Waislamu wa Ghana wawataka walimwengu kupinga uchomaji Qur'ani barani Ulaya
Waislamu wa Ghana wametoa wito wa kufanyika maandamano ya kimataifa ya kulaani uchomaji wa Qur'ani wakati huu wa maombolezo ya Muharram.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iranpress, jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Ghana imefanya maandamano makubwa ikilaani kuvunjiwa heshima na kuchomwa moto kwa makusudi nakala za Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark. Waislamu wa Ghana walikuwa wameshika Qur'ani Tukufu mikononi mwao na kuiweka juu ya vichwa vyao kama ishara ya heshima kwa kitabu hicho kitakatifu.
Imam Saeed Sandow ambaye amezungumza na ripota wa Iranpress mjini Accra amelaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden na kusema kuwa, kitendo hicho ni cha kichochezi, kisichokubalika na kisicho na mantiki.
Mwanafikra huyo wa Ghana amesisitiza kwamba, kuvunjiwa heshima kitabu chochote kitakatifu kwa kisingizio cha uhuru wa kusema ni jambo la kulaumiwa, na kunaibua hisia za uhasama wa kidini; hivyo maadili ya Kiislamu hayapaswi kuchezewa shere.

Imam Saeed Sandow ameitaja Qur'ani Tukufu kuwa ni mstari mwekundu wa kila Muislamu ambao haupaswi kuvukwa, na kusisitiza kuwa, nchi mbalimbali na taasisi maarufu zinapaswa kususia bidhaa za Sweden ili kukabiliana na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.
Hivi karibuni mkazi wa Sweden aliyejulikana kwa jina la Salwan Momika aliivunjia heshima Qur'ani Tukufu mara mbili kwa idhini na himaya ya serikali ya nchi hiyo na kukichoma moto kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu zaidi ya bilioni mbili mbele ya kamera wa waandishi wa habari, jambo ambalo limeibua hasira za Waislamu duniani kote.