Balozi wa zamani: Mapinduzi ya Niger yanatokana na watu kukataa 'uwepo wa Ufaransa'
Mwanadiplomasia wa zamani wa Ufaransa anasema mapinduzi ya kijeshi Niger yanatokana na wananchi kuchoshwa na uingiliaji wa Ufaransa na kukataa kwao uwepo wa dola hilo la Ulaya nchini humo.
Gérard Araud, balozi wa zamani wa Ufaransa nchini Marekani, Umoja wa Mataifa na katika utawala haramu wa Israel, amesema katika mahojiano na EURACTIV kwamba mgogoro wa sasa nchini Niger ni "kukataliwa kwa uwepo wa Wafaransa nchini humo.
Amesema watu wa Nigeria wanapinga ukoloni mambo-leo wa Ufaransa barani Afrika ambao unajulikana kama "Françafrique".
Araud amesema: "Tunashuhudia uasi wa vijana" dhidi ya Ufaransa na serikali zao za kitaifa, ambazo zinaonekana kuwa vibaraka wa Ufaransa katika eneo hilo."
Jenerali Abdourahamane Tchiani, mkuu wa zamani wa walinzi wa rais wa Niger, alimpindua rais Mohamed Bazoum katika mapinduzi ya Julai 26 na kujitangaza kuwa kiongozi wa nchi hiyo ya Sahel, siku chache baadaye.
Rais aliyepinduliwa anazuiliwa na wanajeshi katika ikulu ya rais katika mji mkuu Niamey.
Mapinduzi ya Niger, ambayo ni ya hivi punde zaidi katika mfululizo wa mashambulizi ya kijeshi huko Afrika Magharibi, ni pigo jingine kwa mkakati wa kijeshi wa Ufaransa katika eneo la Sahel.

Ufaransa ilikuwa dola la kikoloni katika Afrika Magharibi hadi 1960. Tangu uhuru, Ufaransa hata hivyo imedumisha ushawishi kibiashara na uwepo wa kijeshi katika eneo hilo.
Ufaransa ina wanajeshi 1,500 nchini Niger. Wanajeshi wa Marekani na wa nchi zingine Ulaya pia wanaendelea kubakia nchini Niger.
Kulingana na Araud, kufungwa kambi za jeshi la Ufaransa nchini Niger kumecheleweshwa kwa muda mrefu. Amesema, "Kuwa na vituo vya kijeshi ni ishara ya kutaka kuingilia masuala ya Afrika."
"Niger kwa Ufaransa ni kama Afghanistan ilivyo kwa Marekani", mwanadiplomasia huyo wa zamani amesema, akibainisha kuwa ni wakati muafaka kwa Ufaransa kuwachukulia wenzao wa Afrika kama mataifa huru.
Amesisitiza kuwa, Ufaransa haina tena jukumu lolote "lenye maana" katika eneo hilo.