Nov 11, 2019 07:56 UTC
  • Wiki ya Umoja wa Kiislamu-2  (Ruwaza Njema)

Alipozaliwa alipewa jina la Muhammad lenye maana ya msifiwa. Jina hili hakuwahi kupewa kiumbe mwingine kabla yake yeye. Jina hilo, kama alivyokuwa yeye mwenyewe, liliteuliwa na Mwenyezi Mungu Muweza na lilitajwa katika vitabu vya Mitume waliotangua.

Hii leo ni watu wachache sana dunia kote ambao hawajawahi kusikia au kusoma jina la Muhammad msifiwa na mwaminifu ambalo linatukuzwa na kuadhimishwa na zaidi ya Waislamu bilioni moja na nusu kila siku katika maombi na swala zao. Alihuisha thamani za kibinadamu na kubeba bendera ya Tauhidi na kumpwekesha Mungu mmoja badala ya ibada ya masanamu na mizimu. Muhammad alikuwa dhihirisho la kila jema, safi, tukufu na maadili yote mema. 

Katika kipindi chote cha uhai wake, mwanadamu hutafuta ruwaza njema na kigezo cha kufuata na kuiga katika maudhui makhsusi au katika maisha yake yote kwa ujumla kwa shabaha ya kufika kwenye muradi na makusudio yake. Ruwaza njema na kigezo ni miongoni mwa mambo yaliyopewa nafasi ya juu sana katika mijadala ya elimu na malezi, elimu ya nafsi, irfani na masuala ya kiidara. Uislamu kama dini kamili zaidi ya Mwenyezi Mungu, pia haikupuuza suala hilo, na daima imekuwa ikitoa na kuonesha vigezo vya kufuatwa na wanadamu katika awamu na vipindi mbalimbali vya historia. Mwenyezi Mungu SW anataja kigezo na ruwaza njema zaidi ya kufuatwa na wanadamu katika aya ya 21 ya Suratul Ahzab kwa kusema: Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana

Aya hii inawahusu Waislamu wote katika kila zama na mahala walipo na inaweka wazi kwamba, kumfuata na kumuiga Mtume Muhammad (saw) hakufungamani na zama au eneo makhsusi. Kwa hakika miongoni mwa nguzo za Uislamu na kumwamini Mtume Muhammad (saw) ni kufuata njia na mwenendo wake yeye (saw) ambaye alistahamili mashaka makubwa kupita kiasi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwaelekeza wanadamu katika njia ya saada na ufanisi. 

Si rahisi kupata mtu ambaye amesifiwa na kutukuzwa sana katika Qur'ani tukufu zaidi ya Muhammad (saw). Katika Qur'ani tukufu Muhammad kama walivyo wanadamu wengine, ni kiumbe anayeishi, kula, kulala na kadhalika, lakini wakati huo huo ni kito na johari inayong'aa na kumeremeta baina ya viumbe wote. Qur'ani inataja sifa ya Muhammad (saw) kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwanadamu kamili zaidi ya wote. Ni kiongozi na kinawa wa viumbe aliyeasisi ustaarabu mpya na uadilifu unaotembea mitaani. Kwa sababu hiyo Qur'ani tukufu inamtaja Muhammad (saw) kuwa ni kigezo na ruwaza njema kwa wanadamu wote.

Muhammad (saw) alikuwa mithili ya nahodha wa safina ambaye pale chombo kinapokumbwa na dhoruba na mawimbi makali husimama imara na kukabiliana na mawimbi hayo ili kuhakikisha safina inafika bara ya amani. Alikuwa akifanya kazi pamoja na masahaba zake kama inavyotuhadithia historia kwamba, alikuwa akibeba mawe na kushiriki katika ujenzi wa Msikiti wa Madina, au wakati aliposhiriki katika kuchimba handaki kandokando ya Madina akitumia sururu na sepetu. Alikuwa akitaniana na masahaba, akiwapa moyo na motisha na kuwahamasisha kusoma Qur'ani na tungo za hamasa. Daima alikuwa akiwahimiza watu kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na kuwapa bishara ya mustakbali mwema na bora. Aliwatahadharisha kuhusu fitina za wanafiki na kuwataka wawe macho na makini na watu wa aina hii. Wakati wote alikuwa akichagua mbinu sahihi na bora zaidi za vita na masuala ya kijeshi na kukabiliana na maadui wa ubinadamu. Naam, Muhammad alikuwa kigezo bora na ruwaza njema kwa waumini na wanadamu wote katika medani na mambo yote. 

Katika aya ya 4 ya Suratul Qalam, Mwenyezi Mungu SW anamtaja Muhammad (saw) kuwa ana maadili adhimu na bora zaidi. Aya hiyo inasema:

Na hakika wewe una tabia tukufu. Katika aya hii Mwenyezi Mungu anasifu tabia za Mtume wake na kuzitaja kuwa ni adhimu. Si hayo tu, bali kitabu hicho cha mbinguni kinataja tabia njema za Mtume Muhammad (saw) kuwa ndiyo sababu ya mafanikio yake katika kutangaza ujumbe wa Mola Muumba na kisha kinasifu kilele cha upendo, huruma na upole wake kwa kusema: Hakika amewajieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayokutaabisheni; anawahangaikia nyinyi sana, kwa waumini ni mpole na mwenye huruma.

Hapana shaka yoyote kwamba, maisha ya Mtume Muhammad (saw) ni ruwaza na kigezo bora zaidi cha maisha ya kiumbe mwanadamu yeyeto anayetaka kupata saada na ufaniisi wa dunia na Akhera.

Huruma na upendo wa Muhammad (saw) pia ulikuwa wa kupigiwa mfano na ni muhali kuweza kupa mithili yake. Daima aliwajulia hali masahaba zake, na kama hakumuona mmoja wao kwa muda wa siku tatu aliwauliza wengine hali yake. Kama atakuwa safarini alikuwa akimuombea dua njema, na kama alikuwa nyumbani kwake alikuwa akienda kumtembelea na kumjulia hali. Si hayo tu bali hata maadui zake walifaidika na bahari ya upendo na huruma ya Muhammad. Historia inahadithia kwamba, wakati wa vita vya Badr Waislamu walifanikiwa kudhibiti visima vya maji vya eneo hilo na wakajenga hodhi na kisha kujaza maji ndani yake. Wakati jeshi la adui lilipokaribia eneo hilo kwa ajili ya kunywa maji baadhi ya Waislamu walitaka kuwanyima maji lakini Mtume wa upendo na huruma, Muhammad aliwaamuru Waislamu wawaruhusu makafiri na maadui zake watumie maji hayo.

Katika upande mwingine uadilifu wa Muhammad (saw) ulikuwa miongoni mwa sifa zake kuu katika mambo yote kwa kadiri kwamba, sifa hiyo ilidhihiri na kutawala mienendo na harakati zake zote, kubwa na ndogo. Naam, Muhammad alikuwa mwadilifu hata katika kuwatazama watu waliokuwa wakiketi kandokando yake. Mjukuu wa Mtume (saw), yaani Imam Ja'far Swadiq (as) anasimulia kwamba: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akigawa kwa usawa hata jinsi ya kuwatazama masahaba zake, na alichunga uadilifu katika kumtazama huyu na yule" 

Muhammad (saw) alitumia mantiki, busara, hikima na akili sambamba na mawaidha mema na kauli nzuri iliyoandamana na upendo na upole katika kuwalingania watu dini na ujumbe wa Allah. Alitumia vitu hivyo kwa ajili ya kuingia katika akili na nyoyo za watu. Katika uwanja huu pia alikuwa kigezo bora zaidi cha kufuatwa na kuigwa. Aliwalingania watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa adabu kamili iliyoandamana na upendo na hamu kubwa ya kutaka kuwaongoza njia sahihi. 

Hapana shaka kuwa Muhammad (saw) alikuwa mwanadamu adhimu na asiye na kifani. Hakuwa na hatakuwa na mithili yake baina ya wa binadamu na kwa ufupi tu tunaweza kusema kuwa, alifika katika kilele cha ukamilifu wa mwanadamu katika kila kitu. Alikuwa mwalimu hodari aliyelea rijali adhimu, mtunga sheria mahiri, kiongozi shupavu, kadhi mwadilifu, mchapakazi makini na daktari aliyejua vyema maradhi na matatizo ya wagonjwa wake ya jinsi ya kuyatibu. Muhammad alifanya mapinduzi makubwa zaidi katika dunia hii.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Ali Khameni anasema: "Mwenyezi Mungu SW ametuamuru sisi Waislamu kumfuata Mtume Muhammad (saw). Ufuasi huo unahusu kila kitu maishani mwetu, kwa sababu mtukufu huyo alikuwa ruwaza njema na kigezo bora cha kuigwa si katika maneno yake tu, bali pia katika mienendo yake, katika sira na maisha yake, katika jinsi ya kuamiliana na watu, familia na marafiki zetu, bali hata katika jinsi ya kuamiliana na maadui, katika jinsi ya kusuhubiana na watu dhaifu, wenye nguvu na katika kila kitu... Hivyo basi kama hatuwezi kufuata nyayo za mtukufu huyo mia kwa mia, kwa uchache tujitahidi kujifananisha naye katika mienendo yetu…"

Tags