Kwa mnasaba wa siku ya kuzaliwa Imam Sajjad AS
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika dakika hizi za kipindi hiki maalumu ambacho tumekuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS mmoja wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW. Kabla ya jambo lolote tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wapenzi wote wa Ahlul Bait AS na wapenzi wote wa haki duniani kwa mnasaba huu tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.
Mwezi 5 Shaaban ya kila mwaka inasadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Hussein AS, Imam ambaye kwa upande mmoja alikuwa ni 'pambo la wafanya ibada' na kwa minajili hiyo akapewa lakabu ya 'Zaynul Abidiin', na kwa upande mwingine alifanya juhudi kubwa za kufikia malengo matukufu ya babu yake, Mtume Mtukufu Muhammad SAW ya kuwepo utawala wa Allah SW katika pembe zote za dunia.
Imam Ali bin Hussein AS alizaliwa mwezi 5 Shaaban mwaka 38 Hijria katika mji wa Madina na baba yake ni Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS na mama yake ni Bi. Shaharbanu, aliyekuwa mmoja wa mabanati wa mfalme wa Kiirani. Hali ya kisiasa katika zama za Imam Sajjad AS ilikuwa nyeti na tata mno, baada ya Imam Hussein AS kusimama kidete dhidi ya utawala fasiki wa Bani Umayyah na hatimaye kuuawa shahidi huko Karbala.
Imam Sajjad AS alipambana na fikra potofu za watu waliokuwa wanataka kuupotosha Uislamu, wakati ambao jamii ya Kiislamu ilikuwa imezama kwenye hofu na woga. Kwani kitendo cha kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW na kushikwa mateka watu wa familia yake, kilikuwa ni cha jinai isiyo na mfano. Kipindi cha Imam Sajjad AS kilisadifiana na kipindi cha harakati za kijamii.
Kipindi hicho kilikuwa kimegubikwa na vitendo vya upotoshaji wa sheria za Kiislamu, kwani utawala wa Bani Umayyah ulikuwa ukiwapotosha Waislamu kwa kuwapelekea wapokezi waongo wa hadithi na riwaya zisizo sahihi bali za kumsingizia Bwana Mtume Muhammad SAW mambo ambayo hakuyasema wala hakuyatenda. Harakati za Imam Sajjad AS zilileta mabadiliko makubwa, kwani baadhi ya watu walifikiri kwamba, Imam AS alikuwa amejikita zaidi kwenye masuala ya kiibada tu, na kujiepusha na masuala ya kijamii na kidunia.
Hali ngumu na mbinyo uliokuwa ukitolewa na Bani Umayyah kwa upande mmoja na hali ya kiutamaduni na kijamii iliyokuwa ikitawala kipindi hicho kwa watu waliokuwa mbali na mafunzo sahihi ya Kiislamu kwa upande wa pili, ilimuongezea Imam Sajjad AS moyo na ari kubwa ya kuwalingania watu kwenye njia ya haki. Imam Ali bin Hussein AS aliamua kutumia mbinu mpya ya kimantiki na busara zaidi kwa lengo la kuhuisha fikra halisi ya Kiislamu. Imam Sajjad AS aliamua kutumia mawaidha na dua kwa lengo la kufikia kwenye malengo ya kimaanawi na ya kiharakati.
Alichukua hatua hiyo ili kukabiliana na harakati za kimaada za watu wa zama hizo. Kwa hakika Imam Ali Zainul Abidiin AS alichukua njia sahihi na bora zaidi ya kutumia dua na nasaha ili kufikisha itikadi, ujumbe na fikra sahihi, zilizokuwa zikihitajika kwa watu walioishi katika kipindi hicho.
*******
Moja ya nasaha zilizotolewa na Imam Sajjad AS wakati alipokuwa akitoa mawaidha kwenye Msikiti wa Mtume SAW katika siku za Ijumaa alisema: 'Jambo la kwanza atakalokutana nalo mja wa Allah akiwa kwenye barzakh, ni kuulizwa maswali kutoka kwa Malaika wawili waliotumwa na Allah SW kuhusiana na Mungu aliyekuwa akimuabudu mtu, Mtume aliyeteremshiwa, dini aliyokuwa akiifuata, kitabu alichokuwa akikisoma na Imam aliyekuwa akimfuata.'
Imam Sajjad AS alikuwa akibainisha kwa uwazi mkubwa itikadi ya asili ya Uislamu, yaani tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Utume, Kiyama na suala muhimu la Uimamu. Maimamu AS wanauelezea Uimamu kuwa ndio huohuo utawala. Imam anayeelezwa hapa ni mrithi wa Mtume Mtukufu SAW, yaani shakhsia adhimu anayebeba jukumu la kuwaongoza watu katika masuala ya kidini na ya kidunia, na bila shaka kumtii yeye ni wajibu kwa Waislamu wote, kama ilivyokuwa sawa na kumtii Mtume Mtukufu SAW.
Watu katika zama hizo walikuwa mbali na mafundisho ya Uislamu na wengi walikuwa wanafikiri kwamba mtu mmoja anatawala katika masuala ya kidunia na mwingine anatawala katika masuala ya kidini na majukumu hayo mawili hayawezi kufanywa na mtu mmoja kwa wakati mmoja. Bila shaka mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Imam Sajjad AS yalikuwa yakiwakera na kuwachukiza mno makhalifa na viongozi wa Bani Umayyah, kwani Imam AS alikuwa akibainisha kinagaubaga suala la Uimamu, kuwa ni mfumo wa utawala wa Kiislamu na uongozi kwa jamii ya Kiislamu.
Kwa kutumia njia hiyo hiyo, Imam Sajjad AS alikuwa akiwaeleza watu kile kinachojiri kwenye jamii ya Kiislamu na hasa kuhusiana na tawala zilizokuwa zikitumia mabavu, zilizojaa ufasiki na unafiki kama vile utawala wa Yazid na Abdul Malik Marwan ambazo hazikutawala kwa mujibu wa misingi na sheria za Kiislamu.
Abu Hamza Thumali mmoja wa wafuasi na wasaidizi wa karibu wa Imam Sajjad AS amenukuliwa akisema kwamba, Imam AS alikuwa akiwausia wafuasi wake na waumini wengine wajiweke mbali na maliwazo na faraja za uwongo walizopewa na watawala madhalimu. Imam Sajjad alikuwa akiwatahadharisha wafuasi wake na suala zima la kushirikiana na watawala madhalimu na kuwaonya kuwa viongozi hao walikuwa wakiwahadaa kwa anasa na vivutio hivyo bandia na vya kughururisha vya kidunia ili kudhoofisha imani zao na wakati huohuo kupunguza makali ya upinzani wao dhidi ya mfumo wa utawala wa Bani Umayyah.
Imam alikuwa akisema: 'Enyi waumini! Hawa mataghuti ni watu walioikumbatia dunia, nyoyo zao zimezama kwenye ulimwengu huu, hivyo msihadaike na neema zisizokuwa na thamani na zenye ladha ya muda mfupi tu.' Imam Sajjad alikuwa akiwataka wafuasi wake wajifunge kibwebwe katika kukabiliana na vitendo vya dhulma na ukandamizaji na kuwakumbusha misukosuko na mashinikizo makubwa waliyoyapata wafuasi wa Ahlul Bait AS katika zama za Muawiya, Yazid na Marwan.
Katika lahdha kama hizo, Imam Sajjad AS alikuwa akielezea pia suala la Uimamu na kubainisha ni mtu gani aliyepaswa kufuatwa baada ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na ili kuondoa shaka na wasiwasi kwenye nyoyo na fikra za wafuasi wake na hadhirina alikuwa akisema; 'Tangulizeni na wekeni mbele amri ya Mwenyezi Mungu ya kumtii mtu ambaye Mwenyezi Mungu amelazimisha atiiwe, na kamwe msiwatangulize mataghuti ambao wamepumbazika na kuikumbatia dunia'.
******
Dua ni moja ya mbinu zilizokuwa zikitumiwa na Imam Sajjad AS katika kufanya tablighi wakati wa zama zake. Mtukufu huyo alikuwa akibainisha masuala mbalimbali kama vile ya kielimu, maarifa ya Kiislamu, kiirfani, kijamii, kimalezi na masuala nyeti ya kisiasa katika sura ya dua, ambapo dua zake nyingi zimekusanywa kwenye kitabu kinachoitwa Swahiifat Sajjadiyyah. Katika kitabu hicho ambacho kinajulikana pia kwa jina la 'Injili ya Ahlul Bait' na 'Zaburi ya Watu wa Muhammad', Imam Sajjad AS kwa kutumia njia ya dua ameweka vigezo mbalimbali vya maisha ya Kiislamu kwenye fikra za watu.
Huku akionesha upeo wake mpana wa kuelewa masuala ya zama hizo na zama zitakazokuja baadaye, Imam Ali bnil Hussein Zainul Abidiin AS aliwaamsha watu walio wengi ambao walikuwa wamepumbazika na dunia na kuyapa mgongo masuala ya ibada na mafundisho ya Kiislamu, na alitumia dua kama njia ya kuwaamsha na kuwaongoza kwenye njia ya kumuabudu Allah SW na kujiidilisha kufuata mambo ya kimaanawi. Jambo la kuzingatiwa hapa ni kwamba, Imam AS kwa kutumia dua aliweza kubainisha wazi masuala ya Uimamu na haki ya Ahlul Bait AS katika kadhia ya kuchukua uongozi wa jamii ya Kiislamu.
Mbinu nyingine zilizotumiwa na Imam Sajjad AS za kuweka wazi zaidi nafasi ya Ahul Bayt AS, ilikuwa ni suala la kukaririwa kwenye dua zake utajo huu wa kumswalia Mtume na Aali zake watoharifu kwa kusema 'Rehema na amani za Allah ziwe kwa Mtume Muhammad na Aali Muhammad'.
Ni vyema hapa wapenzi wasikilizaji tukunukulieni baadhi ya miongozo iliyojaa hekima iliyotolewa na Imam Sajjad AS kwa ajili ya watu wa zama zake na zama za baada yake hadi zama zetu hizi na zitakazokuja baadaye.
Kama tulivyotangulia kusema, sehemu kubwa iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Sajjad AS ni ucha Mungu wake mkubwa na ibada zake nyingi mno. Kama tulivyosema pia kuwa kitabu cha dua cha Sahifatu Sajjadia ni miongoni mwa urithi bora kabisa tulioachiwa Waislamu na mtukufu huyo. Imam Sajjad AS alitumia muda wake mwingi kuwalingania watu kujiepusha na madhambi. Hadithi nyingi zimepokewa kutoka kwa mtukufu huyo kuhusu suala hilo, hadithi ambazo zinaweza pia kuwa dawa ya kumzuia mtu na kufanya madhambi mazito kama ya kusengenya.
Katika moja ya hadithi zake, Imam Sajjad (AS) amesema: "Mtu anayeuzuia ulimi wake usiwafedheheshe na kuwaharibia watu heshima zao, Mwenyezi Mungu atayafumbia macho madhambi yake Siku ya Kiyama".
Vile vile alikuwa akisisitizia mno suala la kutumia hekima katika kulingania watu dini. Pia alikuwa akimiza mno wajibu wa kujua mbinu za kulingania dini ya Allah SWT.
Katika hadithi moja iliyopokewa na Sheikh Kulaini katika kitabu cha al Kafi na kupokewa pia na maulamaa wengine wa Hadithi inasema: Mabwana kadhaa wa Kiquraish walimuuliza Imam Ali bin Hussain Sajjad AS kwamba: Tuwalinganie vipi watu dini hii? Imam Zainul Abidin AS aliwabainishia misingi ya dini na kuashiria kwamba misingi hiyo ni kuamini Utume wa Nabii Muhammad SAW. Aidha alisema: Mhimili wa nguzo zote hizo ni mambo mawili ambayo ni maarifa na kumjua Mwenyezi Mungu Mtukufu na kutafuta radhi Zake.
Pia amenukuliwa akisema: Kumjua Mwenyezi Mungu ni kumpwekesha Yeye na kutambua kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma, Mrehemevu, Mwenye nguvu na utukufu, Mwenye ilimu na kudra na kujua kwamba Yeye ni Muweza wa kila kitu Ambaye macho hayawezi kumuona lakini yeye anayaona macho na wenye macho.
Aidha ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu na kwamba Muhammad SAW ni mja na Mtume Wake na aliyokuja nayo ni haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu SWT na yasiyo hayo ni batili na upotofu..."
Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu maalumu ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS kimefikia ukingoni. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu wote duniani, na hasa wafuasi wa kweli wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW, kwa mnasaba huu adhimu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.