Maadhimisho ya Siku ya Kuzaliwa Imam Mahdi AS
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS. Tunaianza makala hii fupi kwa kusema: Nuru ya umaanawi ya uwepo wa Imam Mahdi AS imeenea hata katika wakati huu wa "ghaiba" wa kutokuwepo mtukufu huyo machoni mwa walimwengu.
Miongoni mwa athari za nuru hiyo ni kwamba suala lenyewe tu la kusubiri kudhihiri kwa mwokozi huyo wa walimwengu kunafungua njia ya mustakbali bora, kufanya harakati na watu kupata nishati mpya. Itikadi hiyo huwa sababu ya kuzuia uhalifu na kutodhulumu wala kukubali kudhulumiwa katika kipindi chote cha kusubiri kudhihiri mwokozi wa ulimwengu.
Ilikuwa ni katikati ya mwezi wa Shaabani, pole pole mbingu zilikuwa zinaanza kutoa fursa ya kupuliza upepo mwanana wa alfajiri. Ilikuwa muonzi wa dhahabu wa kuchomoza jua bado haujapasua kifua cha upeo wa macho; alipozaliwa mtukufu huyo. Bila ya kukusudia, udongo wa ardhi ulianza kunukia harufu ya umaanawi. Mzizimo ulienea kila mahala. Kitoto kichanga kikaanza kuonyesha makarama yake kwa kunyoosha kidole chake cha shahada mbinguni na kusema, Alhamdulillahi Rabbil Alamin, Waswalallahu Alaa Muhammadin Waalih. Furaha na ukunjufu wa moyo ukaenea kila mahala, na mripuko wa bashasha za furaha ukamuelea mama, huku shauku ikijaa machoni mwa baba yaani Imam Hasan Askari AS ambaye alisema: Hamdu na shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Ambaye amenijaalia kuwa hai na kushuhudia kuzaliwa mrithi wangu ambaye amefanana mno na Mtume Muhammad SAW kwa sura na kwa sira kuliko watu wengine wote. Mwenyezi Mungu atamuweka nyuma ya pazia mtoto huyu na baadaye atadhihiri na kuijaza ardhi uadilifu na ustawi kama ambavyo utakuwa umejaa dhulma na ukandamizaji.
********
Imam Mahdi AS alizaliwa siku ya Ijumaa ya mwezi 15 Shaabani mwaka 255 Hijria mjini Samarra Iraq na baba yake akiwa ni Imam Hassan Askari AS. Imam Mahdi ni mjukumuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW kupitia kizazi cha masharifu na masayyid cha binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad yaani Bibi Fatimatu Zahra SA. Mama yake alikuwa Bibi mwenye heshima kubwa aliyejulikana na jina la Nargis. Imam Mahdi AS ni nyota ya 12 ya Maimamu wa Ahlul Bayt AS waliousiwa na Bwana Mtume Muhammad SAW. Ni vyema kusema pia hapa kwamba masuala mengi yanayohusiana na Imam Mahdi AS ni mambo ya ajabu ikiwa ni pamoja na namna ya kuzaliwa kwake kiasi kwamba hata athari za ujauzito wa mama yake haukuwa wa kawaida na wala hazikuonekana hadharani athari za ujauzito wake. Siri ya jambo hilo nayo iko wazi kwamba watawala wa wakati huo wa Bani Abbas walikuwa wamesoma hadhithi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW na Maimamu watoharifu kuwa Imam Hassan Askari AS angelizaa mtoto ambaye angelikuja kuvunja tawala zote za kidhalimu na kidikteta, na kuangamiza kambi zote za upotofu na ufisadi na hatimaye kuijaza ardhi uadilifu na haki. Hivyo majasusi wa watawala wa Bani Abbas wakawa wanafuatilia kwa karibu sana maisha ya watu wa nyumbani kwa Imam Askari AS kwa nia ya kuzuia kuzaliwa mtoto huyo na kama wakiona amezaliwa, wamuue mara moja. Hivyo namna ya kuchukuliwa mimba, kuzaliwa na maisha ya baadaye ya Imam Mahdi AS hayakuwa na hali za kawaida.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu alitaka Imam Mahdi azaliwe katika mazingira yanayofanana na yale ya Nabii Musa AS. Maadui wa Imam Mahdi walitumia mbinu ile ile iliyotumiwa na majasusi wa Firauni waliofanya ujasusi na njama kubwa za kutaka kumuua Nabii Musa AS akiwa bado mdogo. Hata hivyo Mwenyezi Mungu kwa uwezo Wake alimuokoa Mtume Wake huyo. Watawala wa Bani Abbas nao walitaka kuzuia kuzaliwa Imam Mahdi AS na kumuua akiwa bado mchanga. Waliwawekea ulinzi mkali - mbali na majasusi wengi - watu wa nyumba ya Imam Askari AS, lakini Mwenyezi Mungu amemlinda Imam Mahdi AS hadi leo hii.
**********
Hivi sasa miaka 1178 ya umri uliojaa baraka wa Imam Mahdi AS imepita. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake. Yumkini baadhi ya watu wakasema kuwa, jambo hilo haliwezekani. Wako baadhi ya watu wanasema kuwa, hakuna mtu anayeweza kuishi miaka yote hiyo. Lakini hilo si jambo geni katika historia ya mwanadamu. Tayari hivi sasa kuna watu kadhaa wamethibitika kuishi miaka mingi sana. Qur'ani Tukufu inathibitisha kwamba Nabii Nuh AS alifanya tablighi kwa muda wa miaka 950 na hii ni mbali na miaka mingine umri wake uliojaa baraka. Waislamu aidha tunaamini kuwa Nabii Issa AS yuko hai hadi hivi sasa kama ambavyo kuna riwaya zinazoonyesha kwamba Nabii Khidhri AS naye yuko hai hadi leo hii. Fauka ya yote ni kuwa nguvu mutlaki za Mwenyezi Mungu zina uwezo wa kufanya jambo lolote ambalo katika macho ya watu linaweza kuonekana haliwezekani. Vile vile katika upande wa kiakili na uhalisia wa mambo ni kuwa tunashuhudia jinsi Mwenyezi Mungu anavyokadiria miaka ya watu, huyu anampa umri mrefu na mwingine umri mfupi. Huyu anafariki dunia akiwa mtoto mdogo, mwengine anaishi miaka sitini au chini ya hapo na mwingine miaka 200 na zaidi, na hakuna kizuizi kwa Mwenyezi Mungu kumjaalia mja Wake kuishi umri mrefu zaidi ya huo.
Amma kitu cha kuvutia zaidi hapa ni kwamba watafiti na wataalamu hivi sasa wameelekeza jitihada zao katika kazi ya kuandaa mazingira ya kulea jeni za wanadamu ili kuwawezesha waishi umri mkubwa zaidi wa wanadamu wanaoishi leo hii. Hilo pia halikinzani hata kidogo na uwezo mutlaki wa Mwenyezi Mungu wa kwamba ni Yeye Peke Yake anayefisha na kuhuisha. Mwenyezi Mungu amemwekea njia mwanadamu, akizifuata na kujiepusha na mambo yanayopunguza umri wake, anaweza kuishi muda mrefu, tab'an hawezi kukiepuka kifo, na ndio maana leo hii takwimu za vifo vitokanavyo na maradhi kwa mfano zikawa kubwa zaidi kwa nchi maskini kuliko katika nchi zilizoendelea. Hali ni hiyo hiyo katika wastani wa umri wa watu kuishi na kufa katika nchi hizo.
Aidha tunasoma katika Qur'ani Tukufu kwenye Sura ya as Safat kuanzia aya ya 142 hadi 144 wakati Mwenyezi Mungu anapozungumzia kisa cha Nabii Yunus AS aliyemezwa na chewa kwamba: Samaki akammeza (Yunus) hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. Na laiti kama hakuwa katika wanaomtakasa Mwenyezi Mungu, Basi bila ya shaka (Yunus) angelikaa ndani ya samaki mpaka siku ya kufufuliwa.
Maana yake ni kuwa, kama Mtume huyo asingelikuwa anamtakasa Mwenyezi Mungu ndani ya tumbo la chewa, basi Mwenyezi Mungu angelimbakisha hai hadi siku ya kufufuliwa ndani ya tumbo hilo la samaki. Hivyo hakuna kizuizi chochote cha kumfanya mwanadamu aishi miaka mingi. Hata ushahidi wa kihistoria pia unaonesha kuwa, watu wa zama za maelfu ya miaka ya huko nyuma, walikuwa mashuhuri kwa kuishi muda mrefu sana. Kwa kuzingatia yote hayo tutaona kuwa, Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kumbakisha hai khalifa na Huja Wake wa mwisho duniani kwa mamia ya miaka ili isipite hata siku moja bila ya kuweko Huja wa Mwenyezi Mungu katika dunia hii.
*******
Wasikilizaji wapenzi, sambamba na kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS tunakamilisha dakika hizi chache za makala hii maalumu kwa dua ya kumuomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwa mwokozi huyo wa ulimwengu tukisema:
Ewe Mwenyezi Mungu mmiminie rehema zako Walii Wako, uliyempa majukuu ya kusimamia masuala ya waja Wako, Imam anayesubiriwa, Imam Mahdi AS. Ewe Mola wetu msheheneze baraka Zako na utufanye azizi kwa kudhihiri kwake, umsaidie; na kupitia kwake utusaidie na sisi, umpe nusura Yako kamili na nguvu za kuweza kuikomboa kirahisi dunia, na umpe kutoka Kwako cheo na nguvu. Ewe Mola wetu itie nguvu dini Yako na sunna za Mtume Wako kupitia kwake, ili kisibakie chochote katika dunia ghairi ya haki. Ewe Mwenyezi Mungu wape nguvu Waislamu na wapenda haki na uwadhilishe madhalimu na watu wa batili na utuingize peponi kwa rehema Zako. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.