Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hassan al Askari AS
(last modified Wed, 07 Dec 2016 09:15:50 GMT )
Dec 07, 2016 09:15 UTC
  • Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hassan al Askari AS

Kwa mara nyingine leo tunakumbuka tukio la kuuawa shahadi mmoja wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW naye si mwingine isipokuwa ni Imam Hassan Askari AS. Siku kama ya leo mwaka 260 Hijiria, ulimwengu ulipatwa na huzuni ya kuondokewa na Imam Hassan Askari AS, ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW.

Maisha mafupi ya Imam Hassan AS yaliyoendelea kwa kipindi cha miaka 28 yalijaza kurasa za vitabu vya historia. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka ya tukio hili la kuuawa shahidi mtukufu huyo. Kwa mnasaba huo, leo wapenzi wasikilizaji tutasimulia sehemu ndogo ya maisha ya mtukufu huyo. Endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Maisha ya Maimamu na Ahlul-Bayti wa Mtume SAW, yamejaa maarifa na mafunzo kwa ajili ya kumlea mtu na jamii kwa ujumla. Hata hivyo utawala wa kitwaghuti, kidhalimu na halikadhalika kuwepo vizingiti vingi, kulitatiza harakati na shughuli za Ahlul Bayt AS kwa ajili ya kueneza mafundisho asili ya dini Tukufu ya Kiislamu.

Vizingiti hivyo vilishamiri sana katika kipindi cha Imam Jawad na Imam Ali al Hadi AS na kushtadi zaidi wakati wa kipindi cha Imam Hassan Askari AS. Watawala wa wakati huo wa Bani Abbas, walimlazimisha Imam Ali al Hadi na mwanawe Imam Hassan aliyekuwa na umri wa miaka minne wakati huo, kuuhama mji wa babu yao, Mtume Muhammad SAW wa Madina na kuelekea mjini Baghdad, Iraq ambako kulikuwa makao makuu ya watawala hao.

Baada ya kufariki dunia Imam Hadi AS Imam Hassan Askari AS alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu huku akiwa na umri wa miaka sita tu. Katika mazingira hayo magumu, mtukufu huyo aliweza kufikisha ujumbe wa mafundisho ya Kiislamu katika nyanja tofauti zikiwemo za kisiasa na kijamii kwa wanafunzi wake. Hata hivyo vikwazo na vizingiti vya aina mbalimbali vilivyowekwa na watalawa wa Bani Abbas, havikuweza kuzuia upendo wa watu kwa Imam Askari AS. Hali hiyo inaonyesha kuwa, nuru ya Mtume Muhammad SAW na Ahlul-Bayti wake AS, ni nuru ya haki ambayo kamwe haiwezi kuzimwa.

Image Caption

 

Kipindi cha Imam Hassan Askari AS kilikuwa kipindi chenye misukosuko mikubwa zaidi cha watawala wa Bani Abbas. Uongozi usiofaa, migogoro ya ndani ya utawala, upinzani wa wananchi, harakati za mara kwa mara dhidi ya watawala na kuenea mafundisho potofu, ni miongoni mwa sababu za machafuko ya kisiasa na kijamii ya kipindi hicho.

Viongozi walikuwa wakiwanyonya raia, huku wakijenga makasri na majumba makubwa ya kifahari na kuwaacha watu wa kawaida katika hali ngumu ya kimaisha. Viongozi hao madhalimu hawakujali umasikini na tabu za raia bali waliendelea kujineemesha katika utawala. Waislamu walikuwa wanatambua kuwa Imam Hassan Askari ndiye atakayezaa mtoto anayesubiriwa kuja kuijaza dunia haki na uadilifu baada ya kuenea dhulma na uonevu.

Hali hiyo, ilizidisha vizingiti na ukandamizaji wa watawala dhidi ya Imam kiasi kwamba, ilimlazimu mtukufu huyo chini ya mpango ulioandaliwa na utawala, kuripoti katika siku maalumu za wiki katika ofisi za watawala wa wakati huo.

Hata hivyo na licha ya kuweko njama kubwa za watawala hao, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mapenzi na utukufu Wake, aliamua mtoto wa Imam Askari, yaani Imam Mahdi AS ambaye ni mwokozi wa ulimwengu, azaliwe salama usalimini. Baada ya kuzaliwa Imam Mahdi AS, Imam Hassan alianza kuiandaa jamii ya wakati huo kukabiliana na hali ngumu itakayoikabili jamii ya baadaye.

Kila alipokuwa akipata fursa, Imam Hassan alikuwa akitumia fursa hiyo kuzungumzia hali ya baadaye atakayokuwa nayo Imam Mahdi AS yaani ya ghaiba kutoweka mbele ya macho ya watu pamoja na taathira chanya za uongozi wa mwanawe Imam Mahdi AS kwa walimwengu. Mtukufu huyo alisisitiza kuwa, uadilifu na usawa vitaenea ulimwenguni kupitia kwa mwanawe huyo.

Katika kipindi ambacho kilikuwa kimetanda giza la fikra potofu na aina kwa aina za uzushi, Imam Hassan AS alifanya juhudi kubwa za kubainisha uhakika na uhalisia wa dini tukufu ya Kiislamu kwa watu. Imam alikuwa akiwanywesha elimu Waislamu waliokuwa na kiu ya kutaka kuelimika kutoka katika chemchem ya maarifa ya Ahlul Bayt AS.

Dalili madhubuti za kielimu zilizokuwa zikitolewa na Imam zilikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba, hata Ya’aqub bin Is’haqa al Kindi, mtaalamu mkubwa wa falsafa wa wakati huo, aliweza kufahamu ukweli baada ya kujadiliana kielimu na mtukufu huyo na mwishowe akaamua kuchoma kitabu chake alichokuwa amekiandika hapo kabla kukosoa baadhi ya mafundisho ya dini Tukufu ya Kiislamu.

Image Caption

 

Licha ya kwamba, utawala wa Bani Abbas ulikuwa na ugomvi na Imam Askari AS, lakini mmoja wa mawaziri wa utawala huo aliyejulikana kwa jina la Ahmad bin Khaqan, alikiri juu ya fadhila na utukufu aliokuwa nao Imam Hassan Askari kwa kusema kama ninavyonukuu: “Sijaona mtu mithili ya Hassan bin Ali mjini Samarra, Iraq. Hakukuwepo mtu mwenye sifa kama zake katika uchaji-Mungu, utakasifu na utukufu kati ya watu wote. Licha ya kwamba, alikuwa kijana, lakini watu wa kabila la Bani Hashim walikuwa wakimtanguliza mbele ya watu wote. Alikuwa na nafasi kubwa kiasi cha kupendwa na rafiki na adui.” Mwisho wa kunukuu.

Utukufu wote huo Imam aliupata kutokana na unyenyekevu wake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kushikamana kwake na haki. Naye mtukufu huyo anasema: “Hakuna mtu mtukufu aliyetengana na haki ispokuwa alidhalilika na hakuna mtu duni na mdogo aliyefungamana na haki, ispokuwa atatukuzwa.”

Kile ambacho kilikuwa kikiwasaidia Ahlul-Bayt wa Mtume SAW akiwemo Imam Hassan AS, katika njia ya kuvumilia matatizo na kuwafanya kuwa thabiti katika njia ya haki, ni kushikamana na kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hii ni kwa sababu ibada na mapenzi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu - mambo ambayo wanadamu wameumbwa nayo katika maumbile yao - yanawatia nguvu kubwa watu hao za kuweza kuvumilia tabu na matatizo.

Kwa kufikia kilele cha uchaji-Mungu, watu watakatifu wanakuwa wamejinasua na minyonyoro ya ndani na nje na hivyo kufikia nafasi ya utukufu na akhlaqi. Mtume na Ahlul-Bayt wake ndio watu wa kwanza walioweza kufikia kilele hicho cha ucha-Mungu.

Watukufu hao hawakushindwa hata kidogo katika mapambano yao dhidi ya shirki, ukafiri, kupenda vitu vya kidunia, viongozi waovu na madhalimu, kutokana na kufikia daraja ya unyenyekevu wao mbele ya uwezo wa Mwenyezi Mungu wa Milele.

Imepokewa katika hadithi tukufu kuwa, wakati Imam Hassan Askari AS alipokuweko gerezani, alikuwa akijishughulisha muda wote na ibada, kumkumbuka Mola wake na kumwelekea Yeye, kiasi cha kumuathiri askari aliyekuwa amewekwa kwa ajili ya kutoa adhabu na mateso kwa wafungwa. Siku moja maafisa wa utawala wa Bani Abbas walienda kumtembelea mlinzi wa jela aliyokuwa amefungwa Imam Hassan Askari AS.

Mlinzi huyo alijulikana kwa jina la Swaleh bin Waswif na kumtaka awe mkali na mgumu dhidi ya Abu Muhammad na kamwe asimpe utulivu hata kidogo mtukufu huyo. Mlinzi huyo aliwajibu maafisa hao wa Bani Abbas akiwaambia: Mnanitaka nifanye nini tena? Kwani humjasikia kuwa nimewapeleka askari wawili wakali zaidi kwenda kumtesa Abu Muhammad lakini kinyume na nilivyotarajia, watu hao wameathirwa sana na Abu Muhammad yaani Imam Hassan Askari-AS na baada ya hapo si tu kwamba hawakumtazama kama mfungwa, bali waligeuka na kuwa ni watu wa kufanya ibada na kufunga na hivyo imani yao ikaimarika zaidi, hapo maafisa wale wa utawala wa Bani Abbas walitaka wale askari wawili waletwe mbele yao na wasailiwe, walipofika wakawaambia:

Ole wenu! Nini kimetokea mpaka mmeshindwa kumuadhibu mtu huyu yaani Imam Hassan, wale askari wakajibu kwa kusema: Mlitarajia tuseme nini mbele ya mtu ambaye mchana kutwa hufunga na usiku kucha hukesha katika kufanya bada? Mtu ambaye hajishughulishi na jambo jingine ghairi ya kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wakati alipokuwa akitutazama, tulikuwa tukiona haiba na utukufu wake.” Mwisho wa kunukuu.

 

Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mu’utamad, mtawala dhalimu wa Bani Abbas wa wakati huo akafanya njama ambazo zingeweza kumuua shahidi Imam. Haukupita muda ispokuwa kiongozi huyo akamuwekea sumu ambayo ilimuua mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW baada ya kuugua kwa siku kadhaa. Mtumishi wa mtukufu huyo amenukuliwa akisema kuwa: Wakati Imam alipokuwa amelazwa akiwa mgonjwa katika hatua za mwisho wa maisha yake, alifahamu kuwa muda wa Salatus Sub’h umewadia. Hapo alisema: “Ninataka kusali.” Kisha nikamuandalia msala kitandani pake. Imam akatawadha na akasali Salatus Sub’h iliyokuwa sala yake ya mwisho katika kitanda chake na kisha akaaga dunia.” Innaa Lillaahi Wainnaa Ilayhi Raajiuna.

Akielezea nafasi ya Maimamu na Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Askari AS amenukuliwa akisema: Sisi tumeweza kufikia vilele vya juu kabisa vya uhakika kutokana na kuweko kwetu Unabii na Wilaya...

Mtukufu huyo alikuwa analihesabu suala la kuzidisha welewa na muono wa mbali wa watu kuwa ni jambo muhimu mno. Katika moja ya hadithi zake amenukuliwa akisema: Ibada si kufunga saumu sana na wala kusali sana tu, bali ibada ya kweli ni kuzidisha kumkubuka Allah (kwa dhati na kwa wakati wote). Vile vile amesema katika hadithi nyingine kwamba: Sura ya wema ni ujamali wa dhahiri na akili na tafakuri ya wema ni ujamali wa batini. Kwa mara nyingine tena Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inatoa mkono wa pole kwenu nyinyi nyote kwa mnasaba wa kukumbuka siku alipouawa shahidi Imam Hassan Askari AS mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags