Magaidi 20 wa kundi la al-Shabab waangamizwa katikati ya Somalia
Viongozi wa Somalia wametangaza kuwa, magaidi 20 wa kundi la wanamgambo wa al-Shabab wameuawa na vikosi vya serikali katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Ripoti zaidi zinasema kuwa, operesheni kubwa ya kijeshii iliyofanywa na vikosi vya nchi hiyo katika mji wa Galgaduud ulioko katikati mwa nchi hiyo imepelekea kuangamizwa magaidi 18 wa kundi hilo la al-Shabab wakiwemo makamanda wake kadhaa wa kundi hilo.
Taarifa ya maafisa usalama wa Somalia inaeleza kuwa, ngome kadhaa za wanamgambo hao wenye misimamo ya kufurutu ada zimeangamizwa katika operesheni hiyo kikiwemo kituo kimoja cha kutengeneza mabomu.
Kundi la kigaidi la al Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya kila liwezalo kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007; na hadi kufikia sasa kundi hilo limefanya mashambulizi mengi ya kigaidi na kuuwa wanajeshi na raia wengi.
Vikosi vya serikali vimeimarisha operesheni dhidi ya magaidi wa al-Shabab katika mikoa ya kusini, lakini wanamgambo hao bado wanadhibiti maeneo ya vijijini ya mikoa hiyo na huwa wanafanya mashambulizi ya kuvizia na kutega mabomu ya ardhini.
Tangu alipoingia madarakani mwezi Mei, 2022, Rais Hassan Sheikh Mohamud ametangaza vita vya kila namna dhidi ya al Shabab, ambalo lenyewe limejitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaida.