Imam Hassan AS, Kigezo cha Ukarimu
Imam Hassan Mujtaba AS alikuwa mjukuu wa kwanza wa Mtume Muhammad SAW. Alikuwa mwana wa mwanamke mtakatifu, Bibi Fatima Zahra SA. Imam alikuwa dhihiriso la kivitendo la Qur’ani Tukufu na alikuwa mujahid, mwenye subira mbali na kuwa mbeba mwenge wa wote wapiganiao haki duniani.
Imam Hassan AS aliuawa shahidi katika siku kama hii na sisi hapa katika Radio Tehran tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za rambi rambi kwa mnasaba huu na tunawakaribisha kusikiliza machache tuliyowaandilia kuhusu mtukufu huyo.
Mwana Mtukufu wa Fatima SA alizaliwa tarehe 15 Ramadhani mwaka wa Tatu Hijria. Imam Hassan Mujtaba AS alipata fursa ya kulelewa katika mikono ya watu walio wabora wa viumbe vya Mwenyezi Mungu yaani Mtume SAW, Imam Ali AS na Bibi Zahra AS. Imam alilelewa katika mazingira bora ya kimaanawi na alikuwa akitayarishwa kuchukua uongozi wa Umma wa Kiislamu katika mustakabali.
Watukufu hao watatu na hasa Mtume SAW, walikuwa wakiwabainishia watu mara kwa mara kuhusu nafasi na cheo cha Imam Hassan AS. Mtume Muhammad SAW alitangaza fadhila za Imam Hassan Mujtaba AS kwa Waislamu na kuzungumzia kuhusu uhusiano wa Imamu huyo na Unabii.
Mtume SAW amenukuliwa akisema: “Kila ambaye anataka kuona Bwana wa vijana wa peponi basi amtazame Hassan AS.”
Katika sehemu nyingine Mtume SAW amesema: “Hassan ni ua lenye harufu nzuri ambalo nimelichukua duniani.”
Mtume SAW amemsifu Hassan na ndugu yake, Hussein kiasi kwamba baadhi walidhani kuwa wana hadhi ya juu zaidi kumliko baba yao, Imam Ali AS. Hali hii ilimbidi Mtume Mtukufu SAW afafanue kuhusu suala hili kwa kusema: “Hassan na Hussein wana hadhi ya juu duniani na akhera na baba yao ni aula na ana hadhi ya juu zaidi kuliko hawa wawili.”
Mmoja kati ya masahaba zake RasulullahSAW anasema: ‘Nilimuona Mtume SAW akiwa amembeba Imam Hassan AS mabegani huku akisema: “Ewe Allah! Mimi ninampenda Hassan, wewe pia mpende.”
Abu Dharal-Ghaffari mmoja kati ya masahaba zake Mtume SAW vile vile anasimulia hivi: ‘Nilimuona Rasulullah SAW akimbusu Hassan bin Ali na kusema: “Kila ambaye atawapenda kwa ikhlasi Hassan na Hussein na dhuria yao basi moto wa jahanam hautamchoma…”
Kwa hakika Mtume wa Uislamu alilenga kuwabainishia masahaba zake mtazamo wake kumhusu Imam Hassan AS na kumuarifisha kama kigezo kwa waumini. Wote walikuwa wakifahamu kuwa Bwana Mtume SAW hasemi chochote bila dalili na Qur’ani Tukufu imethibitisha hili katika Aya ya Tatu ya Surat An'aam inayosema: “Wala hatamki kwa matamanio.”
Katika kipindi chote cha maisha yake yaliyojaa baraka, Imam Hassan AS daima alikuwa akijishughulisha na kuwaongoza watu kuelekea katika njia ya haki. Muamala wake na watu wa kawaida hata maadui ulikuwa mzuri sana kiasi kwamba aliweza kuwavutia wote.
Katika historia tunasoma kuwa siku moja Imam Hassan Mujtaba AS alikuwa njiani akiwa amepanda farasi kisha mbele yake akajitokeza mtu kutoka Sham na kuanza kumtusi. Wakati alipomaliza kumtusi, Imam Hassan AS alimuelekea na kumpa salamu! Akatabasamu na kusema: "Ewe Bwana! Ninadhani wewe ni mgeni hapa. Iwapo unataka nikupe kitu nitakupa. Iwapo wewe una njaa nitakushibisha, iwapo hauna nguo nitakupa, iwapo unahitaji nitakidhi mahitaji yako, iwapo umefukuzwa sehemu nitakupa hifadhi, iwapo una haja nitakutimizia, hivi sasa njoo uwe mgeni wetu! Utakuwa mgeni wetu muda wote utakapokuwa hapa…..” Baada ya kusikia maneno hayo yaliyojaa ukarimu na mahaba kutoka kwa Imam, mtu huyo kutoka Sham alisema hivi huku akitokwa na machozi: “Nashuhudia kuwa wewe ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi na kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua zaidi sehemu ya kuweka cheo cha ukhalifa na risala. Kabla ya hapa nilikuwa na uadui mkubwa kwako na baba yako. Lakini sasa nakutambua kama kipenzi cha Mwenyezi Mungu.”
Katika mafundisho ya Uislamu, matajiri wana wajibu mzito mbele ya wanaohitaji na wasiojiweza na hivyo wanapaswa kujitahidi kukidhi mahitaji ya wasiojiweza katika jamii. Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika mawaidha yao na vitendo vyao walikuwa mfano wa kuigwa kuhusu masuala ya kuwapenda na kuwahudumia wanaadamu wenzao. Miongoni mwa hawa, Imam Hassan Mujtaba AS alikuwa na nafasi ya juu kwa mtazamo wa elimu, taqwa, fadhila na ibada. Katika suala la kuwasaidia na kuwahudumia mafukara na wasiojiweza, Imam Hassan alikuwa mashuhuri sana hadi kufika kiasi cha kupewa lakabu ya ‘Karim Ahlul Bayt’ kutokana na ukarimu wake mkubwa. Uwepo uliojaa baraka wa mtukufu huyo ni jambo ambalo lilileta utulivu kwa mafukara na wasiojiweza na kuwapa matumaini. Katika historia tunasoma kuwa, Imam Hassan AS alitoa utajiri wake wote mara mbili, na mara tatu, nusu ya utajiri huo kwa njia ya Allah SWT.
Imam Hassan AS alikuwa kimbilio la wenye masaibu, alikuwa tumaini la wasiojiweza na mtulizaji nyoyo za wenye masaibu. Hakushuhudiwa hata mara moja, fakiri akija kwa mtukufu huyo na kurejea mikono mitupu. Tunasoma katika riwaya kuwa siku moja Imam Hassan AS alikuwa akipita walipokuwa mafukara ambao walikuwa wakila mikate mikavu wakiwa wamekaa chini. Walimualika Imam ajiunge nao ili wakule chakula hicho pamoja. Mtukufu huyo alishuka kutoka farasi wake na kusema: “Allah hawapendi wenye kiburi”, kisha akaketi na kula pamoja nao na kuwaomba wote waje nyumbani kwake ili wapate kula pamoja pamoja. Hapo Imam Hassan AS aliwatayarishia chakuka kizuri na kuwapa nguo bora.
Wapenzi wasikilizaji, utawala wa miezi kadhaa na Uimamu wa miaka 10 wa Imam Hassan AS ulijiri katika kipindi cha utawala wa Muawiyya katika ardhi za Kiislamu. Utawala huo wa Muawiyya uliandamana na ukandamizaji mkubwa. Katika mazingira kama hayo ilikuwa vigumu sana kueneza mafundisho ya Kiislamu. Katika zama hizo, Imam Hassan AS alitumia tadbiri, uono wa mbali na sera za kihekima ili kuunusuru na kuuhifadhi Uislamu kutoka katika hatari ya upotofu na utawala mbovu uliokuwa ukienezwa na Muawiyya.
Awali, ili kuunusuru Uislamu na kuondoa hatari iliyokuwepo, Imam Hassan AS aliafiki suluhu na Muawiyya. Suluhu hiyo ya Imam Hassan AS ilikuwa katika msingi wa tadbiri na hekima. Katika hali maalumu ya wakati huo suluhu hiyo ilikuwa kwa maslahi ya Uislamu na jamii ya Kiislamu. Tab’an kumesemwa mengi kuhusu suluhu ya Imam Hassan AS na Muawiyaa pamoja na sababu za mtukufu huyo kukubali suluhu. Kwa hakika suluhu hiyo inaweza kutajwa kuwa ni usitishaji uhasama wa Imam Hassan AS mbele ya adui kwa lengo la kuhifadhi umoja wa jamii na thamani za Kiislamu.
Katika njia hii ya suluhu, Imam Hassan AS, kwa ujasiri mkubwa aliwastahamili watu waliokuwa na fikra finyu na mitazamo ya kufurutu mipaka na hivyo kutia saini makubaliano ya suluhu. Jambo hilo lilikuwa kielelezo cha namna Imam alivyotambua uhakika wa zama na hivyo hatua kwa hatua akaanza kuandaa mazingira ya mapinduzi ya Imam Hussein AS. Imam Hassan Mujtaba AS alitoa hotuba kuhusu suluhu hiyo. Hotuba hiyo yenyewe ni thibitisho la tadbiri yake. Sehemu ya hotuba hiyo inasema: “Nafadhilisha umoja na mshikamano wa Waislamu kuliko utengano. Kile ambacho ninaona kinawafaa ni bora zaidi ya kile mnachodhani kinawafaa. Kwa hivyo msipinge ninayowaambia….Mwenyezi Mungu SWT atusamehe sote na atuongoze katika kila ambacho kinamfurahisha.”
Uhasama wa Muawiyya dhidi ya Imam Hassan AS ni jambo ambalo lilimpelekea kughusubu nafasi yake ya ukhalifa. Jambo hilo lilipelekea Ukhalifa wa Imam Hassan AS kudumu kwa miezi sita tu.
Baada ya suluhu, Imam Hassan AS alirejea Madina kutoka Kufa na kuishi huko kwa muda wa takribani miaka 10. Akiwa na umri wa miaka 47 aliuawa shahidi kwa njama iliyotekelezwa na Muawiyya.
Imam Mohammad Baqer AS alibainisha kwa masikitiko namna babu zake watakatifu na hasa Imam Hassan Mujtaba AS walivyouawa shahidi mikononi mwa watu waovu kwa kusema: “Balaa nyingi zimetufikia kutokana na udhalimu wa Maqureishi ambao walikuwa kitu kimoja katika kutudhulumu na kutukandamiza….walimbai Kiongozi wa Waumini Ali AS na kuvunja baiya hiyo na kisha kumnyoshea upanga….hadi kumuua shahidi. Kisha wakambai mwanae yaani Imam Hassan AS. Baada ya kumbai wakapanga njama na kumkabidhi kwa adui. Watu wa Iraq walisimama dhidi yake na kumdunga kwa kisu kifuani kisha wakalivamia hema lake na kulipora kisha wakambughudhi hadi wakati wa suluhu na Muawiya…Watu elfu 20 kutoka Iraq walimbai Imam Hassan AS lakini baada ya hapo walimnyoshea upanga na kumuua shahidi.