Jun 17, 2024 03:22 UTC
  • Saddam Haftar ateuliwa kuwa mkuu wa jeshi la Libya

Saddam Haftar mtoto wa Khalifa Haftar mbabe wa kivita nchini Liibya ameteuliwa kuwa mkuu wa jeshi la nchi hiyo.

Mbabe wa kivita mashariki ya Libya, Khalifa Haftar, amemteua mmoja wa wanawe wa kiume Saddam Haftar kuhudumu katika wadhifa wa mkuu wa jeshi hatua inayoifanya familia yake kuchukua zaidi udhibiti wa eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.

Saddam ni mmoja wa vijana sita wa kiongozi huyo, anayehudumu katika nyadhifa tofauti katika eneo hilo suala ambalo weledi wa masuala ya kisiasa wanaiona kama mipango ya mbabe huyo wa kivita kuwaandaa wanawe kumrithi.

Pia wameonya kuwa hatua hii inazidisha zaidi mpasuko katika taifa hilo la kaskazini mwa Afrika ambalo limekumbwa na machafuko tangu kuangushwa kwa kiongozi wake Kanali Muammar Gaddafi mwaka wa 2011 katika uasi ulioungwa mkono na Shirika la Kijeshi la NATO.

Khalifa Haftar

Mwezi Juni, Jenerali Saddam Haftar, 33, alichukua wadhifa wa mkuu wa wafanyakazi katika jeshi la ardhini la Libyan Arab Armed Forces chini ya uongozi wa Haftar.

Kakake Saddam,  Khaled, alitajwa mwezi Julai kuhudumu katika wadhifa wa mkuu wa wafanyikazi katika vitengo vya usalama ndani ya  LAAF. Libya yenye utajiri wa mafuta imegawanyika kati ya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa katika mji mkuu Tripoli magharibi na utawala hasimu unaoungwa mkono na Khalifa Haftar ambao unatawala kutoka Benghazi na Tobruk mashariki.

 

 

 

Tags