Umoja katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA) na Ayatullah Khamenei
Uislamu umeufanya umoja kuwa jambo la wajibu na lazima miongoni mwa Waislamu na waumini na dini nyinginezo za mbinguni zinazomwamini Mwenyezi Mungu Mmoja. Uzito wa jambo hili unaonekana wazi katika aya za Qur'ani Tukufu na riwaya zilizopokelewa kutoka kwa Maimamu Maasumu (as). Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 103 ya Surat Aal Imran kitabu hicho kitakatifu: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuw
Historia ya Kiislamu inaonyesha wazi kuwa kila mara Waislamu wa
madhehebu tofauti wanapochukua uamuzi wa kuungana na kushirikiana katika
ngome moja dhidi ya audui, jamii ya Kiislamu huwa ni tukufu na yenye
nguvu na maadui kuwa dhaifu, lakini Waislamu wanapoghafilika na kusahau
amri hiyo muhimu ya Mwenyezi Mungu, hukabiliwa na misiba mingi ukiwemo
wa kudhibitiwa na maadui na kuhatarishwa kizazi na jamii nzima ya
Kiislamu. Qur'ani Tukufu inasema katika aya ya 46 ya Surat al- Anfaal:
Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga,
na zikapotea nguvu zenu.
Katika karne hii, Mapinduzi ya Kiislamu ya
Iran ni mfano bora wa dhihirisho la nguvu ya Umma wa Kiislamu ambayo
imepatikana kutokana na imani na umoja wa wananchi. Wananchi hao
waliokuwa mikono mitupu lakini waliokuwa na nyoyo zilizojaa imani ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu, walisimama imara mbele ya utawala wa kitaghuti
wa Shah uliokuwa umehijami vilivyo kwa kila aina ya silaha za kisasa na
kupata uungaji mkono wa kila upande kutoka kwa madola ya kibeberu na
kiistikbari ya Magharibi. Hatimaye wananchi walijipatia ushindi wa
kishindo kutokana na mshikamano na ushirikiano wao imara kwa ajili ya
kuung'oa mzizi wa upotovu nchini.
Iran ni nchi ambayo ina madhehebu
na makabila mengi. Hata kama Mashia ndio walio wengi nchini, lakini
Masunni pia wanaunda asilimia kubwa ya Waislamu wa nchi hii. Mbali na
madhehebu haya mawili kuna wafuasi wa dini nyinginezo kama vile Mayahudi
na Wakristo. Jambo la kuvutia hapa ni kwamba licha ya kuwepo tofauti
hizi zote za kimadhehebu, kidini, na kikabila lakini wananchi wote wa
Iran katika vipindi vyote vya mapambano dhidi ya uistikabari walisimama
pamoja na kushirikiana bega kwa bega dhidi ya utawala dhalimu wa Shah
huku wakitambuana kama ndugu. Hivi sasa pia kutokana na misingi muhimu
ya utamaduni wa umoja iliyoandaliwa nchini na Imam Khomeini (MA),
wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali wanaishi pamoja kwa amani,
ushirikiano na udugu. Katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya miaka
minane vya Iraq dhidi ya Iran, Masuni walipigana bega kwa began na
wenzao Mashia dhidi ya utawala huo wa Kibaathi na kutoa mashahidi wengi
kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Wakristo na Wakalimi wa Iran pia
walishiriki vilivyo katika medani ya vita na kufuatilia kwa uwezo wao
wote malengo ya Jamhuri ya Kiislamu na kuuawa shahidi kwenye njia hiyo.
Kutokana
na uongozi shupavu na wa busara wa Imam Khomeini (MA), Mapinduzi ya
Kiislamu ya Iran yameweza kudhihirisha muujiza wa umoja katika karne
hii. Kwa kufuata kikamilifu miongozo ya Qur'ani Tukufu ambayo inawataka
Waislamu kuwa na umoja na pia kuungana na wafuasi wa dini nyinginezo
zinazompwekesha Mwenyezi Mungu, Imam Khomeini (MA) alitoa wito wa kuwepo
umoja miongoni mwa madhehebu zote za Kiislamu na hata wafuasi wa dini
nyingine, kushirikiana kwa pamoja chini ya kivuli cha Mapinduzi ya
Kiislamu. Ni wazi kuwa umoja hapa hauna maana ya wafuasi wa madhehebu na
dini tofauti kuacha imani zao na kufuata itikadi moja lakini una maana
ya kwamba licha ya kuwepo tofauti za kiimani na kiitikadi lakini wote
wanapasa kuimarisha umoja na kushirikiana kwa msingi wa kuheshimiana na
kuzingatia udugu baina yao. Tofauti zilizopo zinapaswa kuchunguzwa na
kujadiliwa si kwa njia za kawaida na za kijuu juu tu bali kwa mbinu za
kielimu, kitaalamu na katika mazingira yaliyo mbali na dharau, matusi na
kukufurishana ili ukweli wa mambo upate kufahamika.
Kwa kuwa na
mtazamo wa kina na mwamko wa kupigiwa mfano na katika hali ambayo
ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa umedhoofishwa pakubwa na hitilafu za
kikabila na kimadhehebu, Imam Khomeini (MA) alifanikiwa kulifahamisha
taifa la Iran udharura wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu na hivyo
kuzuia kutokea mgawanyiko katika jamii hii ya kimapinduzi, kupitia
hotuba zake za hamasa na mwamko. Alisema: 'Leo ni siku ambayo makundi
yote ya Kiislamu yamesimama mkabala na nguvu za kishetani ambazo
zinataka kufuta msingi wa Uislamu, nguvu ambazo zimetambua kwamba kitu
ambacho ni hatari kwao ni Uislamu na umoja wa mataifa ya Kiislamu. Leo
ni siku ambayo Waislamu wa nchi zote za dunia wanapasa kushikamana.'
Imam Khomeini (MA) alikuwa akisema: 'Katika Uislamu, lugha, kabila na
sehemu havitambuliki (havipewi umuhimu). Waislamu wote, wawe ni Masuni
au Mashia, ni ndugu na wote ni sawa, na wote wananufaika na fursa na
haki za Kiislamu. Usuni na Ushia haujadiliwi kwenye Uislamu wala Mkurdi
na Mfursi, wote ni ndugu."
Si taifa la Iran tu, bali Imam Khomeini
aliwataka Waislamu wa mataifa yote bali wanyonge wote wa ulimwengu bila
kujali dini zao kuwa na umoja mbele ya uistikbari wa dunia. Hata hivyo
alitilia mkazo sana umoja baina ya Shia na Suni katika nchi za Kiislamu.
Aliamini kuwa jambo lililowadhoofisha Waislamu wengi na kuwafanya
wadhalilishwe duniani ni mfarakano ulio baina yao. Alikuwa akisema:
'Hitilafu zinazoletwa nchini Iraq, Iran na nchi nyigine za Kiislamu
zinapasa kutiliwa maanani na viongozi wa serikali za Kiislamu na
kutambua kwamba hitilafu hizo zitafuta nguzo yao. Wanapasa kutambua kwa
kutumia akili na busara kwamba wanataka kuufuta Uislamu kwa kisingizio
cha madhehebu na Uislamu. Mikono miovu ambayo inazua hitilafu miongoni
mwa Mashia na Masuni katika nchi hizi sio Mashia wala Masuni halisi. Hii
ni mikono ya wakoloni ambayo inataka kudhibiti nchi za Kiislamu kupora
utajiri wao na kuanzisha masoko ya magendo katika nchi zinazotajwa kuwa
zimeendelea.'
Tokea mwanzoni, Mapinduzi ya Kiislamu yamewanyooshea
Waislamu na wapwekeshaji wote wa Mwenyezi Mungu mkono wa udugu na
urafiki. Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alikuwa akisema:
Sisi na Waislamu wa Ahlu Sunna ni ndugu. Ikiwa mtu atatamka maneno
ambayo yatachochea mfarakano na tofauti kati ya Waislamu, basi jueni ya
kuwa mtu huyo atakuwa ima ni jahili au ni miongoni mwa watu wanaotaka
kuleta hitilafu miongoni mwa Waislamu. Hapa hakuna kabisa suala la Ushia
wala Usuni bali sisi sote ni ndugu.' Fikra ya umoja ilibadilika na kuwa
stratijia muhimu katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambapo uhusiano
wake na nchi nyingine za Kiislamu ulisimama na ungali unasimama juu ya
msingi huu wa udugu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitofautishi kati ya
Shia na Suni katika kutetea Uislamu na Waislamu wanaodhulumiwa katika
sehemu yoyote ile ya dunia na kama ambavyo inatetea kwa maneno na
vitendo Mashia wa Lebanon ndivyo hivyohivyo inavyotetea na kuwaunga
mkono Waislamu wa Kisuni wa Palestina wanaodhulumiwa na kukandamizwa na
utawala ghasibu wa Israel. Katika miongo minne iliyopita tokea ijipatie
ushindi, Jamhuriya Kiislamu ya Iran imethibitisha wazi kwamba inaamini
na kuzingatia umoja miongoni mwa Waislamu kuwa msingi muhimu kwa ajili
ya kuimarisha nafasi ya Uislamu ulimwenguni.
Ayatullah Ali Khamenei,
ambaye alichukua nafasi ya kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada
ya kuaga dunia Imam Khomeni pia husisitiza mara kwa mara juu ya umuhimu
wa kuimarishwa umoja wa Waislamu na kuainisha siasa kuu za mfumo wa
Kiislamu wa Iran lwa msingi huo. Anasema katika moja ya hotuba zake
ambapo anaashiria moja ya manufaa wanayoyapata maadui wa Uislamu
kutokana na mfarakano wa Waislamu kwa kusema: 'Kuna watu bilioni moja
duniani ambao wana imani moja kuhusu Mwenyezi Mungu, Mtume Mtukufu
(saw), Swala, Hija, Al-Kaaba, Qur'ani Tukufu na mambo mengine mengi
katika dini na kuhitilafiana katika baadhi ya mambo. Je, ni mantiki kwa
watu kama hawa kutumia hitilafu hizi chache kwa lengo la kuanzisha vita
baina yao na hivyo kuwapa watu wasiomwamini kabisa Mwenyezi Mungu, Mtume
(saw), dini na mambo mengine yote ya msingi fursa ya kuuhujumu Uislamu
na Waislamu? Anasema katika sehemu nyingine: 'Moja ya maamrisho ya
Qur'ani ni kumtaka kila mtu katika Umma wa Kiislamu kuzingatia umoja na
kushirikiana na wenzake. Mwenyezi Mungu anasema shikamaneni na kamba
yake na wala msifarakiane. Ni nani wanaokusudiwa kwenye maneno haya?
Maneno haya yanatuhusu sisi, ni maneno yanayolihusu taifa la Iran, nchi
na mataifa ya Kiislamu na ni maneno yanayowahusu waumini wote wa dini ya
Kiislamu kote duniani. Je, tunafanya kama tulivyoamrishwa? Nukta iliyo
kinyume cha mafundisho haya ya Qur'ani ni mafundisho ya kikoloni yaani
ya kuleta na kuzua hitilafu kati ya Waislamu, ili kundi moja
lilikufurishe jingine, kulaani na kujitenga na jingine. Hili ndilo jambo
linalofuatiliwa na ukoloni hii leo ili tusiwe pamoja.'
Ulimwengu wa
Kiislamu hii leo unahitaji kuwa na umoja kuliko wakati mwingine wowote.
Mfarakano na utakfiri ni balaa kubwa linalowakabili Waislamu ambao wote
wanaswali kuelekea kibla kimoja, wana kitabu kimoja cha mbinguni,
wanamwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja na wote wanampenda Mtume wa Mwisho. Leo
maadui wa Uislamu wanapiga ngoma ya kuwatenganisha Waislamu kwa nguvu
kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote na kuota ndoto ya kuzidhibiti
nchi za Kiislamu. Katika hali kama hiyo umoja wa Kiislamu ni dawa
mujarabu ambayo Mwenyezi Mungu amewataka waja wake wema waitumie.
Kuitikia wito huo wa Mwenyezi Mungu bila shaka kutafungua njia ya saada
na utukufu kwa Waislamu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.