Waliouawa katika mapigano ya pande hasimu za jeshi Libya wafika 55
(last modified Thu, 17 Aug 2023 03:16:18 GMT )
Aug 17, 2023 03:16 UTC
  • Waliouawa katika mapigano ya pande hasimu za jeshi Libya wafika 55

Idadi ya waliouawa katika mapigano baina ya pande mbili hasimu za kijeshi katika mji mkuu Libya, Tripoli imeongezeka na kufikia watu 55.

Shirika la habari la Press TV limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mbali na watu 55 kuuawa, wengine wengi wamejeruhiwa kwenye mapigano hayo yanayoripotiwa kuwa mabaya zaidi kushuhudiwa nchini humo mwaka huu 2023.

Kwa mujibu wa msemaji wa masuala ya dharura na utoaji misaada nchini Libya, Osama Ali, baada ya utulivu wa kiwango fulani uliokuwepo hapo kabla, mapigano ya utumiaji silaha yalizuka katika mji wa Tripoli kuanzia Jumanne alfajiri kati ya Kikosi cha 444 cha askari wa miguu na kitengo cha uzuiaji hujuma cha vikosi viwili vinavyohusishwa na Makao Makuu ya jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya.

Mapigano hayo yaliyopamba moto juzi Jumanne, yalianza Jumatatu usiku kufuatia kutiwa nguvuni Mahmoud Hamza, kamanda wa Kikosi cha 444 cha askari wa miguu na maafisa wa Idara ya Operesheni na Usalama wa Mahakama inayohusishwa na Kitengo cha uzuiaji hujuma.

Hata hivyo shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa kamanda huyo ameachiwa huru. Reuters imenukuu duru za kiusalama zikisema kuwa, Hamza aliachiwa huru Jumanne usiku.

Libya imekumbwa na vita na machafuko ya kisiasa tangu mapinduzi ya 2011 ya wananchi, yaliyopelekea kupinduliwa serikali ya kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Muammar Gaddafi kwa uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo.

Tags