Feb 21, 2020 10:06 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama

Tarehe 21 Februari inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama.

Lugha, wapenzi wasikilizaji, ni kitu muhimu sana katika maisha ya kiumbe mwanadamu. Kupitia lugha wanadamu wanaweza kuwasiliana, kutafakari, kueleza hisia zao za ndani ya nafsi na kutengeneza hali ya amani kwa mtu binafsi na wanaomzunguka. Hata hivyo baina ya lugha mbalimbali zinazoweza kuwa zinazungumza na mtu, lugha ya mama inabakia kuwa na umuhimu wa aina yake. Ni kwa sababu hiyo na ili kulinda aina tofauti za lugha na tamaduni za dunia, ndipo Shirika ya Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwaka 1999 likaitangaza siku ya tarehe 21 Februari kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama. 

Asili ya Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama ni tukio la mwaka wa 1952 nchini Bangladesh, wakati wanafunzi wa chuo kikuu wa Dhaka walipofanya maandamano wakitaka kutambuliwa rasmi lugha ya Bangla, na wanne miongoni mwao wakauawa kwa kipigwa risasi na polisi.

Siku ya Lugha ya Mama husherehekewa kila mwaka katika nchi zilizojiunga na UNESCO kwa ajili ya kujadili mambo ya wingi wa lugha, haki za lugha zote, na mazingira ya kutumia lugha tofauti. Kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama ni "Languages Without Borders" kwa maana ya Lugha Zisizo na Mipaka. 

Wataalamu wengi wa elimu nafsi wanaamini kuwa, lugha ya mama ni lugha ambayo hutumiwa na mama kuzungumza na mtoto anayekuwa tumboni mwake katika kipindi cha ujauzito, na tunaweza kuitaja kuwa ndio sauti ya kwanza kabisa inayosikizwa na mtoto. Pindi anapozaliwa mtoto huyo hunyamanza na kuacha kulia pale anaposikia sauti ya mama yake mzazi; hii ni kwa sababu huanisika na sauti hiyo ya mama ambayo amekuwa akiisikia tangu akiwa tumboni mwake. Wataalamu hao wa elimu nafsi wanasema kuwa, lugha ya mama ndiyo lugha ya utotoni ya mwanadamu na lugha ya kueleza hisia na matakwa yake ya kimaumbile na ya kipindi cha utotoni. Baadhi ya wataalamu wanaiita lugha ya mama kuwa ndiyo "lugha ya awali" kwa sababu ndiyo lugha ya kwanza anayojifunza na kuisikia mtoto.

Nukta ya kuvutia zaidi ni kwamba, ubongo wa mwanadamu una muundo tata sana na uwezo wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuzungumza na kujifunza lugha. Utafiti uliofanywa na wataalamu hao unasema kuwa, watoto ambao tangu baada ya kuzaliwa huwajihiana na lugha tofauti, huwa na uwezo wa kujifunza lugha kadhaa, na lugha hizo hufanya kazi sawa katika ubongo wao. Baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa, kujifunza lugha ya pili au ya tatu kwa wanadamu kunaathiriwa sana na jinsi wanavyoielewa lugha ya mama na uwezo wao wa kuchambua na kunyambua lugha hiyo. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, lugha ya mama ni msingi wa kijifunza lugha nyingine au kwa maneno fasaha zaidi “lugha ya mama ni mama wa lugha zote.”

Katika zama za sasa lugha nyingi za mama katika pembe mbalimbali za dunia zinakabiliwa na hatari ya kutoweka kabisa. Walimwengu wanazungumza zaidi ya lugha elfu 6 ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) nusu ya lugha hizo imo katika hali ya kutoweka. Baadhi ya ripoti pia zinasema kuwa, idadi ya wazungumzao baadhi ya lugha za dunia hii imepungua na kufikia watu elfu 10 na katika maeneo mengine wamekuwa chini ya watu elfu moja. Wanasisitiza kuwa suala hili ni kengele ya hatari kwa dunia nzima.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa, wingi na kuwepo kwa lugha tofauti duniani ni kielelezo cha utajiri wa kiutamaduni na kwamba lugha zote zilizopo ni turathi ya wanadamu wote. Umoja huo unasisitiza kuwa, kuna udharura wa kulindwa lugha zote za mama ili zisitoweke au kusahaulika. Taasisi hiyo ya kimataifa pia imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kulinda haki za lugha za watu ambao ni jamii za waliowachache katika nchi zao na wanalazimishwa kutumia lugha ya waliowengi. Vilevile Umoja wa Mataifa unazitaka serikali za nchi mbalimbali kutambua rasmi wingi wa lugha na kutayarisha mazingira mazuri ya kuwepo haki sawa kwa lugha zote katika nyanja zote ikiwemo haki ya kufundishwa lugha ya mama. Mwandishi wa Czech, Milan Kundera anasema: "Hatua ya kwanza ya kuangamiza taifa lolote ni kufuta kumbukumbu zake na kuangamiza vitabu vyake, utamaduni wake na lugha yake.”     

Baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza kwamba, ni kwa nini taasisi na jumuiya mbalimbali zinasisitiza udharura wa kulindwa lugha ya mama?

Kila lugha ni hazina ya historia, fasihi, elimu na maarifa na iwapo lugha hiyo itatoweka basi utamaduni na ustaarabu wa wanadamu pia unapungua na kuwa maskini zaidi. Umuhimu wa lugha ya mama unaoneka zaidi katika kuwafunza watoto wadogo. Kuwapa mafunzo watoto wadogo kwa kutumia lugha ya mama zao huwa na tija na matunda makubwa zaidi katika ustawi wao wa kimasomo, na miongoni mwa mambo yenye umuhimu mkubwa ni wazazi wawili kuzungumza na watoto wao kwa kutumia lugha ya mama ili watoto wasibakie njia pandana na katika hali ya sitafahamu. Kutohamishwa na kutofunzwa lugha ya mama kwa vizazi vya baadaye kunazifanya lugha hizo zitoweke taratibu na polepole. Wataalamu wanasema kuwa, pale lugha nyingine zitakapotoweka na kukabakia lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kichina tu ulimwengu wetu utatumbukia katika umaskini wa kiutamaduni.

Hivyo, shirika la UNESCO limekuwa likitilia mkazo udharura wa kulindwa lugha za mama ili watu binafsi na jamii zisipoteze utambulisho wao. Shirika hilo linazihimiza tawala na serikali za nchi mbalimbali kuenzi na kustawisha lugha za mama zilizopo katika nchi hizo na zisitangaze lugha moja tu na kuiarifisha kama utambulisho wao wa kitaifa.

Tangu zamani nyanda za juu za Iran (Iranian Plateau) yalikuwa maskani ya kaumu na watu  asili wa maeneo hayo, na kila moja kati ya kaumu hizo ilikuwa na lugha na utambulisho wake. Baada ya kuwasili kaumu ya Aryan katika maeneo hayo ya kale, ustaarabu na maendeleo ya eneo hilo yalishika kasi kubwa zaidi na kuifanya Iran kuwa miongoni mwa tawala na madola yenye nguvu kubwa duniani, dola ambalo lilikuwa na tamaduni na kaumu nyingi. Tamaduni hizo tofauti zinaweza kushuhudiwa hii leo katika lugha za mama za kaumu mbalimbali zinazopatikana katika maeneo mbalimbali ya Iran. Hii leo kunapatikana lugha na lahaja karibu 69 nchini Iran kama vile lugha ya Kifarsi, Kiazari, Kiarabu, Kikurdi, Gilaki, Mazani, Lori, Taleshi na Tati. Kila moja kati ya lugha hizo inawakilisha utamaduni na sanaa ya kundi au kaumu ya watu wa Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya jitihada za kuhakikisha kwamba, lugha hizo zote zinalindwa. Hii ni kwa sababu inaelewa kwamba, kutoweka kwa kila moja kati ya lugha hizo kuna maana ya kutoweka sehemu moja ya utamaduni na historia ya Iran.  

Kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, japokuwa lugha na kaligrafia rasmi ya Wairani wote ni Kifarsi lakini inaruhusiwa kutumia lugha za kienyeji na za kaumu mbalimbali katika magazeti, vyombo vya habari vya mawasiliano ya umma na katika kufundisha fasihi za lugha hizo katika shule za wakazi wa maeneo husika na wazungumzaji wa lugha hizo. Vilevile kwa mujibu wa hati ya haki za kiraia, kila Muirani ana haki ya kujifunza, kutumia na kufundisha lugha na lahaja za kienyeji. Hapa nchini pia kumefanyika jitihada kubwa za kuimarisha lugha za mama ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo cha lugha na fasihi ya lugha ya Kikurdi katika Chuo Kikuu cha Kurdistan na kitengo cha lugha na fasihi ya Kiazari katika Chuo Kikuu cha Tabriz.

Lugha za dunia hii zimekata masafa na vipindi vingi na virefu tangu zilipoanza kuundika hadi zinakuwa lugha kamili na kila lugha imetengeneza cheni na mnyororo wa historia ya wanadamu kutokana na dafina na vito vyake vya thamani. Sisi pia, kama warithi wa lugha za mama, tunawajibika kufanya jitihada za kulinda lugha hizo ambazo ndizo zinazounda utambulisho wa kila mmoja wetu na kukabidhi lugha hizo kwa vizazi vivyavyo ili mnyororo huo wa dhahabu, usitoweke.    

Tags