Syria na hujuma ya vyombo vya habari vya Magharibi
Mji wa Halab au Aleppo ulioko kaskazini mwa Syria umeshuhudia matukio mengi na ya aina mbalimbali katika kipindi cha miaka elfu tatu ya umri wake. Sehemu kubwa ya mji huo mkongwe sasa imeharibiwa na kuwa magofu katika miaka minne ya vita na mashambulizi ya makundi mbalimbali ya kigaidi.
Vita na mapigano ya Syria vimeoneshwa na kuakisiwa na vyombo vya habari vya Magharibi na vya nchi za Kiarabu washirika na tegemezi kwa Wamagharibi katika sura tofauti.
Hata hivyo sambamba na kukombolewa mji huo ambao umekuwa ukidhibitiwa na makundi ya kigaidi kwa zaidi ya miaka minne iliyopita, vyombo vya habari vya nchi zinazowaunga mkono magaidi katika nchi za Syria na Iraq zimeanza kutumia timu za wataalamu kwa ajili ya kutangaza na kueneza ripoti na picha za uongo kuhusu matukio ya Syria hususan katika mji wa Aleppo. Kampeni na propaganda hiyo inafanyika kwa lengo la kutaka kuzishawishi fikra za walimwengu na kuwaambia kuwa jeshi la Syria na waitifaki wake wamefanya mauaji ya umati na jinai za kivita katika ukombozi wa eneo hilo. Ripoti za kuaminika zinasema kuwa, baadhi ya tawala za kifalme za Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi zimeanzisha vita vya kipropaganda na hujuma ya vyombo vya habari dhidi ya serikali ya Syria tena kwa kutumia bajeti kubwa ya fedha. Katika mkondo huo vyombo vya propaganda vya tawala za Kiarabu vimekuwa vikitengeneza picha, ripoti na video za kubuni na zisizo za kweli na kuzisambaza kwa mashirika ya habari ya Kimagharibi na kanali mbalimbali za televisheni. Vyombo vya propaganda vya tawala hizo za Kiarabu vimekuwa vikichochea vita vya kimadhehebu na kikaumu kwa kuonesha mara kwa mara picha ya wanawake na watoto waliouawa katika vita vya Syria na kuituhu serikali ya Syria kuwa ndiyo iliyohusika na mauaji hayo. Kazi hiyo hiyo inafanwya na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi zinazowaunga mkono na kuwasaidia makundi ya kigaidi nchini Syria kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo na kuwachafulia jina washirika wake ambao ni wapinzani wakubwa wa sera za kimabavu na kibabe za Israel.

Tunaporudi nyuma kidogo kabla ya kujadili utendaji wa sasa wa vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu na Kimagharibi, tunakumbuka jinsi vyombo vya habari kama televisheni ya Aljazeera ya Qatar, al Arabiyya inayomilikiwa na watu wa karibu na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, CNN, BBC na kadhalika vilivyoanzisha hujuma kali ya kipropaganda dhidi ya serikali ya Syria na washirika wake sambamba na kuanza maandamano mjini Damascus na kisha katika miji mingine ya mpaka wa Syria na nchi za Uturuki, Jordan na Iraq ambayo baadaye yaligeuka na kuwa vita vya silaha. Vyombo hivyo vya habari hususan Aljazeera vimekuwa vikionesha matukio ya Syria kinyume na kuakisi isivyo matukio ya vita vya nchi hiyo kwa kurusha hewani picha na mikanda ya video iliyotengenezwa kitaamu katika studio zao hususan katika studio za Doha. Vyombo vya habari kama al Arabiyya, al Hadath, BBC ya Kiingereza na Kiarabu na kadhalika na vilevile mitandao ya kijamii daima imekuwa ikitangaza na kurusha hewa picha na ripoti za vita vya Halab (Aleppo) na kutaka kuonesha kuwa jeshi la serikali ya Syria na washirika wake linafanya mauaji ya kimbari. Vyombo hivyo vya propaganda vinafanya jitihada kubwa za kuathiri fikra za walimwengu kwa lengo la kutaka kupunguza taathira na ushawishi wa jeshi na makundi ya kujitolea ya wananchi katika vita vya Syria.
Uingiliaji wa kijeshi na kisiasa wa nchi za Magharibi na washirika wao wa Kiarabu na kikanda kwa ajili ya kubadili mwelekeo wa maandamano na mamlalamiko ya watu katika nchi za Kiarabu tegemezi kwa Marekani na nchi za Magharibi katika wimbi kubwa la mwamko wa Kiislamu uliambatana na harakati kubwa ya hujuma na propaganda za vyombo vya habari.

Katika anga hiyo kulifanyika kazi ya kugawana majukumu baina ya nchi zinazoyaunga mkono makundi ya kigaidi katika nchi za Iraq na Syria. Televisheni ya Aljazeera ya Qatar kama chombo cha habari chenye nguvu kubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu na televisheni ya al Arabiyya zilipewa jukumu la kushawishi na kutia tashwishi fikra za Waarabu huku vyombo vya habari vya BBC, Voice of America na CNN, Associated Press, Reuters na kadhalika vikitekeleza majukumu kama hayo katika nchi zisizo za Kiarabu. Umuhimu wa nafasi ya televisheni ya Aljazeera katika kampeni hiyo ya kipropaganda unatokana na historia ya chombo hicho. Aljazeera ilianzishwa mwaka 1996 ikitangaza habari na matukio mbalimbali hususan ya nchi za Kiarabu na Kiislamu kwa kutumia wataalamu kutoka maeneo mbalimbali ya duniani na ikaweza kuwavutia watu wengi katika ulimwegu wa Kiarabu. Mahmoud al Muhtadi, mkuu wa zamani wa ofisi ya kulinda maslahi ya Iran nchini Misri ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya vyombo vya habari anasema: Imepita zaidi ya miaka 20 sasa tangu kuanzishwa televisheni ya Aljazeera na katika kipindi hicho chote chombo hicho kimekuwa na awamu mbili zinazotofautiana kikamilifu. Katika awamu ya kwanza- anaendelea kusema al Muhtadi- Aljazeera ilikuwa ikifanya kazi kitaalamu na kiufundi, lakini mwenendo huo ulibadilika sambamba na kuanza harakati ya mwamko wa Kiislamu na vuguvugu la mataifa ya Kiarabu la kutaka kuziondoa madarakani tawala za kidhalimu na tegemezi kwa Magharibi. Majukumu na risala mpya ya Aljazeera ni kutumia mtaji wa imani ya Waarabu kwa chombo hicho iliyopatikana katika awamu ya kwanza kwa ajili ya kuelekeza na kuongoza mirengo na matukio ya kisiasa katika ulimwengu wa Kiarabu kwa kadiri kwamba, baadhi wanaamini kuwa, ushawishi wa Aljazeera ulikuwa na taathira kubwa katika kuiondoa madarakani serikali ya Zainul Abidin bin Ali nchini Tunisia.

Utendaji wa kanali ya televisheni ya Aljazeera kuanzia mwaka 2010 hadi sasa unaweka wazi zaidi hakika na utambulisho wake. Katika miaka yake kumi ya mwanzo Aljazeera ilijidhihirisha kama chombo vya kupigania na kutetea haki za watu katika nchi za Kiarabu na kuizidishia hadhi na ushawishi wake kupitia mbinu hiyo. Baada ya hapo ilitumia mtaji huo wa imani ya watu kuingilia masuala ya siasa na kubadili mwelekeo wa harakati ya mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu.
Watu katika nchi za Kiarabu walikuwa wakitaka mageuzi katika nchi zao na viongozi wa nchi hizo waling'amua kwamba, watu wao wanaitaza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama kigezo kizuri kwa ajili ya kutimiza matakwa na malengo yao; kwa sababu hawana kigezo mbadala kwa ajili ya mageuzi makubwa na ya kimsingi. Katika upande mwingine mafanikio ya Iran baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein nchini Iraq yalizidisha uwezekano wa harakati ya kutaka mageuzi na mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu kujiunga na harakati ya wananchi wa Iran. Hapa ndipo Aljazeera ilipoingia uwanjani na kuanzisha vita vya kipopaganda dhidi ya serikali ya Syria kabla hata ya nchi hiyo kukumbwa na mgogoro wa ndani uliochochewa na nchi za Kimagharibi na washirika wao wa Kiarabu. Umuhimu wa Syria katika stratejia za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel uliifanya televisheni ya BBC itumie kanali zake za lugha mbalimbali katika kuhudumia malengo ya washirika hao wawili wa Uingereza. Kwa msingi huo BBC, Aljazeera, Al Arabiyya na kadhalika zilianza kutia chumvi na kukuza kupita kiasi maandamano ya kawaida yaliyokuwa yakifanywa dhidi ya Rais Bashar Assad na kila tukio dogo lililokuwa likitokea nchini Syria liliwekwa katika vichwa vya habari muhimu katika vyombo vya hivyo vya propaganda.
Sambamba na BBC na Aljazeera, Voice of America, CNN, Sky News, Al Arabiyya na Reuters vilitumia mbinu na tajiriba yao katika uwanja wa habari kutaka kuwaonesha walimwengu kwamba, wananchi wote wa Syria wamesimama kupinga utawala wa Rais Bashar Assad! Katika kipindi chote cha miaka 6 ya machafuko ya Syria vyombo hivyo vya habari vimekuwa vikieneza tetesi na habari za uongo kama vile madai ya kutekwa miji ya Damascus na Aleppo au tetesi kwamba Rais Bashar Assad ameuawa na kwamba familia yake imekimbilia nje ya nchi ili kuzichochea fikra za watu.

Propaganda hizo zilishika kasi na mwelekeo mpana zaidi baada ya Russia kutuma majeshi yake nchini Syria kulisaidia jeshi la nchi hiyo kupambana na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi na za Kiarabu. Kanali ya televisheni ya BBC ilikuwa ukificha habari za kushindwa na kurudishwa nyuma mkundi ya kigaidi kwa kutoa ripoti zisizo za kweli kuhusu madai ya kuuawa raia katika mashambulizi ya anga yanayofanywa na Russia na jeshi la Syria. Chombo hicho chenye mfungamano mkubwa na siasa za serikali ya Uingereza kimekuwa kikikuza na kutia chumvi kuhusu nafasi ya Iran, makundi ya wapiganaji wa kujitolea na wapiganaji wa Hizbullah ya Lebanon nchini Syria na kuweka alama ya kuuliza kuhusu uwezo wa jeshi la taifa la nchi hiyo. BBC na washirika wake pia wamekuwa wakizusha makelele mengi na kutoa madai ya kupelekwa Syia wapiganaji wa kigeni kwenda kuisaidia serikali ya nchi hiyo, na wakati huo huo vinafumbia macho wimbi kubwa na magaidi wanaotolewa katika nchi mbalimbali hata za Ulaya na Marekani kwenda kupigana dhidi ya serikali ya Damascus. Vyombo hivyo pia vimekuwa vikipuuza na kunyamazia kimya mauaji ya raia yaliyofanywa na magaidi kwa kutumia silaha za kemikali katika nchi za Syria na Iraq.
Alaa kulli hal, vyombo vya habari vya nchi zinazoyaunga mkono makundi ya kigaidi vimeweza kwa kiasi fulani kubadili mwelekeo wa vita nchini Syria kwa kutangaza habari na ripoti za kichochezi na za uongo kuhusu vita hivyo katika mwaka uliopita wa 2016. Hata hivyo mapambano ya jeshi la Syria na waitifaki wake yamezuia njama hiyo na kuifanya igonge mwamba.
Wataalamu wa masuala ya vyombo vya habari wanasema: Tangu mwaka 2011 kanali za televisheni za nchi za Magharibi na za Kiarabu ziliungana kwa sura ya kustaabisha kwa ajili ya kukabiliana na serikali ya Syria. Wataalamu hao wanaashiria muungano wa kanali za televisheni za BBC, Sky News, Aljazeera ya Qatar na al Arabiyyah ya Saudi Arabia na kusema: Kwa mara ya kwanza duniani kumeshuhudiwa ushirikiano wa kihabari baina ya vyombo vya habai vya Kimagharibi, Kiarabu na Kiebrania yaani vyombo vya habari vyenye uhusiano na Israel.

Muungano na ushirikiano mkubwa wa kanali hizo za televisheni zinazokwenda kinyume na matakwa ya mataifa ya Mashariki ya Kati ulifikia kiwango cha mtangazaji mashuhuri na mwenye mikasa mingi wa Aljazeera, Faisal Qasim kueleza waziwazi wasiwasi wake kuhusu mashambulizi makali ya jeshi la Syria dhidi ya makundi ya kigaidi katika mji wa Aleppo. Wakati huo Faisal Qasim aliyataka makundi ya wapiganaji yaliyokuwa eneo la Dar'a kuharakia kuwasaidia magaidi waliokuwa wakishambuliwa vikali na jeshi la Syria katika mji wa Aleppo! Mbali na hayo Mkurugenzi Mkuu wa BBC, Tony Hall alikataa wito wa Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza, David Cameroon na wabunge 120 wa nchi hiyo walioitaka televisheni hiyo kuacha kutumia istilahi ya "Dola la Kiislamu" kama jina la kundi la kigaidi la Daesh kwa ajili eti ya kulinda msingi wa kutopendelea upande wowote!!
Haya yote yanaonesha kuwa, wakati nchi kama Saudi Arabia, Qatar, Imarati na Uturuki zikitoa misaada ya kifedha na silaha za aina mbalimbali kwa makundi ya kigaidi, vyombo vya habari na propaganda vya nchi hizo pia vikishirikiana na vya mabwana zao wa Kimagharibi vimekuwa vikifanya hujuma na mashambulizi makubwa ya kipopaganda na kisaikolojia dhidi ya jeshi na watu wa Syria na Iraq na mashambulizi hayo yangali yanaendeleo.