu katika historia ya Uislamu na ya wanadamu wote. Katika mbinu yake ya malezi, Fatima (sa) ambaye yeye mwenyewe alikuwa chemchemi ya elimu na imani, alipanda mbegu ya upendo, tabia njema na maadili mengine mema katika nyoyo za watoto wake. Mfano mmoja bora wa malezi hayo muhimu maishani ni kuwa wakati mmoja Imam Ali na Fatima (as) walifunga kwa siku tatu mfululizo na kuwapa masikini, yatima na mfungwa chakula chao cha futari na kuamua kufuturu kwa kunywa maji tu katika siku hizo za funga ya nadhiri. Jambo hilo liliwashajiisha watoto wao kufuata tabia na sira hiyo ya kuvutia maishani ambapo walijitolea na kujinyima mambo mengi kwa ajili ya kutetea na kuhuisha haki na thamani tukufu za mbinguni. Nyumba ya Fatima ilikuwa nyumba ambayo wakazi wake walifikiria jinsi tu ya kumridhisha Mwenyezi Mungu na kuichukulia ridhaa hiyo kuwa msingi wa matendo yao.
Kwa mtazamo wa Bibi Fatima (sa), mwanamke kushughulikia masuala ya nyumbani na familia hakuna maana ya kumzuia kujishughulisha na masuala mengine ya kijamii, lakini inampasa ajichunge suala hilo lisije likamfanya asahau utambulisho wake na kuanza kujifananisha na wanaume kwa njia isiyofaa. Fatima (sa) anawafundisha wanawake kwamba, ubora wa wanawake haupatikani katika kujifananisha kusikofaa na wanaume, bali ni kutekeleza ipasavyo majukumu yao ambayo wameainishiwa na Mwenyezi Mungu, ambayo kwa hakika wanaume hawana uwezo wa kuyatekeleza. Kwa mtazamo huo, Bibi Fatima (sa) aliyapa kipaumbele majukumu yake ya kuwa mke na mama, na wakati huohuo kujishughulisha pia na masuala ya kijamii na kisiasa. Historia inashuhudia kuwepo kwa bibi huyu mtukufu katika medani mbalimbali na muhimu za Uislamu. Uwepo muhimu wa mtukufu huyo katika matukio tofauti, kuanzia katika hijra hatari ya Mtume (saw) kutoka Makka kuelekea Madina, kuchangia masuala ya kusaidia na kuwapa moyo wapiganaji wa Kiislamu katika medani za vita na vilevile katika matukio ya baada ya kuaga dunia Mtume, yote hayo yanathibitisha wazi mchango mkubwa alioutoa bibi huyo mteule katika nyanja za kijamii na kisiasa. Bibi Fatima (sa) alikabiliana na kupinga vikali watu waliokuwa na nia mbaya ya kutaka kuharibu na kukanyaga thamani za Kiislamu. Hakuwa akihubiri thamani za Kiislamu kwa maneno matupu, bali alikuwa akizitekeleza kivitendo pia na kupambana vilivyo na wale wote waliojaribu kuzikanyaga.
Mtazamo wa kina wa Fatima kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa katika zama zake ulitokana na mafundisho aali ya Qur'ani Tukufu ambayo yalimshajiisha kusimama na kupambana na dhulma, uonevu, ufisadi na ubaguzi katika jamii. Alikuwa akizingatia na kutekeleza kivitendo thamani za kiakhlaki na kimaanawi. Kwa mtazamo wa Fatima (sa), kuizingatia Qur'ani kunatimia kwa kufahamu na kutekeleza mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu. Alikuwa akisema: 'Ikiwa mtu ataifuata Qur'ani, bila shaka atafikia saada na wokovu.' Ni kwa sababu hiyo ndipo, baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw), na ili kuzuia kutokea mfarakano na mgawanyiko miongoni mwa Waislamu, Bibi Fatima akawakumbusha watu nafasi muhimu ya Qur'ani kwa kuwaambia: "Ni kwa nini mnapotea njia hali ya kuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu kiko baina yenu? Mafundisho yake yako wazi na hukumu zake zinang'aa. Alama zake za uongozaji ziko wazi na tahadhari zake zimebainishwa. Je, mnavutiwa na Qur'ani ilihali mnatafuta muamuzi asiyekuwa Qur'ani?" Mbali na kuienzi Qur'ani kwa maneno, Bibi Fatima alikuwa mtekelezaji mkubwa pia wa mafundisho aali ya kitabu hicho kitakatifu cha Mwenyezi Mungu.
Siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatu-Zahra (sa) huadhimishwa hapa nchini Iran kama Siku ya Mwanamke na Mama.Tunatumai kwamba wanawake na akina mama Waislamu duniani watafanya juhudi za kuufahamu vyema Uislamu na kuiga mifano ya wanawake wema kama Fatima (sa) katika kufikia nafasi yao halisi katika familia na jamii, na hivyo kuishi katika mazingira bora wanayostahiki.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.