Watoto milioni 3 katika hatari ya kufa njaa Sudan Kusini
Maafisa wa serikali ya Sudan Kusini wamesema mamilioni ya watoto nchini humo wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na mgogoro wa njaa unaolikabili taifa hilo changa zaidi barani Afrika.
Esther Ikere Ladu, Katibu Msaidizi wa Wizara ya Jinsia, Watoto na Masuala ya Jamii wa Sudan Kusini amesema watoto milioni 3.1 wanahitaji msaada wa dharura kutokana na baa la njaa linaloisakama nchi hiyo.
Ladu amesema, "Kinachowasukuma watoto kuingia mitaani ni ukosefu wa chakula na mizozo ya kinyumbani. Wakati wa migogoro (nchini Sudan Kusini), baadhi ya wanawake wanaachwa wajane na wengine wanaolewa tena, na huenda mazingira ya nyumbani yasiwe mazuri kwa watoto hao."
Naye Obia Achieng, Naibu Mwakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF nchini Sudan Kusini amesema watoto ni wahanga wa migogoro kadhaa inayoikabili nchi hiyo ya Kiafrika.
 
Kwa upande wake, Mohamed Kamal, Mkurugenzi wa shirika la misaada ya kibinadamu la Plan International nchini Sudan Kusini amesema kuna haja kwa sekta zote kushirikiana ili kuwadhamininia watoto usalama wao ukiwemo usalama wa chakula.
Amefichua kuwa, watoto milioni 3.3 nchini humo wanaishi katika familia ambazo hazina uwezo endelevu wa kuwanunulia watoto wao chakula; na kwamba watoto wengine milioni 2.8 hawaendi shule kutokana na mgogoro wa chakula.
 
							 
						 
						