Hijra ya Mtume (saw) kutoka Makka hadi Madina
(last modified Wed, 30 Oct 2019 10:19:48 GMT )
Oct 30, 2019 10:19 UTC
  • Hijra ya Mtume (saw) kutoka Makka hadi Madina

Jumatano ya wiki hii tarehe Mosi Mfunguo Sita Rabiul Awwal ilisadifiana na siku ya Hijra ya Mtume wetu Muhammad (saw) kutoka Makka na kuhamia Madina na inakumbusha tukio maarufu la "Lailatul Mabiit', usiku ambao ndani yake Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) alisabilia nafsi yake kwa kulala katika kitanda cha Mtume wakati mtukufu huyo alipoondoka Makka akielekea Madina.

Kudhihiri kwa Uislamu katika mji wa Makka halikuwa tukio la kuvumilika kwa mabwanyenye na waliokuwa na nguvu na madaraka ambao walihisi kwamba, dini hiyo mpya inahatarisha viti na maslahi yao. Mabeberu hao, kama walivyo wenzao wa zama hizi, walitumia mbinu zote kwa ajili ya kukabiliana na Uislamu na kuzima nuru yake, na walitumia mashinikizo yote kuwakandamiza wafuasi wa dini hiyo mpya. Mashaka na mashinikizo haya yalimfanya Mtume (saw) afikirie jinsi ya kuwalinda waumini wa awali wa dini hiyo na ndipo ilipukuja fikra ya hijra na kuhama Makka. 

Wakati wa msimu wa ibada ya Hija Mtume Muhammad (saw) alikutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya watu wa Yathrib iliyokuja kujulikana baadaye kwa jina la Madinatu Nabii. Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa makini maneno ya Mtume (saw) watu hao walisimu na kukubali dini ya Mwenyezi Mungu. Kundi hilo la waumini wa kwanza wa Yathrib lilirejea makwao na taratibu idadi ya Waislamu katika mji huo iliongezeka siku baada ya nyingine. Mwaka uliofuatia watu 12 wa Yathrib walikwenda tena Makka na kumpa Mtume Muhammad (saw) bai'a na mkono wa utiifu katika tukio lililojulikana kama Bai'atul Aqaba al Uula.

Idadi ya Waislamu wa Yathrib iliongezeka na katika msimu wa ibada ya Hija ya mwaka wa 13 baada ya kubaathiwa Mtume, walifikia watu 73. Watu hao walimpa Mtume mkono wa utiifu na kula kiapo cha kumlinda na kumnusuru yeye na masabaha zake kama wanavyozilinda na kuzinusuru familia na jamaa zao. Baada ya makubaliano hayo ya Aqaba Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa na kuteswa huko Makka walianza kuhamia Yathrib. Mtume aliwaamuru wahamie Yathrib mmoja mmoja na katika makundi kwa kadiri kwamba, aghlabu ya Waislamu walihahijri na hakubakia Makka isipokuwa Mtume Muhammad (saw) na idadi ndogo ya msahaba zake pamoja na wazee na vikongwe.

Kadiri muda ulivyopita Yathrib ilibadilika na kuwa kituo na makimbilio ya Waislamu. Suala hilo liliwakasirisha sana viongozi wa kabila la Quraish; hivyo wazee wa kabila hilo waliamua kukutana katika eneo la Darun Nadwah kujadili kadhia hiyo. Abu Jahl alikuwa wa kwanza kuzungumza na akatoa pendekezo la kuchagua mtu mmoja wa kwenda kumuua Muhammad. Bwana mwingine alitoa pendekezo la kumkamata Mtume (saw) na kumfunga jela kifungo cha maisha. Mtu mwingine alitoa pendekezo Muhamamd apelekwe uhamishoni. Hata hivyo mapendekezo hayo yote hayakukubaliwa. Wakati huo mzee mmoja alijitokeza na kupendekeza kwamba, wachague mashujaa kutoka makabila yote kisha watu hao wamshambulie kwa mapanga na kumuua Muhammad akiwa amelala kitandani usiku wa manane. Kwa njia hiyo makabila yote yatakuwa yameshiriki katika kumuua Muhammad, na uko wake wa Banii Hashim hautakuwa na uwezo wa kupigana na makabila yote yaliyoshiriki kumwaga damu yake; kwa msingi huo utaridhia kupewa dia. Pendekezo la mzee huyu lilikubaliwa na hadhirina. Waliteuliwa watu wa kutekeleza mpango huo, na usiku wa kwanza wa mfunguo Sita Rabiul Awwal ukaainishwa kuwa ndio wakati wa kutekeleza njama hiyo.

Usiku wa kwanza wa Mfunguo Sita Rabiul Awwal uliwadia na giza lilikuwa limetanda Makka na nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Watu 40 walioizingira nyumba ya Mtume walikuwa wakichungulia ndani kupitia tundu moja la nyumba hiyo. Mapema alfajiri walivamia nyumba ya Mtume na mapanga yao wakiwa tayari kumkatakata Mtukufu huyo. Hata hivyo watu hao 40 kutoka mababila mbalimbali ya Quraish walipigwa na mshangao baada ya kuona kwamba, mtu aliyekuwa amelala kitandani kwa Mtume (saw) alikuwa Ali bin Abi Twalib aliyeamua kujitolea kwa ajili ya kumnusuru Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo usiku huo unajulikana katika historia kama 'Lailatul Mabiit', yaani usiku wa kulala kwenye kitanda cha Mtume.

Lailatul Mabiit

Baada ya kuhamia Yathrib jina la mji huo lilibadilishwa na kuwa Madina Nabii. Kuhamia Mtume katika mji huo kulikuwa kama upepe mwanana wa kipindi cha machipuo uliohinikiza harufu nzuri ya marashi na kueneza furaha na utanashati baina ya wakazi wote wa mji huo. Tarehe 12 Rabiul Awwal Mtume (saw) aliwasili kijiji cha Quba kilichoko karibu na Madina. Baadhi ya vitabu vya historia vinasimulia kwamba: Wakati Mtume (saw) na masahaba zake walipokaribia kijiji cha Quba, bwana mmoja Myahudi aliyekuwa juu ya ngome alimuona mtukufu huyo na wenzake kwa mbali akiwa amevaa nguo nyeupe. Myahudi huyo ambaye alikuwa na habari kwamba Waislamu wa Yathrib wanamsubiri kwa hamu Muhammad (saw) alisema kwa sauti kubwa kwamba: Mtu mnayemsubiri amewasili. Baada ya kupata habari hiyo, baadhi ya makundi ya watu wa Yathrib yalikimbia eneo la Quba kumlaki Mtume na masahaba zake waliokuwa wameketi chini ya kivuli cha mtende. Wakazi wa Yathrib walifurahi sana kusikia habari ya kuwasili Mtume wa Mwenyezi Mungu katika mji huo na walitoka nje wakiwa na mavazi ya vita. Wanawake kwa wanaume walitoka nje kwa vifijo na shangwe na kwenda kumlaki mtukufu huyo. Walikuwa wakiimba mashairi na tungo za kumkaribisha mgeni adhimu na wa aina yake. 

Watu wa Yathrib waliizingira ngamia iliyokuwa imepandwa na Mtume (saw) wakimkaribisha. Vinara wa makabila makubwa ya Yathrib kama makabila ya Banii Salim, Banii Najjar na Banii Khazraj walimwendea mtukufu huyo na kumuomba afikie majumbani mwao. Hata hivyo Mtume (saw) aliwaambia: "Mpisheni ngamia huyu kwa sababu amamerishwa." Watu walimpisha ngamia wa Mtume ili aainishe wapi mtukufu huyo atafikia. Mgamia huyo alipita vitongozi vya Yathrib kimoja baada ya kingine na kwenda moja kwa moja katika eneo la watu maskini na kandokando ya nyumba ya Abu Ayyub al Ansari ambaye alikuwa miongoni mwa watu maskini na mafuraka zaidi wa mji huo. Ngamia alipiga magoti eneo hilo na Mtume akashuka huku akizungukwa na umati mkubwa wa watu. Kila mtu alimuomba afikie nyumbani kwake ili apate sharafu na hadhi ya kuwa mwenyeji wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

اللهم صل علی محمد و آل محمد

Wakati wa shamrashamra hizo, mama yake Abu Ayyub alibeba mizigo ya Mtume (saw) na kuipelekea nyumbani kwake. Mtume ambaye alikuwa bado amezingirwa na watu aliulizia mizigo yake. Aliambiwa kwamba, mama yake Abu Abu Ayyub ameichukua nyumbani kwake. Wakati huo Mtume (saw) alisema: Mtu huwa pamoja na mabegi na mizigo yake ya safari. Kwa utaratibu huo Mtume wa Mwenyezi Mungu aliingia nyumbani kwa Abu Ayyub na alibakia hapo hadi msikiti na chumba chake kilipojengwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: Mtume (saw) aliingia nyumbani kwa Abu Ayyub al Ansari kama mgeni na kujiepusha kwenda kwenye nyumba za matajiri, vinara na wakuu wa makabila wa Yathrib. Hatua hii ya Mtume ilionesha msimamo wake wa kijamii. Kitendo hiki cha Mtume kilidhihirisha kwamba, shakhsaia huyu hategemei nguvu ya fedha, hadhi na mafungamano ya kikabila na sharafu na nguvu ya utawala na kabila fulani, na wala hatakuwa tegemezi kwa kaumu na kabila, familia, mabwanyenye na mfano wake…

Katika nyakati hizo za mwanzoni mwa kuwasili Yathrib, Mtume (saw) alionesha atakuwua mtetezi wa kundi gani katika mienendo yake ya kijamii. Naam, watu wa matabaka yote watafaidika na mienendo na mafundisho yake lakini hapana shaka kuwa, watu waliokuwa wakidhulumiwa na haki zao kukanyagwa ndio watakaofaidika zaidi kutokea na kuwepo kwake.

Mbele ya nyumba ya Abu Ayyub al Ansari kulikuwepo ardhi iliyoachwa hivihivi bila ya kutumiwa. Mtume (saw) aliuliza, ardhi hii ni mali ya nani? Aliambiwa kwamba ni mali ya watoto wawili mayatima. Alitoa fedha kwenye kifuko kidogo na kununua ardhi hiyo. Kisha akasema tutajenga msikiti katika ardhi hii kwa maana ya kujenga kituo cha masuala ya kisiasa, kiibada, kijamii na makao ya serikali mahala hapo. Waislamu walianza mara moja kujenga msikiti eneo hilo. Mtume (saw) alinunua ardhi ya kujenga msikiti kwa fedha zake mwenyewe na hakusubiri kupewa. Vilevile aliwasimamia watoto hao mayatima na kuwa kama baba yao mzazi. Aliwapa haki zao zote. Ulipochukuliwa uamuzi wa kujenga msikiti, Mtume Muhammad (saw) alikuwa wa kwanza kabisa kuchimba msingi wa ujenzi wa msikiti huo kwa mikono yake mwenyewe.

Maasjidu Nabii

Hakufanya hivyo kirasmi na kimaonyesho kama wafanyavyo viongozi wa zama hizi, bali kama mjenzi na mfanyakazi halisi. Alichimba na kubeba vifaa vya ujenzi kwa mikono yake hadi akabubujikwa na jasho. Kitendo hicho kiliwahamasisha Waislamu walioamua kujifunga kibwebwe na kujenga msikiti wa Madina katika kipindi kifupi. Kwa harakati yake hiyo, Mtume (saw) alionesha kuwa, licha ya nafasi yake adhimu na hadhi yake kubwa baina ya watu lakini hakuna tofauti baina yake na watu wengine katika masuala ya kijamii.

Mtume (saw) alihamia Madina kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri zaidi ya kupambana na dhulma iliyokuwa inatawala jamii za wanadamu katika kipindi hicho na kueneza neno la Mwenyezi Mungu SW. Hijra hiyo iliweka jiwe la msingi la kuasisiwa mfumo wa utawala wa Kiislamu utakaokuwa kigezo bora cha kuigwa katika vipindi vyovye vya historia ya mwanadamu. Hijra hiyo ya Mtume ilikuwa sababu ya kubakia hai Uisalmu na kueneza dini hiyo ya Mwenyezi Mungu katika maeneo mengine ya dunia.  

Miongoni mwa matunda muhimu ya Hijra ya Mtume (saw) ni kupata eneo salama la kuweza kutumia kwa ajili ya kumwabudia Mwenyezi Mungu na kutekeleza maamrisho yake. Kwa msingi huo Qur'ani tukufu inawakemea Waislamu waliobakia katika safu za makafiri na kukubali kudhalilishwa na kudunishwa na kuwapongeza Muhajirina waliocha kila kitu na kuhama makazi na miji yao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Aya ya 100 ya Suratu Nisaa inasema:

وَمَن یُهَاجِرْ فِی سَبِیلِ اللَّهِ یَجِدْ فِی الأَرْضِ مُرَاغَمًا کَثِیرًا وَسَعَةً وَمَن یَخْرُجْ مِن بَیْتِهِ مُهَاجِرًا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ یُدْرِکْهُ الْمَوْتُ فَقَدْ وَقَعَ أَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ وَکَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِیمًا

Na mwenye kuhama katika Njia ya Mwenyezi Mungu atapata pengi duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na anayetoka nyumbani kwake kuhama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti njiani basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.