Mapigano ya utumiaji silaha yaanza tena katika mji mkuu wa Libya, Tripoli
(last modified Wed, 16 Aug 2023 02:49:36 GMT )
Aug 16, 2023 02:49 UTC
  • Mapigano ya utumiaji silaha yaanza tena katika mji mkuu wa Libya, Tripoli

Msemaji wa masuala ya dharura na utoaji misaada nchini Libya ametangaza kuwa mapigano ya utumiaji silaha yameanza tena katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Osama Ali amesema, baada ya utulivu wa kiwango fulani uliokuwepo hapo kabla, mapigano ya utumiaji silaha yalizuka katika mji wa Tripoli kuanzia jana asubuhi kati ya Kikosi cha 444 cha askari wa miguu na kitengo cha uzuiaji hujuma cha vikosi viwili vinavyohusishwa na Makao Makuu ya jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya.
 
Osama Ali ameongeza kuwa, katika mapigano hayo, idadi ya majeruhi iliyojumuisha raia na wanamgambo wa makundi hayo mawili yenye mfungamano na Makao Makuu ya Jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa imefikia watu 20.

Msemaji huyo wa masuala ya dharura na utoaji misaada nchini Libya amebainisha kuwa mapigano hayo yamesababisha pia vifo vya watu kadhaa, lakini idadi yao bado haijajulikana.

 
Mapigano hayo yaliyopamba moto jana Ijumaanne, yalianza Ijumaatatu usiku kufuatia kutiwa nguvuni Mahmoud Hamza, kamanda wa Kikosi cha 444 cha askari wa miguu na maafisa wa Idara ya Operesheni na Usalama wa Mahakama inayohusishwa na Kitengo cha uzuiaji hujuma.
 
Libya imekumbwa na vita na machafuko ya kisiasa tangu mapinduzi ya 2011 ya wananchi, yaliyopelekea kupinduliwa serikali ya kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Muammar Gaddafi kwa uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo.../

Tags